WAKATI kumekuwa na mijadala kuanzia mtaani hadi mitandaoni kuhusu kanuni za Ligi Kuu Bara msimu huu ambao zimeonekana kuuma kwelikweli, baadhi yaa mastaa na manahodha wa klabu za ligi hiyo wameshindwa kujizuia na kuzungumza.

Kama hujui, kuna baadhi ya kanuni za Ligi Kuu zinazowahusu moja kwa moja wachezaji lengo likiwa ni kulinda nidhamu ya mechi na soka kwa ujumla, ambapo kutokana na hilo baadhi ya mastaa wamezizungumzia kwa namna tofauti.

Kanuni inayozungumzia majukumu ya manahodha uwanjani na inapotokea wachezaji wakayaingilia mara nyingi wanakuwa wanaadhibiwa siyo kwa kuonewa, bali kusimamia kifungu.

Sura ya 1, kanuni ya 1.10 kifungu (d) cha Kanuni za Ligi Kuu 2025 zinampa fursa nahodha kuzungumza na mwamuzi yanapotokea malalamiko uwanjani na inawataka wachezaji wengine kurudi nyuma hatua kumi.

Mwanaspoti limezungumza na manahodha na wachezaji kujua kama wanaijua kanuni hiyo ili kuepuka kufanya kosa wakati wa mechi.

Nahodha wa Namungo, Jacob Masawe alisema japokuwa wachezaji wanafahamu jukumu la kuzungumza na refa ni la kapteni, lakini wanapokuwa na hisia inakuwa ngumu kuvumilia.

“Jambo la kwanza kama nahodha nawatuliza, kisha nawarudisha nyuma ndipo namfuata mwamuzi kuelezea kile tunachokilalamikia. Ukiwatuliza hakuna adhabu, ila wakikomaa na ubishi ndiyo maana unaona kadi zinatolewa. Lakini, niwe mkweli sijazisoma (kanuni), isipokuwa naelekezwa na benchi la ufundi,” alisema.

Nahodha wa Mtibwa Sugar, Oscar Masai alisema inapotokea wachezaji wakamfuata kwa wingi mwamuzi inakuwa ‘damu imechemka’ na jukumu lake ni kuwatuliza na kumfuata mwamuzi ili kutafuta haki ya kile wanachokilalamikia.

“Kanuni zinapotoka makocha wanakaa na manahodha kutuelekeza kama viongozi wa wachezaji. Soka lina sheria zake haiwezi timu nzima ikamvaa refa atamsikiliza nani sasa. Ndiyo maana imewekwa kanuni hiyo ili kuleta nidhamu na amani uwanjani,” alisema.

Mshambuliaji wa Singida Black Stars, Offen Chikola alisema ni mara chache huzisoma kanuni za ligi, lakini anazingatia nidhamu na anatambua nahodha ndiye mwenye jukumu la kuzungumza na mwamuzi.

“Kanuni wanatumiwa viongozi. Mara moja moja huwa nazisoma ninapoziona sehemu ili kujua kipi sipaswi kukifanya. Pia tunaelekezwa kuzingatia kile makocha wanatuambia,” alisema.

Mchezaji wa Tanzania Prisons, George Mpole alisema: “Binafsi natambua jukumu la kuzungumza na waamuzi ni la nahodha. Labda itokee bahati mbaya ‘tempa’ inapokuwa juu. Pamoja na hilo lazima nahodha atatuliza ghasia.”

Mbali na hilo katika kanuni hiyo hiyo kifungu (e) kinasema mchezaji wakati wote anatakiwa atii maagizo ya kocha wake, mchezaji anatakiwa akubali kubadilishwa uwanjani na kuadhibiwa kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu au visivyokuwa vya kiuanamichezo.

Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally alisema: “Mara nyingi tunawaelekeza wachezaji pindi tu kanuni mpya zinapotoka, kwani wasipozingatia hayo ni rahisi kuigharimu timu. Kikubwa nidhamu ni kila kitu katika mpira wa miguu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *