Katika mazungumzo ya Kikanda kuhusu hali ya janga la VVU na mwitikio wa UKIMWI katika ukanda huo, yaliyoandaliwa na UNAIDS, washiriki walisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushiriki wa kimkakati ili kuhakikisha mwitikio uliofanisi zaidi, endelevu na ulioratibiwa dhidi ya VVU.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Angeli Achrekar, amesema mwaka huu unatoa fursa ya kipekee kwa washirika wa kimataifa kuimarisha juhudi za kukabiliana na VVU.
“Mazungumzo haya ya kikanda yanafanyika wakati ambapo kuna maendeleo makubwa ya kijamii; kwa mfano, umri wa kuishi barani Afrika umeongezeka kwa miaka 20 tangu mwaka 2000. Mwaka huu pia tunayo fursa muhimu ya kisiasa ya kuhamasisha hatua za pamoja kwa kuongozwa na Mkakati mpya wa Kimataifa wa UKIMWI wa 2026–2031 ili kukomesha UKIMWI,” amesema Achrekar.
Mandisa Dukashe na familia yake ni wakazi wa Eastern Cape, Afrika Kusini. Mandisa ni muuguzi na anahusika na udhibiti wa VVU na yeye mwenyewe anaishi na VVU. Lakini mumewe na binti zake wamepima VVU na hawana virusi hivyo.
Maendeleo katika mwitikio dhidi ya VVU
Ukanda wa Afrika Magharibi na Kati umeonyesha maendeleo muhimu katika mwitikio dhidi ya UKIMWI katika miaka ya hivi karibuni.
Takwimu za UNAIDS zinaonyesha kuwa mwaka 2024, asilimia 81 ya watu wanaoishi na VVU walikuwa wanajua hali yao ya maambukizi, asilimia 76 walikuwa wanapata matibabu ya dawa za kupunguza makali ya virusi (ARV), na asilimia 70 walikuwa wamefikia kiwango cha kudhibiti virusi mwilini, hatua inayosaidia kuzuia maambukizi mapya.
Kati ya mwaka 2010 na 2024, kulikuwa na upungufu wa asilimia 55 wa maambukizi mapya ya VVU katika ukanda huo na kupungua kwa asilimia 60 kwa vifo vinavyohusiana na UKIMWI.
Hata hivyo, UNAIDS imesema mafanikio hayo bado hayatoshi kufikia malengo ya kimataifa ya kumaliza UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.
“Janga la VVU bado halijaisha. Mwaka jana pekee lilisababisha vifo vya watu 124,000 katika ukanda huu na katika angalau nchi tano za Afrika Magharibi, Kati na Kaskazini, maambukizi mapya ya VVU yanaendelea kuongezeka,” amesema Susan Kasedde, Mkurugenzi wa Kanda wa UNAIDS kwa Afrika Magharibi na Kati.
Tofauti za kikanda zinaonesha mafanikio yanawezekana
Takwimu kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini zinaonesha kuwa maendeleo ya haraka zaidi yanawezekana.
Katika ukanda huo, asilimia 93 ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali yao ya maambukizi, asilimia 84 wanapata matibabu, na asilimia 80 wamefanikiwa kudhibiti kiwango cha virusi mwilini.
Matokeo hayo yanaonesha kuwa kufikia malengo ya mwaka 2030 yaani asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU kujua hali yao, asilimia 90 kupokea matibabu, na asilimia 86 kudhibiti virusi mwilini inawezekana.
Washiriki wa mkutano huo walisisitiza umuhimu wa kuimarisha dhamira ya kisiasa na ushiriki wa wadau ili kuharakisha maendeleo, kuziba mapengo yaliyopo na kumaliza UKIMWI katika ukanda huo.
“Nyuma ya takwimu hizi bado kuna udhaifu mwingi na mapengo makubwa katika huduma za kinga, upimaji na matibabu,” amesema Saffiatou Thiam, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya UKIMWI nchini Senegal.
Ukosefu wa usawa bado changamoto
Katika Afrika Magharibi na Kati, maendeleo pia yanakwamishwa na ukosefu wa usawa unaoendelea kuwepo.
Tofauti hizo zinaonekana kati ya nchi na ndani ya nchi, ikiwa ni pamoja na tofauti za kijiografia, wilaya, jinsia, makundi ya umri na makundi ya watu, hali inayopunguza ufanisi wa hatua zinazochukuliwa na kutishia mafanikio ya juhudi za kumaliza UKIMWI.
“Ili kufikia mwaka 2030, nchi lazima zichukue hatua madhubuti kulinda makundi yaliyo hatarini zaidi,” anasema Magatte Mbodj kutoka shirika la Alliance Nationale Contre le SIDA nchini Senegal.
Jumuiya na mitandao iliyopangwa kuhamasisha watu ina jukumu kubwa katika kuzuia VVU, na kufuatilia makundi muhimu.
Mkakati mpya wa kimataifa
Mazungumzo hayo ya Kikanda yanafanyika wakati muhimu kwa mwitikio wa kimataifa dhidi ya VVU.
Mkakati mpya wa Kimataifa wa UKIMWI wa 2026–2031 umeandaliwa hivi karibuni na unaweka vipaumbele vitatu vya kimkakati: kudumisha mwitikio kupitia mifumo imara inayoongozwa na nchi, kuweka watu katikati ya juhudi za mwitikio kwa kuhakikisha usawa na upatikanaji wa huduma, na kuwezesha jamii kuongoza na kuunda mwitikio dhidi ya VVU.
Mkutano huo pia unafanyika kabla ya mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) kuhusu VVU/UKIMWI unaotarajiwa kufanyika mwezi Juni 2026, ambao unalenga kuimarisha dhamira ya kimataifa na kupitisha tamko jipya la kisiasa litakaloongoza juhudi za kukabiliana na UKIMWI katika miaka mitano ijayo.
Akizungumza katika mkutano huo, Adama Bocar Soko, Naibu Mwakilishi Mkazi anayeshughulikia Operesheni katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), amesema Afrika inapaswa kutumia fursa hiyo kuimarisha uongozi wa kisiasa wa ukanda na kusukuma mbele malengo ya kikanda yanayotekelezeka na yenye ufadhili wa kutosha.