DAR ES SALAAM : WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kufanya uwekezaji katika kituo cha kimataifa cha biashara (EACLC) iliyopo jijini Dar es Salaam ili kukuza uchumi wa nchi.
Akizungumza wakati wa futari iliyowahusisha viongozi wa dini na wananchi mbalimbali iliyoandaliwa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo Prof Kitila, amesema hadi sasa kituo kinaendelea vizuri na wafanyabiashara wengi wameshachukua nafasi na kimeshaanza kuchangamka.
“Nichukue nafasi hii kutoa wito wafanyabiashara wa kitanzania nafasi bado zipo wachukue maduka hapa pia natoa wito kwa Watanzania kutembelea eneo hili ambalo liko sehemu nzuri sana,”amesisitiza.
Amewashukuru viongozi wa dini wilayani humo kwa uamuzi wao wa kumuunga mkono hadharani katika chaguzi zilizopita.
Amesema msaada na mshikamano uliooneshwa na viongozi wa dini ulikuwa na mchango mkubwa katika ushindi wake, huku akiahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Katika hafla hiyo, Prof. Kitila alimtaja Mkurugenzi Mkuu wa EACLC, Catherine Wang, kuwa mshirika muhimu wa maendeleo na kuwahimiza wananchi kukisemea vizuri kituo hicho ili wanufaike na fursa za biashara zilizopo.

Wang amesema EACLC si mradi wa majengo pekee bali ni jukwaa la kitaalamu linalolenga kuimarisha uhusiano mwema kati ya kituo hicho na jamii inayokizunguka.
“Kwa pamoja tumekubaliana na kuthamini mchango wa kituo hiki ambacho kimeendelea kuwa nguzo muhimu kwa taifa, hususan kwa wananchi wa Ubungo na wilaya jirani zinazopata huduma zake. Kituo hiki kimekuwa sehemu salama na yenye utulivu kwa wafanyabiashara kufanya shughuli zao za kibiashara katika mazingira yenye amani.
“Tunaamini kuwa kwa kuendelea kushirikiana, kituo hiki kitaendelea kukua na kuwa mfano wa mafanikio katika sekta ya biashara. Ushirikiano kati ya viongozi, wafanyabiashara na jamii kwa ujumla utaendelea kuimarisha mshikamano na maendeleo ya eneo hili pamoja na taifa letu,” amesema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ubungo,Albert Msando amesema wataendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuhakikisha kila anayefika hapa anapata huduma na ushirikiano unaostahili.
Naye Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Maulid Salim Kidebe, alimshukuru Prof Kitila kwa kuandaa futari hiyo akisema mbunge huyo ana sifa ya kuwajali wananchi wake wakati wote na kwamba viongozi wa dini wataendelea kumuunga mkono hata katika siku zijazo.