Katika shule ya Enkasiti, mazingira ya kujifunzia yameanza kubadilika baada ya kuunganishwa na mtandao wa intaneti. Mkuu wa Elimu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF nchini humo, Deema Jarrar, akiwa shuleni hapo ameeleza.
“Mradi huu unalenga kuboresha aina tofauti za ujuzi. Ujuzi wa kidijitali, ujuzi unaohamishika, ili kuwaandaa wanafunzi hawa kwa maisha bora ya baadaye, vilevile tunazungumzia kuboresha matokeo ya kujifunza kwa ujumla katika masomo mbalimbali.”
Upatikanaji wa Intaneti katika elimu nchini Kenya.
Kabla ya mradi huu hali ilikuwaje? Christine Kerubo ni mwalimu wa Teknolojia ya Habari na Mawasilino ICT
“Wakati hakuna intaneti, nilikuwa nanunua data yangu kwa saa moja tu. Nilikuwa nawasimamia data inapoisha nawaambia tutakutana baadaye, lakini kupitia mtandao huu wa intaneti nawaambia tafuteni kuhusu hiki na hiki na mnafanya wenyewe, nitakuja kukagua na wanaweza kufanya hivyo. Kwa hiyo imerahisisha kazi yangu kama mwalimu na nashukuru kwa hilo.”
Naye mwalimu Julius Mwenda wa shule ya Moipei amesema teknolojia hii inawafungulia watoto ulimwengu mpya, hasa wale wanaotoka maeneo ya mbali ambao hawajawahi kuona vifaa hivyo.
“Wanafunzi wanafahamu kujua nini kinatokea ulimwenguni kwa sababu wanaweza kufikia kupitia vifaa hivi. Pia baadhi ya wanafunzi hawajawahi kukutana na vifaa hivi majumbani mwao. Hapa ndipo mahali pekee wanapokuja na kutumia kwa sababu baadhi yao wanatoka katika maeneo ya mbali sana.”
Mradi huu unaofadhiliwa na Muungano wa Ulaya, umeanza kuleta manufaa kwa wanafunzi kwani sasa wanaonesha uwezo mkubwa wa kutumia teknolojia kwa mambo ya kibunifu kama anavyoeleza Lennox Juma.
“Kimsingi nafanya vitu vingi katika maabara yetu ya kompyuta na inafurahisha sana kutengeneza vitu mwenyewe moja kwa moja. Kimsingi tunatengeneza katuni, tunafanya majadiliano, na tunatengeneza magemu.”
Sherry Simaton, ni mwanafunzi katika shule ya Moipei, ambaye anasema uwepo wa intaneti umemsaidia kuwa na ujasiri wakati wa kujifunza.
Mradi huu unatarajiwa kuwa na faida pana kwa jamii nzima inayozunguka shule hizo . Lengo la mradi huu ni kufikia shule 1,000, ambapo zaidi ya wanafunzi 360,000 watafaidika. Lakini si kwa wale tu walioko shuleni, wazo ni kwamba itanufaisha pia jamii za shule, ikimaanisha watoto walioko nje ya shule na vijana katika jamii wanaweza kufaidika.