Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iitwayo “Kuhakikisha na Kuimarisha fursa ya Haki ya Kisheria kwa Wanawake na Wasichana wote,” msemaji wa UN Women amesema “Hakuna nchi duniani iliyofanikiwa kufikia usawa kamili wa kisheria kati ya wanawake na wanaume.”

 Amesisitiza kuwa ubaguzi wa kisheria bado umejikita katika mifumo mingi ya sheria duniani.

Sarah Hendriks naibu mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, UN Women

Sarah Hendriks naibu mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, UN Women kuhusu sera

Mapungufu ya sheria bado yapo duniani

Akizungumza na waandishi wa habari, Sarah Hendriks, Mkurugenzi wa Sera, Programu na Masuala ya Kiserikali katika UN Women, ameeleza kuhusu takwimu kadhaa zinazotia wasiwasi kuhusu hali ya sheria zinazohusu wanawake na wasichana.

“Zaidi ya nusu ya nchi duniani hazifafanui ubakaji kisheria kwa kuzingatia ridhaa,” amesema Hendriks.

Ameongeza kuwa ulinzi wa kisheria bado ni dhaifu katika nchi nyingi, “Takribani robo tatu ya nchi duniani, yaani asilimia 74, bado zinaruhusu ndoa za utotoni kisheria, hivyo kuruhusu wasichana kuolewa wakiwa watoto. Na katika asilimia 44 ya nchi duniani, sheria hazilazimishi malipo sawa kwa kazi yenye thamani sawa.”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mapungufu hayo ya kisheria yanaendelea kuwanyima mamilioni ya wanawake na wasichana haki ya kupata usawa na haki zao.

Picha ya ukuta yenye nguvu katika Cox's Bazar inaonyesha wanawake wa Rohingya wakitumia simu za mkononi na kutabasamu, ikiashiria ujasiri na mshikamano katikati ya mgogoro wa kibinadamu unaoendelea.

© UN Women/Sanjida Rahman

Mchoro wa ukutani uliokamilika katika Kituo cha Wanawake cha Multi-purpose katika Cox’s Bazar.

Ukiukwaji wa haki na kutowajibika vinaongezeka

Hendriks ameonya kuwa ukiukwaji wa haki za wanawake na wasichana unaongezeka duniani, ukichochewa na utamaduni unaokua wa kutowajibika kwa wahusika pamoja na upinzani dhidi ya usawa wa kijinsia.

“Duniani kote leo, ukiukwaji wa haki za wanawake na wasichana unaongezeka katika mazingira ya utamaduni unaokua wa kutokuwajibika,” amesema.

Amesema tatizo hilo halipo tu katika mahakama bali pia katika maeneo ya migogoro na hata kwenye majukwaa ya kidijitali. 

“Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita pekee, asilimia ya wanawake na wasichana wanaokuwa waathirika wa ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro imefikia asilimia 87.”

Majukwaa ya mtandaoni pia yanazidi kuwa hatari kwa wanawake. Hendriks amesema teknolojia za kidijitali zinatumika vibaya kama silaha za kuwanyanyasa wanawake.

“Teknolojia za kidijitali zinageuzwa silaha kupitia unyanyasaji, matusi na hata matumizi ya picha na video zilizobadilishwa au deepfakes yanayowanyamazisha wanawake na kuwalazimisha kujiondoa kwenye majukwaa ya mtandaoni, na mara nyingi wahusika hawachukuliwi hatua zozote,” amesema.

Mama wa jamii ya rendile akiwa na watoto wake Marsabit Kaskazini Mashariki mwa Kenya, baada ya kupokea msaada wa chakula

Khoboso HarguraAdichareh/KPL

Mama wa jamii ya rendile akiwa na watoto wake Marsabit Kaskazini Mashariki mwa Kenya, baada ya kupokea msaada wa chakula

Mifumo ya haki inaweza kubadilika

Licha ya changamoto hizo, Hendriks amesisitiza kuwa mageuzi ya kisheria yanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wanawake ikiwa yatatekelezwa ipasavyo.

“Mfumo wa haki unaoshindwa kulinda nusu ya watu wa dunia hauwezi kudai kuwa unaleta haki,” amesema. “Hata hivyo, mifumo ya haki inaweza kubadilika na kujibadilisha, na inapofanya hivyo, athari zake huwa za mabadiliko makubwa.”

Amebainisha kuwa mageuzi ya sheria za familia tayari yameleta matokeo chanya kwa mamilioni ya wanawake.

Ameeleza kuwa “Kwa kweli, tangu mwaka 1970, mageuzi ya sheria za familia yamesababisha zaidi ya wanawake milioni 600 kupata fursa mpya za kiuchumi, yote kutokana na mabadiliko ya sheria za familia”.

Wanawake watatu walishiriki katika mazungumzo huko Nagladh, wilaya ya Jajarkot, Nepal, kama sehemu ya majibu ya UNFPA kwa tetemeko la ardhi, wakisisitiza juhudi za kusaidia wanawake na wasichana katika eneo lililoathirika.

Wasichana nchini Nepal.

Wito wa hatua katika mkutano wa CSW70

Ripoti hiyo pia inaonya kuwa katika baadhi ya maeneo sheria zinarekebishwa kwa njia zinazopunguza uhuru wa wanawake, kunyamazisha sauti zao na kuruhusu ukatili kuendelea bila adhabu.

Hendriks ametoa wito kwa serikali na watunga sera kuchukua hatua za kukabiliana na hali hiyo.

“Tunajua kinachofanya kazi, ushahidi upo,” amesema. “Swali lililo mbele ya Kamisheni ya Hali ya Wanawake CSW70 ni kama tutakabiliana na kutokuwajibika na kuwekeza katika mifumo ya haki inayoweza kuleta usawa katika sheria na katika maisha halisi.”

Ripoti hiyo inaonya kuwa bila ulinzi thabiti wa kisheria na upatikanaji wa haki kwa wote, mamilioni ya wanawake na wasichana wataendelea kuwa katika hatari ya unyanyasaji, ubaguzi na ukosefu wa usawa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *