Dar es Salaam. Ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China umeendelea kuimarika, huku nchi hizo mbili zikionekana kunufaika kupitia miamala ya kifedha iliyowezeshwa na Stanbic Bank Tanzania inayofikia zaidi ya Sh200 bilioni ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Hatua hiyo imeleta nafuu kwa wafanyabiashara wa Tanzania kwa kuwapa urahisi wa kufanya malipo, kuagiza bidhaa na kupanua masoko yao katika soko la China, ambalo ni miongoni mwa masoko makubwa duniani.
Kupitia mfumo huo, wafanyabiashara wameweza pia kuhimili changamoto za minyororo ya usambazaji wa bidhaa zilizojitokeza katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa upande wa China, ushirikiano huo umeongeza fursa za kuuza bidhaa zake katika soko la Tanzania na Afrika kwa ujumla, sambamba na kuchochea uwekezaji katika miradi ya kimkakati na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya pande hizo mbili.
Urahisishaji wa miamala hiyo umewezekana kupitia ushirikiano wa Stanbic na kampuni mama ya Standard Bank Group, uliowezesha kuanzishwa kwa dawati maalumu la biashara kati ya Afrika na China, likilenga kuwaunganisha wafanyabiashara na masoko kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mkuu wa Idara ya Biashara wa Stanbic, Fredrick Max, alisema hatua hiyo imeongeza ushindani wa wafanyabiashara wa ndani na kuwapa uwezo wa kushiriki kikamilifu katika biashara ya kimataifa.
Alisema kupitia programu ya Stanbic Biashara Incubator, zaidi ya wajasiriamali 2,000 wamewezeshwa kupata mikataba yenye thamani ya Sh32 bilioni, ikiwemo miradi mikubwa kama Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ambao umefungua fursa za masoko na ajira.
Mbali na sekta ya biashara, ushirikiano huo umechochea ukuaji wa sekta binafsi nchini, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira rafiki kupitia Tanzania Investment and Special Economic Zones Authority (TISEZA) ili kusaidia wazalishaji wa ndani kufikia viwango vya kimataifa.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Utafutaji wa Bidhaa na Mauzo ya Nje, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Kitila Mkumbo, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuimarisha uchumi kupitia sekta binafsi.
Mkuu wa Idara ya Biashara (BCB) Benki ya Stanbic Tanzania, Fredrick Max akipeana mkono na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo mara baada ya hotuba yake katika uzinduzi wa Kituo cha Utafutaji wa Bidhaa na Mauzo ya Nje ulioandaliwa na TISEZA.
Alisema Serikali inaendelea kusaidia biashara ndogo na za kati kuzalisha bidhaa zenye ubora kwa ajili ya soko la ndani na nje, huku akieleza matumaini kuwa programu hizo zitasaidia kukuza kizazi kipya cha wawekezaji, hasa vijana.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, asilimia 76 ya Watanzania wana umri wa chini ya miaka 35, hali inayosisitiza umuhimu wa uwekezaji katika kuwawezesha vijana kiuchumi.
Akizungumza awali, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri, alisema programu hizo zinalenga kukabiliana na changamoto za wajasiriamali ikiwemo ukosefu wa ujuzi, miundombinu duni na masoko ya uhakika.
Alisema katika mwaka wa fedha 2024/2025, TISEZA ilisajili miradi mipya 940 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 11, inayotarajiwa kuzalisha ajira 342,000.
“Tunalenga kuwapatia vijana ujuzi wa ujasiriamali na fursa ya kutumia miundombinu sahihi ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchakataji na uongezaji thamani wa mazao,” alisema.