Lakini sasa mafunzo ya haki ya kumiliki ardhi yanayotolewa na Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake WLAC, nchini humo yanaanza kubadili fikra hizo yakileta ushirikiano mpya ndani ya familia na kufungua milango ya maendeleo. Flora Nducha anatuletea hadhithi ya mke na mume waliofaidika na mafunzo hayo.

Jovita Provius, kutoka wilaya ya Muleba mkoani Kagera Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, mafunzo hayo ya WLAC yamebadilisha kabisa mtazamo wake kuhusu nafasi ya mwanamke katika kumiliki mali ikiwemo ardhi.

“Nilishiriki mafunzo nikagundua kumbe na mwanamke anaweza kumiliki ardhi. Kabla ya hapo nilikuwa najua mwanamke hawezi kumiliki ardhi.”

Ugunduzi huo haukuishia kwenye fikra pekee. Baada ya mafunzo hayo, Jovita na mume wake waliamua kubadilisha namna wanavyoendesha maisha yao ya familia kwa kushirikiana zaidi katika maamuzi na kazi.

“Baada ya kutoka kwenye mafunzo mimi na mume wangu tukashirikiana, tukaanza kufanya kazi pamoja na muda si muda tukapata kiwanja tukakinunua. Sasa hivi tunaendelea na ujenzi wa nyumba yetu.”

Hadithi kama hiyo inaungwa mkono na mume wake Provius Katumbi, ambaye anakiri kwamba kabla ya mafunzo alikuwa haoni umuhimu wa kumshirikisha mke wake katika maamuzi ya mali ya familia.
“Kwa upande wangu nilikuwa simshirikishi mke wangu. Mambo yangu nilikuwa nafanya peke yangu. Lakini niliposikiliza mafunzo yale nilipata mwanga nikaanza kumshirikisha mke wangu.”

Mabadiliko hayo hayakuishia kwenye ushirikiano wa kifamilia pekee. Katumbi anasema hata mwenendo wa maisha yake umebadilika sasa akiweka kipaumbele kwa maendeleo ya familia badala ya tabia zilizokuwa zinapoteza muda na fecha na shukran zake ni kwa mkewe na WLAC
“Namshukuru kweli na mpaka sasa nashukuru sana hili shirika la WLAC kuja. Nitashukuru sana kama shirika linaweza likaja hata siku nyingine , kwa sababu nilivyppata elimu na mwingine anaweza kubhatika kuipata hii elimu.”

Asante WLAC kwani kwa familia hii, elimu waliyopata kuhusu haki ya kumiliki ardhi imekuwa mwanzo wa safari mpya ya usawa, ushirikiano na matumaini ya maisha bora.
Ujumbe hapa ni mmoja, elimu kama hii ikiendelea kufika kwa jamii, inaweza kubadilisha sio tu mitazamo, bali pia mustakabali wa familia nyingi vijijini na kutoa haki zaidi kwa wanawake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *