“Ndoto yetu ya amani iko hatarini,” amesema katika ujumbe wake wa siku hiyo inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Machi.
Ameongeza kuwa “Tishio la matumizi ya silaha za nyuklia sasa ni kubwa kuliko ilivyokuwa katika miongo kadhaa iliyopita.”
Hatari ya nyuklia na matumizi makubwa ya kijeshi
Katibu Mkuu ameonya kuwa ushindani wa kijiografia na kisiasa unasukuma matumizi ya kijeshi kufikia viwango vya juu mno, huku silaha ndogo ndogo na nyepesi zikiendelea kusambaa katika maeneo yenye migogoro.
Wakati huo huo, teknolojia mpya zinaongeza ukali na maangamizi ya vita vya kisasa.
“Mivutano ya kimataifa inasukuma matumizi ya kijeshi kufikia viwango vya juu sana. Silaha ndogo ndogo na nyepesi zinaenea. Na teknolojia mpya zinafanya migogoro kuwa ya mauti zaidi,” amesema.
Kauli zake zinaakisi wasiwasi unaoongezeka katika jumuiya ya kimataifa kuhusu kudhoofika kwa mifumo ya udhibiti wa silaha na kurejea kwa hofu ya makabiliano ya nyuklia.
Wito wa kuchukua hatua
Ametoa wito wa dharura kwa viongozi wa dunia kuchukua hatua za kupunguza mvutano kabla hali haijawa mbaya zaidi.
“Ni lazima tupunguze joto la mvutano,” amesisitiza Guterres. “Nawasihi viongozi warudi nyuma kutoka ukingoni. Acheni vitisho vya nyuklia. Simamisheni mashindano ya silaha.”
Ameeleza kuwa usalama wa kweli haupatikani kwa kuongeza silaha, bali kwa diplomasia, uwajibikaji na kutekeleza kikamilifu wajibu wa kupokonya silaha.
“Ni wakati wa kuwekeza katika miundombinu ya amani, si katika zana za vita,” amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa kwa msisitizo.
Ni katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York, Sanamu iliyokunjwa mtutu wake inaashiria kupinga machafuko na
kuunga mkono amani.
Kujenga upya miundombinu ya amani
Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa kujenga tena uaminifu miongoni mwa mataifa na kuimarisha mifumo ya kimataifa inayozuia ueneaji, majaribio na matumizi ya silaha hatari.
Tangu kuanzishwa kwake, Umoja wa Mataifa umeweka kupokonya silaha na kudhibiti silaha kuwa kiini cha juhudi zake za kulinda amani na usalama wa kimataifa.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Silaha za maangamizi makubwa hasa za nyuklia zinaendelea kuwa chanzo kikuu cha wasiwasi kutokana na uwezo wake wa kusababisha maafa makubwa kwa binadamu.
Mbali na tishio la nyuklia, mkusanyiko kupita kiasi wa silaha za kawaida na biashara haramu ya silaha ndogo ndogo vinahatarisha amani na maendeleo endelevu.
Matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yenye watu wengi yanaweka raia katika hatari kubwa, huku teknolojia mpya kama silaha zinazojiendesha zikiibua changamoto mpya za kimaadili na kiusalama.
Kukuza uelewa, hususan kwa vijana
Kupitia azimio A/RES/77/51, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilianzisha Siku hii ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu mchango wa kupokonya silaha katika kuimarisha amani, kuzuia na kumaliza migogoro ya silaha, na kupunguza mateso ya binadamu yanayosababishwa na silaha.
Azimio hilo linazialika nchi wanachama, mashirika ya Umoja wa Mataifa, asasi za kiraia, taasisi za elimu, vyombo vya habari na watu binafsi kuadhimisha siku hii kupitia shughuli za kielimu na kampeni za uhamasishaji.
Akihitimisha ujumbe wake kwa matumaini, Katibu Mkuu amesema hatua za pamoja ndizo ngao bora dhidi ya maafa.
“Kwa pamoja, tunaweza kuzuia majanga na kuhakikisha dunia salama na yenye amani kwa wote.”