Dar es Salaam. Ni wazi kuwa chapa (brand) ya Staa wa Bongofleva, Nandy (33), inazidi kupiga hatua katika kujiuza na kujitangaza kimataifa kwa lengo la kuvutia fursa mpya ikiwa ni miaka 10 tangu alipotoka rasmi kimuziki.
Nandy, mwanzilishi wa The African Princess Label, kwa sasa yupo katika Paris Fashion Week, moja wapo ya matukio makubwa zaidi ya mitindo duniani na yenye heshima kubwa kutokana na umahiri wa jukwaa hilo.
“Nina furaha kubwa kualikwa Paris Fashion Week huu mwezi huko Paris, kwa kweli ni hatua kubwa kwenye muziki wangu,” alieleza Nandy, mkali wa kibao cha No Stress (2025).
Paris Fashion Week ni tukio kubwa la kimataifa la maonyesho ya mitindo ya mavazi (fashion) linalofanyika kila mwaka katika jiji la Paris, Ufaransa, na limekuwepo tangu mwaka 1973.
Kwa miaka mingi, tukio hili limekuwa likikusanya wabunifu maarufu wa mitindo, wanamitindo, watu mashuhuri, wanahabari na wapenzi wa mitindo kutoka duniani kote.
Mitindo mipya ya mavazi, viatu na vifaa vya urembo huonyeshwa kwa mara ya kwanza na wabunifu wa mavazi ambao kwa kawaida huonyesha mitindo yote mipya (collections) kwenye maonesho ya jukwaani yanayoitwa runway shows.
Nandy anakuwa mwanamuziki wa pili kutokea Tanzania kualikwa katika Paris Fashion Week kwa miaka ya hivi karibuni baada ya Diamond Platnumz kuhudhuria mwaka 2024.
Akiwa huko, Nandy amesema mmoja wa wabunifu wakubwa wa mitindo kutoka Paris alimuomba amvishe mavazi kwa ajili ya maonyesho yake ya mitindo jukwaani (runway shows), kitu ambacho ameridhia.
Hatua hii kubwa inayoacha alama katika kazi yake, inamfanya Nandy kuendelea kujipambanua kama mwanamuziki wa kike Bongo mwenye nyota ya kung’aaa kimataifa kupitia kazi yake.
Nyota ya Nandy kimataifa ilianza kung’aa baada ya kushika nafasi ya pili katika shindano la kwanza la karaoke Afrika, Tecno Own The Stage, huku nafasi ya kwanza ikienda kwa Shapeera kutokea Nigeria.
Katika shindalo hilo ambalo fainali yake ilifanyika Nigeria mnamo Februari 2016, Nandy alizawadia kitita cha Dola15,000, wastani wa Sh37.4 milioni kwa sasa, pia alipewa nafasi ya kupata mafunzo chini ya lebo ya Chocolate City ambayo imewahi kufanya kazi na mastaa kama Ice Prince, Ckay n.k.
Baada ya hapo ndipo akatoka na wimbo wake, Nagusagusa (2016), na mwaka uliofuatia akachaguliwa kuwakilisha nchi katika mradi wa Coke Studio Africa 2017, ambako alifanya show ya kuvutia akishirikiana na mwimbaji kutokea Ethiopia, Betty G.
Tuzo yake ya kwanza kushinda katika muziki ni ya kimataifa, nayo ni All Africa Music Awards (AFRIMA), akishinda kama Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki katika hafla iliyofanyika Lagos, Nigeria mnamo Novemba 2017.
Ushindi huu ulikuja baada ya kuwabwaga Vanessa Mdee, Feza Kessy na Lady Jaydee, wote kutokea Tanzania, wengine ni Juliana Kanyomozi kutokea Uganda na Victoria Kimani kutokea Kenya.
Mnamo Agosti 2024, Nandy alipokea cheti kutoka kwa waandaji wa tuzo za Grammy, Recording Academy baada ya albamu ya Etana kutokea Jamaica, Pamoja (2021) kuchaguliwa kuwania tuzo hizo.
Albamu hiyo iliwania tuzo za 64 za Grammy 2022 katika kipengele cha Albamu Bora ya Reggae, huku Nandy akiwa ameshirikishwa katika wimbo unaokwenda kwa jina la ‘Melanin’ uliyopo katika albamu hiyo.
Hii ilikuwa ni hatua kubwa kwa Nandy kutokana na ukubwa wa tuzo za Grammy ambazo zilianza kutolewa Mei 4, 1959, wakati huo zikifahamika kama Gramophone Awards, huku lengo lake kuu likiwa ni kutambua mafanikio katika tasnia ya muziki.
Na albamu yake ya kwanza, The African Princess (2018) ilitoka chini ya Epic Records, rekodi lebo ya Marekani inayomilikiwa na Sony Music Entertainment (SME), na ilianzishwa mwaka 1953.
Baadhi ya wasanii waliochini ya Epic Records kwa sasa ni Travis Scott, Future, 21 Savage na Tyla, mshindi wa tuzo za Grammy kutokea Afrika Kusini.
Ni Nandy ambaye hadi sasa ameshirikiana na wasanii wa kimataifa kama Joeboy na Oxlade wa Nigeria, Willy Paul, Sauti Sol na Khaligraph Jones wa Kenya, pamoja na Koffi Olomide kutokea DR Congo ambaye walishirikiana katika wimbo, Leo Leo (2021).