
Lindi. Ili kuongeza uelewa wa sheria za ushindani na taratibu za rufaa katika shughuli za kibiashara, baraza la ushindani Tanzania (FCT) limewakutanisha wafanyabiashara na walaji wa mkoa wa Lindi kuwajengea uwezo kuhusu ushindani na haki za rufaa.
Akizungumza leo Jumatatu ,Machi 2,2026 kwa niaba ya katibu Tawala wa mkoa wa Lindi, katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali watu, Nathalis Linuma amesema mafunzo hayo yatawasaidia wafanyabiashara na wadau wengine kuelewa namna sheria na kanuni za ushindani zinavyofanya kazi, pamoja na nafasi ya FCT katika kusikiliza na kutatua migogoro ya kibiashara.
Pia mafunzo hayo yatasaidia kuongeza ushindani wenye tija, kukuza uzalishaji, kupunguza migogoro ya kibiashara, kuboresha utoaji wa huduma na uwajibikaji sokoni.
“Mafunzo haya yatakwenda kuwa chachu kwenu kwa kuongeza uzalishaji pamoja na kuweza kupunguza migogoro ya kibiashara,” amesema Linuma.
Kaimu Msajili wa Baraza la ushindani Kunda Mkenda amesema mafunzo hayo yamelenga kutoa elimu kuhusu mfumo wa rufaa unaotumika pale kunapotokea malalamiko yanayohusiana na mwenendo usio na haki sokoni, ikiwemo katika sekta za miundombinu na huduma nyingine za kibiashara.
“Baraza la Ushindani linajukumu la kusikiliza na kutatua migogoro inayotokana na mienendo isiyo ya haki katika soko, ikiwemo huduma za miundombinu na masuala ya kibiashara kupitia mfumo wa rufaa,” amesema Mkenda.
Naye Ofisa Tehama kutoka baraza la ushindani Tanzania (FCTA) Athumani Juma amesema kuwa baraza hilo limejikita kwenye matumizi ya tehama katika kurahisisha ufikiwaji wa haki, ikiwa pamoja na kufungua kesi za rufaa kimtandao.
“Baraza hili limejikita zaidi katika matumizi ya tehema nakurahisisha ufikiwaji wa haki ikiwa pamoja na kufungua kesi za rufaa kimtandao,” amesema Juma.
Angel Kessy mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo amesema kuwa elimu walijoipata imewasaidia kutambua uelewa wa haki na wajibu wao ilikuweza kupunguza migogorona kuongeza ushindani wenye tija pamoja na kulinda maslai yao.
“Mafunzo haya yatatusaidia kutambua na kuelewa umuhimu wa haki na wajibu ilikuweza kupunguza migogoro na kuongeza ushindani wenye tija,” amesema Kessy.