Wakizungumza na George Musubao kutoka Radio washirika wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Maita ijulikanayo kama Radio canal Victoire du Peuple raia hao wmemwambia bila amani hakuna furaha
Furaha halisi ni amani
Benjamin Asimoni, mkazi wa Beni,jimboni Kivu Kaskazini ameeleza matumaini yake makubwa ya kuona amani ikirejea Congo
“Furaha duniani kama ina siku kuu ni vizuri sana. Lakini kwangu mimi kama mkazi wa Beni, kile ambacho kingelinipa furaha nikuona watu wanaokua chanzo cha vita wanakubali kuongea pamoja kutafuta kurejesha usalama, Ndio furaha yangu hiyo, amani irudi, vita iishe na watu waishi pamoja.”
Benjamin ameongeza kuwa kwa sasa furaha haipo kwa sababu ya changamoto za kila siku
“Furaha haipo kabisa. Nikicheka nikutafuta tulizo la moyo wangu. Kwa kucheka labda nikufanikisha moyo tu. Kwa ujumla furaha haipo.”
Diane Kasomo Marie Claire, mkazi wa Beni, jimboni Kivu Kaskazini.
Changamoto za wakimbizi zinapunguza furaha
Bibi Diane Kasomo Marie Claire, ni mkazi mwingine wa Beni, amesema Siku ya Furaha Duniani inapaswa kuwa wakati wa sherehe, lakini hali halisi Congo ni tofauti
“Kwa kawaida ni Siku ambayo inamaanisha furaha, lakini sio kama tunaishi katika furaha kwani tunapitia mambo mengi sana. Kwa sasa kuna wakimbizi wa ndani kutoka Goma na tunaishi nao nyumbani pasipo furaha.”
Diane ametoa wito kwa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kurejesha amani na usalama
“Naomba Serikali yetu itusaidie kurejesha amani. Wapambane sana ili usalama urudi katika nchi ya Congo, hasa Beni, Butembo na Goma.”
Maoni haya yanatoa taswira ya wazi ya jinsi migogoro na wakimbizi inavyopunguza furaha halisi ya raia.
Kwa wakazi wa Beni, furaha sio tu sherehe, bali ni amani, usalama, na uwezo wa watu kuishi kwa heshima, utu na uhuru.