Dar es Salaam. Unaweza kusema dunia imejaa ubinafsi. Hii ni kutokana na tabia ya baadhi ya watu ya nipe ni kupe. 

Hili wala siyo geni hasa katika sekta ya burudani ambapo wasanii wa kike hukutana na rushwa ya ngono hasa wakati wanajitafuta.

Wapo wanaotoa kwa ajili ya kupata  msaada lakini wapo wachache wanaopinga kwa kuamini kipaji chao ni kikubwa kuliko wanachoombwa. Kilio hiki hakijaanza leo wala jana na siyo Tanzania tu tunaweza kusema ni ulimwenguni kote.

Akiwa ni binti mdogo anayepambania ndoto zake Zulfa Mohamed Ibrahim ‘Xouh’, ni kati ya wasanii wanaokumbana na changamoto hiyo. Akizungumza na Mwananchi msanii huyo anayetamba na ngoma ya ‘Nazidiwa’ amesema licha ya changamoto hizo hawezi kurudi nyuma.

“Changamoto kubwa ambayo inatukumba mabinti ni rushwa ya ngono. Lakini mimi najua nafasi yangu najua thamani yangu, hivyo hainibabaishi. Najua jinsi ya kuiepuka, changamoto nyingine wadada tumezoea kujiona hatuwezi. Upande wangu nimeshasema naweza kufanya vitu kwa weledi kama inavyotakiwa, wadada tusibweteke,”amesema.

Akizungumzia kilichojificha nyuma ya wimbo wake mpya ‘Nazidiwa’ amesema alipata idea baada ya kufika studio kurekodi wimbo mwingine.

“Nazidiwa nimeandika mwenyewe, idea ilikuja  baada ya prodyuza Trone kucheza ‘biti’. Kabla ya  hapo nilienda kurekodi wimbo tofauti ambao niliutengeneza nyumbani. 

“Baada ya kufika tukafanya wimbo ulionipeleka, huwa napenda kuchukua biti kwa ajili ya kwenda nayo nyumbani. Unajua wimbo ukiandikia nyumbani unakuwa tofauti na studio, kwa hiyo baada ya kumaliza kurekodi nikapata idea,”amesema.

Ameeleza baada ya kupewa biti mpya kwenda nayo nyumbani ndipo wazo la Nazidiwa likaja. Wimbo huo unaosifia mapenzi kupitia mwanamke anayeeleza kuzidiwa na mahaba anayopewa na mpenzi wake hadi sasa umetazamwa zaidi ya mara laki moja katika mtandao wa YouTube.

“Tunajua mapenzi ni mazuri ni matamu  lakini pia mimi naimba muziki wa mapenzi kwa ajili ya mashabiki zangu. Kuna komenti nimewahi kuona mtu anasema nikiachia wimbo hata kama akiwa amemchoka mwanaume wake mapenzi yanarudi upya. Kwa hiyo nazidi kukazia ili watu waendelee kudumisha upendo,”amesema Xouh.

Awali wengi walimfahamu Xouh kupitia wimbo wake ‘Huyu wa Sasa’ uliotoka miaka mitatu iliyopita. Hata hivyo anazungumzia utofauti alionao sasa  akilinganisha na alivyoanza muziki.

“Akili yangu imetanuka biashara ya muziki nimezidi kuielewa zaidi. Nilivyokuwa naanza kufanya muziki nilikuwa sijui chochote kuhusu muziki zaidi ya kuimba. Sikujua biashara yake inazunguka vipi.

“Lakini kwa sasa najua biashara hiyo kuna vitu vingi vimebadilika. Hata kwenye nyimbo zangu mavazi, ninavyowasilisha ujumbe na hata kwenye mazungumzo naongea kama msanii,”amesema na kuongezea.

“Wakati naaza nilikuwa na safari nyingi kwa sasa zimepungua sitoki bila sababu ya msingi.”

Akiwa na zaidi ya miaka minne kwenye muziki Xouh amesema kutokana na aliyopitia amejifunza kuwa muziki unahitaji uvumilivu.

“Funzo kubwa ni kuwa mvumilivu pia kutomwamini kila mtu. Watu wa muziki wana mbinu nyingi sana kwa hiyo ukimuamini kila mtu inakuja kukutesa. Wanakuja kwa njia nzuri wanasema watasaidia lakini hawatekelezi chochote mwisho mambo yanakuwa mengi. 

“Muziki pia unahitaji mtu anayejitambia, uwe unajua jinsi gani ya kuishi kwenye mazingira yako, ujue kujithamini na kuchagua watu wako wa kufanya kazi sio kila mtu. Unatakiwa kutumia akili kubwa sana ukilega watu wa muziki watakuendesha,”amesema Xouh.

Ishu ya lebo

Alipoanza muziki msanii huyu alikuwa akipata sapoti kutoka kwa marafiki zake na siyo kuwa na meneja wa uhakika, kwa sasa anasema ana meneja na team yenye nguvu.

“Meneja nilipata lakini pia nina team yangu ambayo ipo ‘strong’ vibaya mno. Inasimamia kazi zangu ziweze kwenda sawa katika mpangilio. Kwa yanayoendelea kwenye lebo nimeyasikia vizuri. Mimi kuingia kwenye lebo naweza ila tu ni makubaliano.

“Wakati vitu vinaendelea  nimejaribu kufuatilia ishu kubwa ni mikataba ambayo tunaenda kusaini. Kuna mahali unaweza usielewe alafu ukasaini kwahiyo baadaye mkataba unakuja kukufunga. Pia hiyo ni kutokana na changamoto  ya elimu ndio maana nimejikita kwenye kusoma kwa sasa,”amesema.

Msanii huyu kwa sasa amerudi shule  kwa ajili ya kusomea biashara ya muziki.

“Mwezi mtukufu ukiisha tunaanza kuachia ngoma. Ikitokea lebo nitasaini kwenye kujipanga hapo niko sawa kukabiliana na changamoto kwa sababu ndio zimetukuza.

“Muziki umenifanya niishi vizuri, mafanikio ni makubwa tofauti na maisha yangu ya awali. Muziki umefanya niishi maisha ambayo nilikuwa nayaota ni kitu ambacho nakiheshimu sana,” amesema Xouh.

Kwenye uigizaji yuko poa

Xouh ni kati ya waigizaji kwenye tamthilia ya Memkwa ya kwake Ndaro na Steve Mweusi. Amesema uigizaji ni kitu alichoanza kabla ya muziki.

“Nimeigiza Memkwa aliyenipa mchongo ni Steve mwenyewe, alinitafuta kitu ambacho hawakijui mashabiki wangu  mimi ni mwigizaji mzuri sana najua kuigiza, Najua kitu gani kinatakiwa kwenye kuigiza kwa hiyo haikuwa ngumu kwangu,” amesema Xouh.

Amemalizia kwa kuwaomba mashabiki zake waendelee kumsapoti kupitia majukwaa mbalimbali anayoweka kazi zake.
Kazi nyingine za Xouh ni Shemeji akiwa na Kontawa, Dua Yangu, Tena, Lalala, Mganga, Nipo Biza na nyinginezo.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *