
Rais wa Colombia, Gustavo Petro, ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kijeshi nchini Palestina, akisisitiza haja ya kuundwa kwa jeshi la kimataifa kwa ajili ya “kuikomboa Palestina” na kupinga “udikteta na utawala wa kiimla” unaoenezwa na Marekani na NATO.
Petro alitoa wito huo katika hotuba yake mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne, akizihimiza nchi zinazopinga mauaji ya halaiki kuungana kama muungano madhubuti wa kimataifa ili kulinda maisha ya watu wa Palestina.
Amesema: “Tunahitaji jeshi lenye nguvu kutoka kwa nchi ambazo hazikubali mauaji ya kimbari. Ndiyo maana naziomba nchi za dunia na watu wake, zaidi ya yote kama sehemu ya ubinadamu, kuunganisha silaha na majeshi. Ni lazima tuikomboe Palestina.”
Petro alisisitiza zaidi kuwa huu si wakati wa maneno bali wa vitendo, akionya kuwa “hawatabaki tu kulipua Gaza, wala Karibiani kama wanavyofanya tayari, bali watalenga ubinadamu wote unaodai uhuru.”
Aidha, alieleza wasiwasi wake kuwa hatua za Washington na NATO zinadhoofisha demokrasia na kuchochea kurejea kwa udikteta na utawala wa kiimla duniani, akisisitiza haja ya kuinua bendera ya uhuru duniani.
Wito wa Petro wa kuchukua hatua za kijeshi Palestina ulilingana na pendekezo la Rais wa Indonesia, Prabowo Subianto, ambaye alieleza utayari wake wa kutoa wanajeshi 20,000 kwa kikosi cha kijeshi kitakachoweza kutumwa Gaza.
Oktoba 7, 2023, Israel ilianzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza, kufuatia operesheni ya kushtukiza ya wapiganaji wa Palestina iitwayo “Kimbunga cha A-Aqsa” dhidi ya utawala wa Kizayuni, kama jibu kwa kampeni ya miongo kadhaa ya umwagaji damu na uharibifu dhidi ya Wapalestina.
Kuanzia Machi mwaka huu, utawala wa Israel ulifunga mipaka yote ya Gaza, ukizuia kuingia kwa misaada ya kibinadamu na kuzidisha zaidi janga la kibinadamu lililokuwa tayari likiendelea.
Mashambulizi ya utawala huo dhidi ya Gaza yamesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 65,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Katika tukio tofauti siku ya Jumanne, Rais wa Chile, Gabriel Boric, alieleza hamu yake ya kumwona Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akifikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa kutokana na mauaji ya kimbari ambayo anayaendeleza katika Ukanda wa Gaza, akifananisha hali hiyo na matukio ya Balkan na Rwanda.
Amesema: “Nataka Netanyahu na wote waliohusika na mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina wafikishwe mbele ya mahakama ya kimataifa ya haki.”
Boric pia alilaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Qatar na uchokozi wake dhidi ya Iran, akisisitiza haja ya jumuiya ya kimataifa kupambana na chuki na kuimarisha mfumo wa ushirikiano wa kimataifa.