
Dar es Salaam. Kama wewe ni mtaalamu katika sekta ya anga, hii ni fursa kwako baada ya Taasisi ya Uchunguzi wa Afya kwa Wataalamu hao, Aerospace Medical and Training Centre (AMTC), kutangaza huduma za uchunguzi wa afya bure kwa kundi hilo.
Huduma hiyo itaanza kutolewa Machi 31 kwa wataalamu hao, ikijumuisha uchunguzi wa shinikizo la damu, sukari kwenye damu, malaria, kiwango cha damu mwilini, uchunguzi wa tezi dume, saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya matiti.
Uchunguzi huo utafanyika katika Uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, na kuanzia Aprili Mosi hadi 2 huduma hiyo itatolewa katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 16, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa AMTC, Dk Nasra Nassor Omar, amesema wafanyakazi 500 watapatiwa huduma za afya.
“Wafanyakazi 200 watapatiwa huduma za afya katika Uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, na katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Terminal 1 na 2, wafanyakazi 300 watapatiwa huduma hizo. Uchunguzi tutakaoufanya utasaidia kubaini changamoto za kiafya mapema kwa wataalamu hao,” amesema.
Dk Nasra amesema lengo lao ni kuhakikisha kila mtaalamu wa sekta ya anga anakuwa na mafunzo sahihi ya afya ili kulinda usalama wa abiria na wafanyakazi wote wa sekta hiyo.
Amesema kwa kipindi cha miaka mitano AMTC imefanikiwa kutoa mafunzo kwa wataalamu wa sekta ya anga, wakiwemo marubani, wahudumu wa ndani ya ndege, wahandisi wa ndege na wafanyakazi wa viwanja vya ndege.
Akizungumzia upimaji wa afya wa wataalamu wa sekta ya anga,Mdau wa afya Magabilo Masambu amesema sekta ya anga ni mojawapo ya maeneo yenye uhitaji wa umakini mkubwa, utimamu wa mwili na afya ya akili.
“Marubani, wahudumu wa ndani ya ndege, wahandisi wa ndege na wafanyakazi wa viwanja vya ndege hufanya kazi katika mazingira yenye msongo wa mawazo, ratiba zisizo za kawaida na wakati mwingine uchovu wa muda mrefu.
“Hali hii inaweza kuongeza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu na kisukari,hivyo, uchunguzi wa mara kwa mara wa afya unaweza kusaidia kugundua matatizo mapema kabla hayajaleta madhara makubwa kwa mhusika na kwa usalama wa safari za anga”amesema.
Amesema vipimo wanavyofanyiwa wataalamu hao ni muhimu kwa afya ya jamii, akisisitiza magonjwa mengi kati ya hayo mara nyingi huibuka bila dalili za awali, hivyo uchunguzi wa mapema ni njia bora ya kinga na matibabu ya haraka.
Maadhimisho miaka mitano
Mbali na hayo, Dk Nasra amesema Aprili 4 mwaka huu watakuwa na maadhimisho ya miaka mitano tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, na katika hafla hiyo watazindua kitabu.
Kitabu hicho ni mwongozo wa vitendo kuhusu huduma ya kwanza katika sekta ya anga, na kimeandaliwa mahususi kwa ajili ya wahudumu wa ndege, wafanyakazi wa ardhini, wakufunzi wa masuala ya anga na wadau wa sekta hiyo.
“Pia tutazindua mfumo wa mafunzo na mitihani mtandaoni wa AMTC. Mfumo huu utatoa fursa kwa wataalamu wa sekta ya anga kupata mafunzo ya tiba ya anga, kufanya mitihani na kupata vyeti kupitia kompyuta bila hitaji la kusafiri,” amesema.