
Jeshi la Iran limetangaza kuwa limetungua ndege ya kivita aina ya F15 ya maadui wavamizi, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, kusini mwa nchi.
Ripoti iliyotolewa na Jeshi la Iran imesema, ndege ya kivita aina ya F15 ya adui imepigwa kwa kombora la jeshi mapema leo katika anga ya maeneo ya pwani kusini mwa Iran, karibu na kisiwa cha Hormuz.
Taarifa ya Idara ya Uhusiano wa Umma ya Jeshi la Iran imesema uchunguzi wa kubaini taarifa zaidi kuhusu hatima ya ndege hiyo ya kivita bado unaendelea.
Hii ni ndege ya saba ya kivita ya muungano wa Marekani na Israel kutunguliwa na majeshi ya Iran katika vita vya sasa vya madola hayo mawili vamizi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Siku chache zilizopita, ndege ya kivita ya kimkakati aina ya F‑35 ya Jeshi la Marekani ilipigwa kwa kombora na kuharibiwa vibaya ikiwa katika anga ya kati mwa Iran kwa lengo la kutekeleza mashambulizi.
Ndege hiyo ya kisasa ilipigwa kwa mfumo mpya wa kisasa wa ulinzi wa anga wa Kikosi cha Anga cha IRGC katika anga ya Iran ya kati, na kuharibiwa vibaya.
Msemaji wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) Kapteni Tim Hawkins amesema kuwa ndege hiyo ya kivita ya kizazi cha tano yenye uwezo wa kujificha kwenye rada ilikuwa ikitekeleza kile kilichoelezwa kuwa “operesheni ya kivita juu ya anga ya Iran”.