Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limesema kuwa zaidi ya watu 822,000 sasa wamejisajili kama wakimbizi wa ndani nchini Lebanon kufuatia kuongezeka kwa mapigano. Takriban watu 128,000 wanahifadhiwa katika karibu vituo 600 vya pamoja vinavyoendeshwa na serikali, ambavyo vingi tayari vimejaa au vinakaribia kujaa.
Mkuu wa Ofisi ya IOM nchini Lebanon, Mathieu Luciano, ameonya kuwa mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka kwa kasi kuliko uwezo wa kuyashughulikia, huku familia zikiendelea kukimbia mashambulizi ya anga na hali ya ukosefu wa usalama.
Ameongeza kuwa, “Mashambulizi dhidi ya familia zilizokimbia makazi yao, kama yale yaliyotokea Beirut usiku wa siku mbili zilizopita, yanaonesha udhaifu mkubwa wa kaya zinazolala kwenye mahema na makazi ya muda ambayo hayatoi ulinzi wa kutosha.”
Shirika hilo pamoja na washirika wake wanaendelea kusambaza chakula, magodoro, mablanketi na msaada wa matibabu, lakini wamesisitiza kuwa upatikanaji salama wa misaada ya kibinadamu na ulinzi wa raia ni muhimu sana.
Majengo yaliyoharibiwa na vifusi huko Khiam, Lebanon, kufuatia mzozo kati ya Israel na Hezbollah.
WFP yalalamikia hofu na msongo wa vita
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Carl Skau, yuko Beirut pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Ameeleza kuhusu kuongezeka kwa kasi kwa mapigano katika mji wa Beirut, ambako amri za kuhama na mashambulizi zimewalazimisha wakazi kukimbia makazi yao.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii X, alisema“Nimewasili Beirut jana usiku wakati mapigano yakiwa yameongezeka sana. Saa 24 zilizofuata zimekuwa ngumu amri za kuhama na mashambulizi kote jijini. Watu wamekumbwa na hofu na msongo mkubwa. Madhara ya kibinadamu yanaongezeka, watu zaidi ya 800,000 tayari wamekimbia makazi yao.”
UNICEF: Idadi ya wakimbizi yaongezeka watoto waathirika zaidi
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa upande wake linaonya kuwa kuongezeka kwa mapigano nchini Lebanon kunasababisha mgogoro wa kibinadamu unaozidi kuwa mbaya haraka, hasa kwa watoto.
Limesema watoto wapatao 91 wameuawa na 275 kujeruhiwa, huku zaidi ya watu 816,000 wakiwemo karibu watoto 286,000 wamekimbia makazi yao, kulingana na takwimu za serikali.
Kwa mujibu wa UNICEF amri za kuhama sasa zinahusu sehemu kubwa za vitongoji vya kusini mwa Beirut, kaskazini mwa Bekaa na maeneo yote kusini mwa Mto Litani, jambo linalowaathiri takriban wakazi 500,000.
Kwa kuwa makazi mengi yamejaa, baadhi ya familia zinalala ndani ya magari au katika maeneo ya wazi, huku shule 344 za umma zikibadilishwa kuwa makazi ya wakimbizi, hali iliyokatiza masomo ya zaidi ya wanafunzi 110,000.
Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa vinasambaza chakula kwa watu waliofurushwa kutoka makazi yao kusini mwa Lebanon.
UNIFIL: Vikosi vya Israel vimeingia hadi kilomita saba ndani ya Lebanon
Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL, umesema hali kusini mwa nchi hiyo imekuwa tulivu kidogo tangu kuongezeka kwa mashambulizi ya makombora na makombora ya masafa marefu kati ya wanamgambo wa Hezbollah na Israel siku mbili zilizopita.
Msemaji wa UNIFIL, Kandice Ardiel, amesema vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) vimeonekana vikiingia hadi kilomita 7 ndani ya maeneo ya kusini mwa Lebanon.
Amewaambia waandishi wa habari hii leo kwamba “Tunashuhudia kila siku mashambulizi ya makombora, makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel na eneo linalokaliwa la Golan kutoka Lebanon, na pia mashambulizi ya mizinga, mashambulizi ya anga na ya ndege zisizo na rubani pamoja na uvamizi wa ardhini hadi kilomita saba ndani ya Lebanon kutoka kwa vikosi vya Israel.”
Hadi tarehe 12 Machi, mamlaka ya Lebanon imeripoti kuwa karibu watu 700 wameuawa na takriban 1,800 kujeruhiwa, aliongeza Bi Ardiel.
Wafanyakazi wahamiaji wajikuta katikati ya mgogoro Mashariki ya Kati
Kwa mujibu wa Shirika la IOM wafanyakazi wahamiaji ni miongoni mwa wale wanaoathirika zaidi na kuongezeka kwa mgogoro katika eneo zima la Mashariki ya Kati.
Mama mmoja ambaye amelazimika kuhama makazi yake kwa sababu ya mgogoro nchini Lebanon anafanya mtoto wake achunguzwe na mfanyakazi wa afya.
Nchini Lebanon, kuna takriban wafanyakazi wahamiaji 200,000, wengi wao wakifanya kazi katika kilimo, ujenzi na kazi za nyumbani.
Inakadiriwa kuwa angalau 30,000 wamekimbia makazi yao, huku baadhi yao wakishindwa au kusita kwenda katika makazi rasmi.
Nchini Iran, IOM inasema wahamiaji wakiwemo idadi kubwa ya raia wa Afghanistan pia wanakabiliwa na hatari zinazoongezeka huku mapigano yakivuruga maisha ya raia.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanatoa msaada wa dharura na yako tayari kusaidia serikali kuratibu uhamishaji salama au kurejesha kwa mpangilio wahamiaji waliokwama.
Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa, kuna karibu wafanyakazi wahamiaji milioni 30 katika eneo kubwa la Mashariki ya Kati.