
Ghana imesema mkutano kati ya Rais John Mahama na mwenzake wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, umeahirishwa, tangazo linalokuja wakati huu Pretoria ikishuhudia raia wake wakiwafukuza wageni nchini humo.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Accra na Pretoria zimekuwa katika sintofahamu ya kidiplomasia kufuatia mfululizo wa maandamano, ambayo mengine yalikuwa ya vurugu dhidi ya raia wageni nchini Afrika Kusini, Ghana ikihisi rais Ramaphosa ameshindwa kuwalinda raia wake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waziri wa mawasiliano wa Ghana, Felix Kwakye, mkutano huo uliopangwa kufanyika mwezi ujao, umeahirishwa, Accra ikisema inahofia ajenda za mkutano huo zitahitilafiwa na yanayoendelea Afrika Kusini.
Hata hivyo kumekuwa na mkanganyiko wa taarifa kutoka pande zote mbili, hasa kuhusu ajenda ya mkutano wa viongozi wa nchi hizo mbili, ambapo rais Ramaphosa alikuwa atembelee Ghana katika kile kinatajwa ni kujaribu kutuliza joto la mvutano baina ya nchi zao.
Raia wa Ghana walikuwa ni miongoni mwa mamia ya raia wengine toka mataifa ya Afrika waliolengwa katika mashambulio ya kibaguzi na wenyeji ambao kwa majuma kadhaa wamekuwa wakiandamana kushinikiza wageni kuondoka kwa kile wanadai wanachukua ajira zao.
Kufuatia maandamano hayo, uhusiano kati ya Afrika Kusini na mataifa mengi ya Afrika umetetereka, baadhi ya viongozi wakiona kuwa Pretoria inashindwa kuwalinda raia wao, licha ya kuwa baadhi wana vibali rasmi vya kuishi na kufanya kazi nchini humo.