YANGA inaendelea na mikakati ya kuhakikisha mpira wa miguu hapa nchini unakua na kutengeneza vijana waliopitia njia sahihi za kulelewa katika misingi inayotakiwa ili kuzitimiza ndoto zao.

Hivi karibuni, klabu hiyo ilitangaza programu ya Yanga Soccer School, ambapo awamu hii umeongezeka udhamini wa GSM Foundation ili kuwasaidia vijana wasiokuwa na uwezo kifedha lakini wana vipaji ambao wanatamani kujiunga na program hiyo.

Klabu hiyo imetangaza Machi 8, 2026 kutafanyika skauti maalumu ya kuwatambua vijana na kuwachuja wenye uwezo wa juu katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam, watakaofuzu ndio wataendelea na programu hiyo.

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, alisema kabla ya skauti hiyo, leo ulianza kufanyika usaili utakaodumu siku nne ukifanyika katika makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Jangwani, Dar es Salaam kuanzia saa 4:00 asubuhi.

“Vijana watakaochukuliwa ni kuanzia umri wa miaka 15 hadi 17, masharti ni vyeti vya kuzaliwa, waambatane  na wazazi au walezi, wakikosekana waende na barua za wazazi za kuridhia pamoja na barua ya viongozi wa mtaa.

“Tumeweka siku nne ili kuwapa fursa watu wa mkoani, lengo ni kukuza vipaji vya Tanzania, hii programu haina ujanjajanja,” alisema Kamwe.

“Wataalamu wanafundisha Yanga B kwa maana ya wachezaji wenye umri chini ya miaka 17 ni wengine na wanaoendesha programu ya Yanga Soccer School ni wengine, hapo ni vitu viwili tofauti, lakini wote wana fursa ya kuitumikia Yanga.”

Kwa upande wa meneja wa udhamini huo, Faith Gugu amesema: “Tumefuatilia Yanga ilipozindua programu, tulipoona kuna gharama ambazo wazazi hawawezi kumudu tumeona tuunge mkono kitu ambacho viongozi wa Yanga wanakifanya na pesa tulizowekeza ni zaidi ya Sh100 milioni.

“Pesa hizo zinatumika katika chakula, usafiri na mavazi ili kuwa sawa na wengine ambao wana uwezo, ili kusiwepo kikwazo cha kuwarudisha nyuma, tunatoa wito kwa makampuni tofauti kusapoti hilo.”

Program hiyo ya Yanga Soccer School, ilizinduliwa rasmi Novemba 15, 2025 ikiwa na lengo la kuandaa wachezaji wa baadaye wa timu ya wakubwa, kuweka mfumo wa kitaaluma wa mafunzo ya soka, kukiletea taifa vipaji vyenye kiwango cha kimataifa na kuhakikisha Yanga ina benchi imara la vijana (academy pathway). Watoto wenye umri kuanzia miaka 5 hadi 17 ndiyo wahusika wakuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *