
Juhudi hizi zinawasaidia akina mama kuboresha ustawi wa watoto wao na kuhakikisha wanapata afya bora katika ukuaji wao.Esther ni mama wa watoto sita na ni mnufaika wa programu hii, anaeleza jinsi inavyosaidia watoto wake.
“Kati ya watoto wangu sita, ni mmoja tu aliyelizaliwa hospitalini kwa sababu sikuwa najua faida zake. Sikuwa nimepewa taarifa kamili. Lakini tangu tulipopata Wahamasishaji wa Afya ya Jamii, nilielewa na nimemlea mtoto wangu mchanga vizuri. Afya yake ni njema na hajaugua mara nyingi kama watoto wangu wengine, na nilifunzwa kuwa kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa miezi sita kabla ya kuanza kumpa chakula kingine ni muhimu sana. Magonjwa yamepungua kwa sababu ya mafunzo kutoka kwa wahudumu wa afya ya jamii. Nimejifunza mengi kutoka kwao na nimemlea vizuri sasa afya yake iko sawa”
Alex Loteng ni mhudumu wa mradi huo na anaeleza umuhimu wake kwa wanajamii wa Kaunti ya Samburu. “Mradi wa Jumuiya Rafiki kwa Watoto BFCI ni mpango unaolenga kusaidia na kuhamasisha akina mama na watoto ili kuhakikisha wanapata lishe bora ya mama na ya watoto wachanga. Katika jamii ya Karoni wahudumu wa afya ya jamii wanatekeleza maeneo mbalimbali, mojawapo ni lishe ya wakina mama ambapo wanawaunga mkono kuhakikisha wanahudhuria kliniki ya wajawazito ambako hupokea huduma mbalimbali ikiwemo virutubisho..”
Akiendelea mhudumu huyo anasema kuwa “baada ya kujifungua, tunahakikisha mtoto ananyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya kwanza. Kuna pia kipengele cha ulishaji wa nyongeza baada ya miezi sita ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee, ambapo mtoto huanza kutambulishwa kwa vyakula vingine. Kupitia hatua hizo.”
Alex Loteng anaeleza kuwa mpango huu umeanza kuwapatia matumaini jamii kwa kuwa . “tumeweza kuona matokeo chanya. Hapo awali kulikuwa na visa vingi vya akina mama kujifungulia nyumbani, lakini baada ya kuanzishwa kwa mpango huu tumeona mabadiliko – kuwahusisha akina baba, kwa kuwa katika jamii hii wanaume ndio wanaofanya maamuzi.Kupitia ushirikishwaji huo, tumeona wanaume wakitoa ushirikiano na kutambua kuwa nao wana jukumu muhimu.”
Kando na lishe bora kwa mtoto, UNICEF na wadau wake wanaendesha mafunzo inayolenga kuwahimiza kinamama kuhakikisha wamenyonyesha watoto wao kwa miezi sita ya mwanzo mfululizo.
Wycliffe Abade ni afisa wa Shirika la Helen Keller International anasisitiza kuwa “Kwa kutekeleza mpango wa Jumuiya Rafiki kwa Mtoto, tunalenga kuunda mazingira wezeshi yanayolinda, kuhimiza na kuendeleza unyonyeshaji bora na ulishaji wa nyongeza. Hadi sasa, tumefunza vitengo 44 vya afya ya jamii katika Kaunti Ndogo ya Samburu Mashariki. Tunawalenga wahudumu 440 wa afya ya jamii ambao wana jukumu muhimu la kutoa ushauri wa lishe katika ngazi ya kaya, kupitia midahalo ya kijamii na majadiliano ya vikundi, ili kuhakikisha kila mtoto anaanza maisha kwa njia bora zaidi.”