Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametaka ufanyike uchunguzi wa haraka kuhusu shambulio lililolenga skuli ya msingi ya wasichana katika mji wa Minab kusini mwa Iran.

Volker Türk ametaka ufanyike uchunguzi wa haraka kuhusu shambulio la kinyama lililofanywa katika siku ya kwanza ya uchokozi wa pamoja wa kijeshi wa Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya skuli ya msingi ya wasichana mjini Minab lililoua wanafunzi wa kike wasiopungua 167.

Kwa mujibu wa Russia al-Yaum, Türk amesisitiza katika taarifa kwamba “masuulia ya kufanya uchunguzi kwanza kabisa yanabebwa na vikosi vilivyofanya shambulio hilo” na kuvitaka vitangaze matokeo ya uchunguzi huo, kisha mbali na kuwafungulia mashtaka wahusika kufidia maafa yaliyosababishwa dhidi ya waathirika pamoja na familia zao.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, ameashiria pia katika taarifa yake takwimu za Shirika la Hilali Nyekundu la Iran kuhusu idadi ya waliouawa nchini Iran hadi sasa ya watu 787.

Wakati huohuo msemaji Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani amesema, shambulio hilo lililofanywa wakati wa masomo wanafunzi wakiwa madarasani ni la umwagaji mkubwa zaidi wa damu na la uharibifu mkubwa zaidi katika machafuko ya karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Shamdasani ameongeza kuwa, Kamishna wa Haki za Binadamu wa UN ametaka ufanyike uchunguzi wa haraka, kamili na usiogemea upande wowote kuhusu kila kilichotokea katika shambulio hilo…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *