Simulizi hiyo imechapishwa Machi 12 2026 ikiwa ni makala ya WFP kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Milo Shuleni, ikimwangazia Abdul-Wahab anayekumbuka jinsi njaa ilivyokuwa kikwazo darasani

Kikundi cha watoto wa shule wa Ghana wenye tabasamu wakiwa wamevaa sare za shule wameketi mezani wakiwa na bakuli za chakula, sehemu ya programu ya chakula shuleni.

© WFP/Abdul-Wahab Mohammed

Kwa watoto nchini Ghana, milo ya shule huwapa kiamsha kinywa na chakula cha mchana cha uhakika.

Kupitia wavuti ya WFP, Abdul-Wahab anasema, “nakumbuka asubuhi zenye baridi kali na vumbi la pepo za Harmattan huko Tishegu, kaskazini mwa Ghana, vumbi jepesi lilivyokuwa likitua kwenye madawati yetu, na upepo mkavu uliopiga nyuso zetu tukiwa tunatembea bila viatu au tukiwa na kandambili zilizochakaa kuelekea shuleni.”

Abdul-Wahab ambaye sasa ni Afisa Mawasiliano wa Shirika la WFP nchini Ghana anakumbuka,  “mama yangu alijitahidi kadiri ya uwezo wake kufanya biashara ya nyumba kwa nyumba, lakini katika misimu ambayo chakula kilikuwa haba, kifungua kinywa kilikuwa anasa ambayo hatukuimudu.”

Njaa ilivyokuwa kikwazo darasani akisema, “nilikuwa nikikaa darasani, sauti ya mwalimu ikififia na kurudi huku tumbo langu likiuma kwa njaa. Ubao ulionekana kama una ukungu siku hizo. Kuzingatia masomo kulihitaji nguvu ambazo sikuwa nazo kila wakati.”

Mwanga wa matumaini katika bakuli la plastiki

Tumaini lake pekee lilikuwa ni mlo wa mchana shuleni ambapo wapishi walijaza bakuli lake la kijani la plastiki kwa chakula cha moto. Mlo huo haukuwa chakula tu, bali ulikuwa ni heshima na nishati iliyomwezesha Abdul-Wahab kumaliza elimu yake na kufikia ndoto zake za juu.

Mlo huo ulimaanisha kuwa naweza kuzingatia masomo ya mchana. Ilimaanisha sikutakiwa kuigiza kuwa sikuwa na njaa. Ilimaanisha mama yangu angeweza kupumua kidogo, akijua kwamba angalau mmoja wa watoto wake angekula siku hiyo. Kwa wengi wetu, chakula hicho ndicho kilikuwa sababu ya sisi kubaki shuleni,” amesema Abdul-Wahab.

Mwanamke mweusi Mwafrika anagawa mbegu za mahindi ya manjano kwenye bakuli kubwa, sehemu ya programu ya chakula cha shule nchini Ghana inayoungwa mkono na Shirika la Chakula Duniani (WFP).

© WFP/Abdul-Wahab Mohammed

Mpango wa WFP wa Mlo shuleni unafadhili soko kwa wakulima wadogo, na kutoa ajira kwa wapishi shuleni.

Leo hii, anatumia uzoefu wake kuelezea ulimwengu kuwa kulisha watoto shuleni si msaada wa hiari tu, bali ni uwekezaji mkubwa kwa viongozi wa baadaye. Kwa sasa, WFP ikishirikiana na Serikali ya Ghana inalisha watoto milioni 3, huku ikitengeneza soko la uhakika kwa wakulima wadogo na ajira kwa wanawake wanaopika vyakula hivyo.

Abdul-Wahab anabainisha kuwa huu ni mnyororo wa mabadiliko akisema,“Chakula kinachopikwa hununuliwa kutoka kwa wakulima wadogo, wanaume na wanawake kama wazazi wangu, ambao zamani walipambana kupata masoko ya uhakika. Sasa, mazao hayo yanalisha wanafunzi kutoka kwenye jamii zao wenyewe. Katika majiko hayo, unaona nguvu. Katika mashamba hayo, unaona ustahimilivu. Katika madarasa hayo, unaona uwezekano.”

Afisa Mawasiliano wa WFP Abdul-Wahab Mohammed akiwa na watoto wa shule nchini Ghana.

© WFP/Adul-Wahab Mohammed

Afisa Mawasiliano wa WFP Abdul-Wahab Mohammed akiwa na watoto wa shule nchini Ghana.

Abdul-Wahab anajiona kuwa yeye ni ushahidi hai wa jinsi mlo mmoja unavyoweza kuimarisha jamii na kujenga mustakabali. Anahitimisha kwa kusema, “Najua hisia za kukaa darasani ukipambana na njaa. Najua hisia za kusubiri bakuli hilo lijazwe. Na najua inamaanisha nini kwa milo hiyo kulinda elimu, kuimarisha jamii, na kusaidia kujenga mustakabali wa mlo mmoja baada ya mwingine.”

Mpango huu nchini Ghana unaendelea kuleta matokeo makubwa kutokana na ushirikiano wa karibu na wafadhili mbalimbali ikiwemo nchi ya Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *