
RAIS mpya wa TBF, Hasheem Thabeet amesema mambo mazuri yanakuja baada ya kuchaguliwa kuliongoza shirikisho hilo la mpira wa kikapu nchini akigusia ligi ya kikapu kupigwa mikoa yote.
Thabeet ambaye ni mchezaji wa zamani wa Ligi ya Mpira wa Kikapu ya NBA alisema ligi ambayo ni maarufu nchini kwa sasa ni ya Dar Es Salaam na anataka kila mkoa uwe na ligi.
“Cha muhimu ambacho ni kikubwa, nitahakikisha ligi inachezwa mikoa yote ya Tanzania na siyo Dar es Salaam peke yake,” alisema Thabeet na kuongeza katika uongozi wake atazileta pia NBA Africa, NBA Academy, BAL na Giants of Africa zifanyike nchini.
Nyota huyo ambaye kwa sasa anakipiga Dar City, aliwashukuru viongozi waliopita kwa kazi kubwa waliofanya ya kuendeleza mchezo wa kikapu.
“Kitu ambacho nitakuja kufanya, ambacho kitakuwa ni tofauti na viongozi waliopita, kwanza nitaanza kuendeleza vitu ambavyo wameacha viongozi hao.
Thabeet aliyewahi kuichezea Memphis Grizzlies katika ligi hiyo, alisema kuhusu timu za taifa, inatakiwa vijana waandaliwe wakiwa wadogo na kutakuwa na program za kuanzia U-13, 15, 18, 21 na wakubwa.
Kocha wa Game Time Squad, Bainazi Wamauza alisema Thabeet anaweza kutufikisha ambako Watanzania wanapopataka.
“Kama Luol Deng aliyewahi kuchezea timu ya Chicago Bulls katika Ligi ya NBA, ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Sudan Kusini, ameifanya nchi hiyo iwe tishio katika kikapu, kwa hili najua Thabeet hatashindwa,” alisema Wamauza.
Katika uchaguzi huo, Thabeet alishinda kwa kura 34 huku mpinzani wake Leonard Benedict akipata kura 25, katika uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa Dodoma Hotel, jijini Dodoma.
Kwa upande wa Makamu wa Rais, nafasi hiyo ilichukuliwa na Mohamed Haruna Kasiji; na upande wa Katibu Mkuu, Mweze Kabida alishinda kwa kura 35, huku mpinzani wake Robert Manyerere akipata kura 25.