
Vikosi vya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vinaendeleza operesheni za ‘Ahadi ya Kweli 4’ ikiwa ni katika kujibu uchokozi wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ulioanzishwa Jumamosi.
Operesheni hizo za kijeshi za Iran zimeendelea kulenga ngome za kijeshi, kiuchumi na kisiasa za utawala wa Kizayuni wa Israel na vituo vya kijeshi na kijasusi vya Marekani katika ardhi za nchi za eneo.
Kikosi cha Baharini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kimetangaza kwamba meli 10 za kubeba mafuta zimeshambuliwa baada ya kupuuza maagizo ya usalama, na sambamba na kutangaza kuwa Lango Bahari la Hormuz liko katika udhibiti kamili wa Iran. Eneo hilo la bahari ni njia ya meli zote za mafuta na biashara zinazotoka katika eneo la Ghuba ya Uajemi.
Kulingana na taarifa ya Shirika la Habari la Mehr katika siku ya tano ya vita, Mkuu wa Kitengo cha Siasa katika Kikosi cha Majini cha IRGC, Kanali Mohammad Akbarzadeh, ametangaza kuwa:
“Ujumbe umeshatumwa katika mtandao wa meli duniani kote, kwamba Lango Bahari la Hormuz, kutoka mwanzo hadi mwisho, lipo katika hali ya vita na hivyo ni hatari kwa meli yoyote. Hadi sasa, meli za mafuta zaidi ya 10, ambazo hazikuzingatia maagizo haya, zimelengwa na kuteketea.”
Ameongeza kuwa: “Hatua hii imesababisha bei ya mafuta kuongezeka kwa kiasi kikubwa katika soko la kimataifa. Ikiwa hali hii itaendelea kwa wiki tatu, uchumi wa dunia utapata mshtuko mkubwa.”
Kwingineko Kamandi ya “Khatam al-Anbia” ya Majeshi ya Iran imetoa onyo kuhusu mpango wa pamoja wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani wa kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa: “Mashambulizi ya Majeshi ya Iran yanalenga tu maadui hao wawili (Marekani na Israel). Ifahamike kuwa nchi jirani na nchi za Kiislamu katika eneo hili hazilengwi na majeshi ya Iran.” Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa inalenga tu vituo vya kijeshi na kijasusi vya Marekani ambavyo viko katika ardhi ya nchi za eneo.
Katika operesheni ya hivi karibuni, ndege zisizo na rubani za “Shahed-136” za Majeshi ya Iran zimelenga kituo cha jeshi la kigaidi la Marekani nchini Bahrain.
Aidha saa chache zilizopita meli ya moja ya kivita ya Marekani iliyokuwa inajaza mafuta kutoka kwa meli ya mafuta ya jeshi la Marekani, ikiwa kilomita 650 kutoka kwenye pwani ya Iran katika Bahari ya Hindi, imelengwa kwa makombora ya “Qadr 380” na “Talaieya” ya cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Kulingana na ripoti ya Shirika la Utangazaji la Iran,, katika Taarifa ya Namba 19 ya Operesheni ya “Ahadi ya Kweli 4”, Jeshi la IRGC limesema
“Operesheni ya Jeshi la Majini la IRGC dhidi ya meli ya kistratijia ya Marekani, iliyokuwa zaidi ya kilomita 600 kutoka Iran katika Bahari ya Hindi, imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
Kulingana na ripoti , moto mkubwa umezuka ndani ya meli hizo mbili na kupelekea moshi mkubwa kutanda katika eneo hilo la bahari.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa itaendeleza operesheni hizo za kulipiza kisasi ili kuwaadhibu vikali maadui walioanzisha uchokozi. Iran ilikuwa imeonya mara kadhaa kuwa shambulizi lolote dhidi yake litawasha moto mkubwa katika eneo la Asia Magharibi.