Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera amekubali kushindwa katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo, akimtaja kiongozi wa zamani Peter Mutharika kuwa “mshindi mtarajiwa”.

Katika hotuba aliyotoa kupitia televisheni ya taifa leo Jumatano saa chache kabla ya kutangazwa matokeo rasmi, Chakwera alisema amezungumza na Mutharika kumpongeza.

“Matokeo haya ni taswira ya nia yenu ya pamoja ya kuwa na mabadiliko ya serikali, na hivyo ni vyema nikakubali kushindwa kwa kuheshimu matakwa yenu kama raia na kwa kuheshimu katiba,” Chakwera ameeleza katika hotuba yake hiyo kwa Wamalawi.

Hadi kufikia jana Jumanne Mutharika alikuwa mbele kwa ushindi wa kishindo, akiwa amejinyakulia karibu asilimia 66 ya kura zote zilizokuwa zimeshahesabiwa.

Rais huyo wa zamani wa Malawi mwenye umri wa miaka 85 alikuweko madarakani kuanzia 2014 hadi 2020 aliendesha kampeni za kuahidi kuirejesha nchi hiyo kwenye enzi bora na uongozi wenye uzoefu. Wakati wa uongozi wake, mwanasiasa huyo alisifika na kupata umaarufu kwa kupunguza mfumuko wa bei na kuboresha miundombinu lakini wakosoaji walimshtumu kwa kupendelea jamaa na marafiki zake.

Chakwera, mwenye umri wa miaka 70 na mhubiri huyo wa zamani wa injili alishinda kwa kishindo katika uchaguzi wa marudio wa urais wa mwaka 2020, lakini utawala wake umekumbwa na misukosuko ya kiuchumi ikiwemo mfumuko mkubwa wa bei, uhaba wa mafuta, na kukatika kwa umeme mara kwa mara…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *