
SERIKALI ya Tanzania inatarajia kuiuzia mahindi Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ili kusaidia nchi hiyo kukabiliana na uhaba wa chakula.
Hatua hiyo imekuja kufuatia ziara iliyofanywa na Serikali ya Tanzania nchini humo. Leo, ujumbe wa Serikali ya DRC umetembelea Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili kuona akiba ya mahindi pamoja na ziada iliyopo kwenye maghala ya wakala huo.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Mkurugenzi wa NFRA, Dk. Andrew Komba amesema wakala ataendelea kuhifadhi akiba ya kutosha ya mahindi ambayo inaweza kusaidia pia soko la nje. SOMA: Tanzania kuendelea kuuza mahindi Malawi
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya NFRA John Ulanga, amesema kutokana na upungufu mkubwa wa takribani tani milioni tatu za unga nchini DRC kuna uwezekano mkubwa wa kufanyika kwa biashara ya mahindi kati ya Tanzania na nchi hiyo endapo pande hizo mbili zitafikia makubaliano.