Afrika Kusini imeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kutoa uamuzi rasmi kuwa mauaji ya kimbari yanatekelezwa katika Ukanda wa Gaza, na kuamuru kusitishwa mara moja kwa machafuko hayo, kwa mujibu wa kauli ya Rais wa taifa hilo mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne.

Ramaphosa amesema: “Afrika Kusini imechukua hatua kwa lengo la kuokoa maisha kwa kusisitiza kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki inapaswa kutoa uamuzi kwamba kweli mauaji ya kimbari yanatekelezwa Gaza na kwamba lazima yakomeshwe.”

Aidha amesema: “Tuna jukumu la msingi kuhakikisha na kulinda haki ya watu wa Palestina ya kujitawala,” akiashiria kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel iliyowasilishwa ICJ.

Afrika Kusini iliwasilisha kesi hiyo mwezi Desemba 2023, ikiishutumu Israel kwa kukiuka wajibu wake chini ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari kupitia vitendo vyake dhidi ya Wapalestina Gaza.

Tangu wakati huo, mahakama hiyo imetoa hatua kadhaa za muda kuilazimisha Israel kuchukua hatua za kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari.

Wiki iliyopita, Brazil iliungana na orodha inayoongezeka ya nchi zilizoomba kuingilia kati katika kesi hiyo, ikiwemo Colombia, Mexico, Uhispania, Uturuki, Chile, Ireland na nyinginezo.

Ramaphosa amesema: “Upo mwafaka wa kimataifa unaozidi kuimarika kwamba Israel inatekeleza mauaji ya kimbari Gaza.” Wiki iliyopita Tume Huru ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Maeneo ya Palestina Yanayokaliwa kwa Mabavu, ilitoa ripoti ikithibitisha kuwa Israel imefanya mauaji ya kimbari Gaza.

Kiongozi huyo wa Afrika Kusini pia alisifu mkutano wa kihistoria wa Umoja wa Mataifa uliofanyika Jumatatu kuhusu suluhisho la kadhia ya Palestina.

Alisema mkutano huo umeakisi azma ya wingi wa mataifa duniani, 142 kwa sasa, ambayo yametangaza kuwa Wapalestina wanastahili kuwa na taifa huru.

Amesema” Nchi nyingi duniani zinatoa wito huo, na huo ndio ujumbe tunaamini Israel inapaswa kuusikiliza.”

Kwa tangazo hilo la karibuni, idadi ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinazotambua rasmi taifa la Palestina imefikia 159 kati ya 193.

Tangu Oktoba 7, 2023, Israel imekuwa ikitekeleza mauaji ya kimbari Gaza, ambapo zaidi ya Wapalestina 65,000 wameuawa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Kampeni hiyo ya kijeshi imeharibu vibaya eneo hilo na kusababisha njaa kali.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *