#HABARI: Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema Serikali iko tayari kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo maalum cha taarifa za maendeleo kitakachoanzishwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA-TAN) kwa ajili ya ukanda wa mikoa ya Kusini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa MISA Tanzania wakiwemo wahariri, waandishi wa habari na wadau wa habari kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, James amesema hatua hiyo inalenga kuboresha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wananchi na wadau wa maendeleo.

Amesema Serikali imepokea ombi hilo na kuiridhia MISA Tanzania huku akiitaka taasisi hiyo kuwasilisha maombi rasmi ili taratibu za kupatiwa eneo hilo ziweze kuanza mara moja.

Mapema, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, amesema kituo hicho kitakuwa jukwaa muhimu la kusambaza taarifa za maendeleo kwa wananchi, hususan wa ukanda wa Kusini.

Ametaja baadhi ya taarifa zitakazotolewa kuwa ni pamoja na bei za mazao, hali ya hewa, teknolojia za kilimo, masoko pamoja na masuala ya huduma za kijamii kama afya, elimu na mazingira akisema hatua hiyo itasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi ya kiuchumi na kijamii.

Soko amesema pamoja na mpango huo, MISA Tanzania inalenga kuhamasisha uandishi wa habari wenye mwelekeo wa suluhisho (solutions journalism) badala ya kuendelea kuangazia changamoto pekee.

“Uandishi wa habari siyo tu kuonesha matatizo, bali pia kuonesha suluhisho na fursa zilizopo katika jamii,” alisema Soko.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, amewataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kubadili mitazamo ya Watanzania, akisema changamoto kubwa siyo uhaba wa rasilimali bali ni uelewa mdogo wa namna ya kuzitumia.

Amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kusaidia kubadili fikra hasa kwa vijana ili waone wana uwezo wa kufanya mambo makubwa badala ya kusubiri wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Mkutano huo umeandaliwa na MISA Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, mfuko wa hifadhi za jamii NSSF, PPRA, na wadau wengine kwa lengo la kukuza ushirikiano baina ya vyombo vya habari na wadau wa maendeleo pamoja na kuimarisha uandishi wa ha

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *