Dar es Salaam. …Tatizo mi bado, nilipoteleza nikakosa sipajui… Mpaka akafunga virago, na akaamua kuondoka sitambui… Ubaya, kinachoniumiza, maneno neno manenoo… Mara kwa ndugu rafiki, kwanini anawapa misemo… Najaribu papasa, kuona hata macho yataona chochote… IIa ndo kutwa mikasa, na nazidi kuanguka, niokote…
Toka Kimbiji Kigambonino hadi Kintagiri Mwanza. Toka Nzovwe Mbeya hadi Sahare Tanga. Toka Kihesa Iringa hadi Micheweni Zanzibar. Au Mikindani Mtwara hadi Njiro Arusha. Awe msela au duu, muulize pini tano za Mondi.
Hawezi kuacha kutaja ‘songi’ la “Ukimuona”. Asipotaja basi ana ubwege na undezi ndezi wa ndani kwa ndani. Mtupe huko endelea na safari zako za ‘laifu’. Hili pini kwa akili na utashi wa kiutu utauhusudu tu.
Lakini msela mwenye makuzi ya Tandale. Ambaye leo hii ni mali ya dunia na ulimwengu. Hakututendea haki kwa kichupa dadeki zake. Aliliachia hili pini chukuchuku bila kuona fujo za Kimwana na wenzake kideoni.
Kwenye ‘praimu’ yake Simba alitutakasa na hilo dude. Na sisi tukalipokea na kuliweka moyoni na akilini. Mpaka leo shabiki wa kweli wa mapini ya mwana, lazima akusanue kuhusu ‘Ukimuona’. Noma na nusu babaake.
Unaweza kuwa umesizi kitaa, huna hili wala lile. Ghafla tu msela akapita na kindinga chake ndani linasikika goma la “Ukimuona”. Kuna namna kusizi kwako kutatoweka na kukupa ‘vaibu’ nyingine. Oya siyo poa hili dude.
Haina maajabu, lakini siku zote ndivyo ilivyo. Msanii yeyote lazima awe na pini ambayo wana wanaielewa kinyama mpaka mwenye pini anashangaa. Ndo Mondi na dude hili, hakuliwekea msuli kulitoa.
Pini lenyewe limeenda ‘vairo’ bila promo yoyote wala kideo mtandaoni. Tafuta pisi kitaa iulize kuhusu ‘Ukimuona’, ni lazima atakuchana. Kwamba analizimia kinoma noma, na hata msela atakujibu hivyo.
Haina kichupa. Kosa kubwa sana la Mondi. Ama Tiffah na kaka zake watalitendea haki mbeleni wakiwa wakubwa. Video ndiyo maktaba sahihi zaidi ya nyimbo kuliko ‘audio’ pekee. Na hili wasanii wetu wanapaswa kufahamu.
Bob Marley kilichosaidia pini zake ziishi muda mrefu ni zile ‘laivu shoo’ zake, zenye video. Ndo maana ngoma zake hata leo zinakimbiza. Kina Marijan, Mbaraka, Tx Moshi, walifanya kosa hili, hawana zile clip zao.
Mondi itakuwa vyema sana akifanya ‘laivu shoo’ ya pini la ‘Ukomuona’, kuchukua video yake. Kuacha kumbukumbu yenye kuishi, kuliko namna hii pini imekuwa kiyatima. Kivipi ‘I mis u’ ina video ‘Ukimuona’ inakosa?
Wimbo huu kurudiwa na kina Bella siyo kwa bahati mbaya. Wanaujua ukubwa wa ngoma hii. Kuacha iishi kinyonge hivi ni kuutendea dhambi muziki mzuri wa Mondi. Dhambi ya hapa duniani na ahera. Hapana!
Bongo Dar es Salaam
…Pitia pitia night kali mitaa ya Kinondoni… Kina dada poa nusu uchi fegi mdomoni… Na kama una gari watajazana madirishani wee… Mpaka ukose hewa wote wanataka hisani…
Kwenye madaladala kuibiwa ni kawaida… Vaa cheni shingoni, saa mkononi utoe faida… Wacha dirisha wazi kisha ukatize Manzese… ili uwape mateja mtaji waende chimbo wakatese… Rudi Mwananyamala oh! Mateja kibao… Katiza saa moja moja uone roba za mbao… Utaona kama mtoa roho yuko karibu yako… Ni kheri utoe chochote ili uokoe nafsi yako…
‘Lejendi’ Joseph Haule Prof. Jay ‘Wa Mitulinga’. Miaka 20 na zaidi iliyopita alitutendea kosa kama hili, huu wimbo ulihitaji video. Yeye anaweza kujitetea nyakati zile watu wa video wasingeutendea haki wimbo wake. ‘Kwalite’.
Lakini laiti kama ingefanyiwa video, angetuachia ‘memori’ nzuri sana Watanzania juu ya jiji lao hili. Mambo aliyoimba mengi yalikuwepo kwa sasa hayapo. Mateja Manzese au Mwananyamala hakuna tena kama zamani.
Daladala hazipo Manzese ni Mwendokasi. Na mateja wa Mwananyamala waliotukaba hawapo tena miaka ya sasa. Mji umechenji, hata mishe za kuuziana cheni za bandia leo zimetoweka kama kisonono.
Hizi mambo zingekaa katika mchupa flan hivi unyama. Na bahati mbaya siyo Jay pekee, wasanii wote wa zamani hili liliwashinda. Coz ‘audio’ zile zilikuwa bora kuliko video. Tulikuwa nyuma ya wakati kwenye video.
Tazama nyimbo zilizopigwa kideo kipindi kile. Nyimbo ni kali kuliko video, hii ilifanya wengi waachie ‘audio’ kuliko video. Jaribu kukumbuka pini za kitambo zisizo na video ‘Geto langu’ Ngwair, Barua ya Daz Nundaz.
Kamanda Daz Nundaz? “Jinsi Kijana” Sir Nature? “Mzee wa Busara” Wachuja Nafaka. Na ile “Mikasi” ya Ngwair, wewe ifanye kama mfano wa pini kali lenye video mbovu. Kwa hili tulichelewa na ‘kutukosti’.
Lakini “Ukimuona” ni kusudi la Mondi. Pini lilitoka nyakati njema za kampuni za video na ‘kamera mani’ wa maana kibao. Halafu msela mawe ya kufanya atakalo yapo tele. Tunahitaji ‘memori’ sahihi ya ‘Ukimuona’ katika video.