Dar es Salaam. Je, wajua kuwa Diamond Platnumz na Jason Derulo wamezaliwa mwaka mmoja?, Derulo, mwanamuziki aliyeuza rekodi zaidi ya milioni 250 duniani kote, alizaliwa Septemba 21, 1989, wakati Diamond, mwanzilishi wa WCB Wasafi, alizaliwa Oktoba 2, 1989.
Wamepishana takribani siku 10, Derulo akizaliwa huko Florida, Marekani, wakati Diamond akizaliwa Dar es Salaam, Tanzania. Kila mmoja amekulia katika nchi yake na baada ya miaka 34 wakakutana na kurekodi pamoja.
Cha kushangaza zaidi ni kwamba Derulo alitoka kimuziki mwaka 2009 baada ya kuachia wimbo wake ‘Whatcha Say’ chini ya Beluga Heights, naye Mondi alitoka kimuziki mwaka huo huo wa 2009 kupitia wimbo wake ‘Kamwambie’ chini ya Sharobaro Records.
Ebu fikiria wasanii wawili wanazaliwa mwaka mmoja katika mabara tofauti, mmoja Amerika Kusini na mwingine Afrika, kisha wanakuja kutoka kimuziki mwaka mmoja katika viwanda viwili tofauti, halafu wanakuja kufanya kazi pamoja!.
Sasa baada ya kuandikia wasanii kama Diddy, Sean Kingston na Lil Wayne, ndipo Derulo alitoa wimbo wake, Whatcha Say (2009) uliomtangaza zaidi duniani ukishika namba moja chati ya Billboard Hot 100 ikiwa ni mara yake ya kwanza.
Kwa upande wake Diamond alitoa wimbo, Kamwambie (2009) baada ya msoto mkali wa kimaisha kama kuuza mitumba, na ulifanya vizuri hadi kumuwezesha kushinda tuzo yake ya kwanza ya muziki Tanzania (TMA) kama Msanii Bora Chipukizi 2010.
Na kingine cha kushangaza kati ya wawili hawa ni kwamba albamu zao za kwanza zote zilitoka ndani ya mwaka mmoja, kuna Jason Derulo (2010) yake Derulo, pia Kamwambie (2010) yake Diamond!.
Kwa hiyo, ukitazama tarehe zao za kuzaliwa, mwaka waliotoka kimuziki na ule uliotoa albamu zao za kwanza, ni wazi utahitimisha kuwa maajabu kwa wawili hao walishirikiana katika wimbo uliotikisa, Komasava (2024).
Ikumbukwe Komasava (2024) uliyotayarishwa na S2kizzy kutokea Pluto Republic, ndio wimbo wa kwanza kwa Diamond, na Tanzania kuingia katika chati ya Billboard US Afrobeats Songs, na hadi sasa hakuna wimbo mwingine uliofanya hivyo.