Moshi. Taasisi ya GGML Kili Trust kupitia programu ya GGML Kili Challenge, imeshiriki maonesho ya Kilimanjaro Marathon 2026 maarufu kama “Mbio za Watu”, yanayofanyika katika viwanja vya Ushirika, Moshi kuanzia Machi 20 hadi 22, kwa lengo la kuhamasisha mapambano dhidi ya UKIMWI.

Kupitia ushiriki huo, GGML Kili Challenge Against HIV/AIDS inaendelea kuhamasisha wadau mbalimbali kushiriki katika jitihada za kupambana na maambukizi ya VVU na UKIMWI nchini, huku rasilimali zinazokusanywa zikielekezwa kusaidia watu wanaoishi na VVU pamoja na taasisi zinazowahudumia.

Mwaka huu, mfuko huo umeongeza ushirikiano na asasi za kiraia kutoka maeneo mbalimbali nchini zinazotekeleza programu za kusaidia waathirika wa VVU na UKIMWI, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kufikia watu wengi zaidi.

Katika banda la GGML Kili Challenge, washiriki wa mbio na wageni wa maonesho wanapata fursa ya kujifunza kuhusu shughuli za mfuko huo, namna ya kushiriki pamoja na miradi inayotekelezwa, huku huduma za upimaji wa VVU zikitolewa kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).

Aidha, wageni wanapata nafasi ya kutoa ahadi ya kuchangia, kujisajili kushiriki GGML Kili Challenge inayotarajiwa kufanyika Julai 2026, pamoja na kupata maelezo kuhusu njia mbalimbali za kushiriki katika mapambano dhidi ya UKIMWI.

Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa GGML Kili Trust, Stephen Mhando amesema mpango huo unaunga mkono mikakati ya taifa ya kupambana na UKIMWI kupitia uhamasishaji wa jamii na ushirikiano wa wadau mbalimbali.

“Tunawaalika washiriki wote wa marathon na wageni wa maonesho kutembelea banda letu ili kujifunza zaidi na kuona namna wanavyoweza kushiriki katika kuunga mkono jitihada hizi,” amesema Mhando.

Tangu kuanzishwa mwaka 2002, mpango huo umekuwa ukiwakutanisha watu binafsi, taasisi na wadau mbalimbali kuchangia juhudi za kinga, tiba, matunzo na msaada kwa jamii.

Kupitia ushiriki huo, GGML Kili Trust imeendelea kusisitiza umuhimu wa kufikia malengo ya sifuri tatu; maambukizi mapya sifuri, unyanyapaa sifuri na vifo vitokanavyo na UKIMWI sifuri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *