
Dar es Salaam. Kama umetoboa shukuru sana Mungu. Kwa sababu kutoboa hakuna ‘fomula’, ‘staili’, mbinu wala ‘sistimu’. Tena Afrika hapa ndo wengi tunajikuta tuna hela au masikini. Lakini mekuaje? Wengi hatujui.
Ndo maana simulizi nyingi sana za waja kuna sehemu hurukwa. Atakuambia tu nilifanya kitu flan au biashara flan kwa mtaji huu. Hapo katikati anakuacha utoe tu macho, kisha anamalizia kusema, “pambana sana”.
Kuna wehu husema kujenga urafiki na kitanda ni kukaribisha umasikini. Lakini hasemi amka ukafanye nini, wanasema tu usilale sana. Huu ni udwanzi kama udwanzi mwingine. Kenge wa buluu, toeni michongo.
Yatazame makabila ambayo watu wake wengi wametoboa. Utaona wengi hushikama mikono na siyo mahubiri ya usilale ama pambana tu. Akitoka huyu, kesho hushikwa mkono yule na yule na mwisho wote wanakuwa watamu.
Ilikuwa kama utani hivi. Wakati huo Bongo Fleva inamilikiwa na watoto wa kihuni. Ilikuwa ngumu sana asiyechana kupokelewa na mashabiki kwa nguvu. Kina Dully walitoboa kwa kuvaa ujasiri na kuingia kwa miguu miwili
Wakaufanya muziki usiwe kwa masela tu kama Manduli Mobb. Watoto wazuri wa kike mitaani nao wakaanza kuelewa na wao kutemana na taarabu. Bongo Fleva ikakamata kutoka Ilala kwa Abdul Sykes hadi Kino kwa Masoud Kalama.
Vikajitokeza na kuzaliwa vipaji siku hadi siku. Mchanganyiko wa wagumu na wabana pua. Ni kama nyanya na kitunguu au yai na viazi vya Uyole milamani. Wahuni wa kitaa walibaki, wahuni wa kishua nao ‘wakajoini’.
Wenye akili wakaulainisha muziki na kuupeleka dunia ya dili zaidi. Daraja la uswazi na ushuani pia likavunjwa kama ukuta wa Berlin.
Maisha yakawa mepesi. Wenye ndoto za kijinga kuzamia Ulaya wakasitisha safari zao.
Mikoroshini Temeke wakaiteka Osterbay na Masaki. Wa kishua wakaanza shobo kwa masela kina Inspector. Taswira halisi ya mtoto wa kutoka uswazi, akawa juu kama mwezi. Kamata viumbe vya kishua kwa ‘lavu’ au saini kwa vitabu vyao.
Kutoka kuishangaa Coco Beach, hadi Coco kuwashangaa wao. Ni ngumu kuamini muziki ulianza na wa kishua Obei na Masaki. Wenye ‘aksesi’ ya kupata pini za majuu na kuielewa lugha ya ‘Joji Bushi’. Maana gemu tuliiga Marekani.
Ajabu wa kiswazi, ambao hata ngeli ilikuwa anasa. Wakawa bora kwenye biti za Mdachi Khalfan na Mchaga Kimario. Wakageuka lulu mitaani, na kugeuza muziki dili la vijana na kupunguza njaa kwa wazazi mitaani.
Bongo Fleva ya sasa ni kama vile inaukataa mtaa wake. Inakuja na kutoweka na kuacha utawala kwa singeli. Huu muziki uliokuzwa na wana wa uswazi tunautenganisha na mtaa. Hii ni ndoa na haivunjwi kizembe namna hii.
Mtaa uliamua madogo wabomoe mijengo ya ushuani na kujenga yao. Mtaa uliamua wabebe tuzo kwenye vibaraza vya mama zao Yemi Alade na Davido. Kila kitu ni mtaa uliozalishia, kuanzia swaga na wasanii wa leo na jana.
Kuivunja ndoa ya mtaa na sanaa. Ni kujipa utukufu wa umauti kwa kasi ama polepole. Kwani wasanii hadi hii leo wengi wao huzalishwa na mtaa. Asilimia 100 ya wasanii ni mbegu za uswazi ambao ndo mtaa wenyewe. Sasa tuulishe.
Nani wa kutudanganya kwamba ‘Ngosha The Don’ Fid Q ni Mbegu ya Capri Point? Hata Isamilo tu hafanani nayo. Vipi Joh Makini ana ‘testi’ na mitaa ya Njiro? Hata Sakina tu bado. Afande Sele wapi anafanana napo kati ya Forest na Mafiga?
Ndivyo ilivyo kwa FA na Muheza. Upanga haikumkuza alienda pale akiwa tayari kakomaa sana. Jide ni mbegu yenye makuzi yake kule Kiwalani na Yombo. Namanga sio makuzi yake ni eneo la ‘kumeki” michuzi. Uswazi ni wodi ya uzazi ya Bongo Fleva.
Ukiambiwa wasanii walio wengi wametokea uswahilini siyo Juma Nature na Inspekta pekee. Hata kizazi cha kina Mondi na Bilnass, Blue na Mbosso. Wote watoto wa uswazi ile kindakindaki, ila dunia inataka kuua asili yake kibwege.
Uswazi na Bongo Fleva ni ndoa, na uswahilini ndo mume, muziki ni mke. Tusikubali hii ndoa ifariki kijinga, kisa dunia inataka hivyo. Mtaa hautaki kulishwa ‘dei tu dei’ na wasanii. Bali mazao yalimwe, kupapaliwa na kuvunwa.
Mtaa unataka kujaza mbegu zaidi ushuani. Mbegu zitoke uswahilini zijae ushuani. Kama Bob Marley alilikimbia geto la King Stone na kuzamia Miami. Siyo ubaguzi, bali mbegu ilitoka ardhini ikachepua juu mwangani. Naeleweka?
Huu muziki lazima uwatoe geto wana. Kituristi, eksipensivu laifu, lavu iti oo livu iti, gademiti. Wana watoke magetoni na tunawajibu wa kuwatoa huko maana na sisi tulitolewa huko. Tusiwe wachoyo wa kunyanyua wengine.
Tusiwe kama wahubiri wale wa kulala sana unaita umasikini bila kutuambia tuamke kufanya nini? Sote zao la uswazi kwenye njaa na matatizo yote, tunawajibu wa kuwatoa wengine. Siyo kila mtu aimbe, hata mawazo na mbinu tuwape wainuke.
Msanii uliyetoka uswazi usijenge urafiki na viongozi kwa sababu ya familia na ndugu zako tu. Kuwa muwakilishi wa watu wa mtaa.
Hatuwezi kutoboa tusiposhikana. Hatuwezi kusonga tusipobebana. Tuwatoe wana magetoni kadiri tunavyoweza.
Ili msanii utambe muda mrefu, unahitaji watu wengi. Na ili watu wawepo kwa wingi, wanahitaji afya, elimu na miundombinu bora. Sasa ni wajibu wetu kushikana.
Msanii ukishapata jina na pesa usiusahau mtaa.
Usigawe pesa na mali, bali wewe wakilisha mtaa kila hatua zako. Watu wanataka sapoti siyo noti. Watu wanataka kusemewa siyo kumegewa. Ni wewe na mimi kuamka sasa. Tuutazame mtaa kwa jicho la wivu mkubwa huku tukiamini bila mtaa sisi siyo kitu kabisa.