Dar es Salaam. Mjadala mkali umeendelea kushika kasi kufuatia sintofahamu inayoizunguka michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), huku wadau wa soka barani Afrika na duniani wakionyesha wasiwasi kuhusu uhalali wa maamuzi yaliyofikiwa katika hatua za mwisho za mashindano hayo.

Jumanne iliyopita Kamati ya Rufaa ya CAF iliamua kwamba kwa mujibu wa Kifungu cha 84 cha Kanuni za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), Timu ya Taifa ya Senegal imepoteza mechi ya fainali ya fainali hizo iliyochezwa Januari 18, 2026 na matokeo ya mechi hiyo  kuwa ushindi wa mabao 3–0 kwa Morocco.

Kanuni ya 82 inafafanua hivi, “Timu itakayoondoka uwanjani kabla ya mchezo kumalizika bila ruhusa ya mwamuzi itapoteza mchezo husika na kuondoshwa kwenye mashindano.”

Kanuni ya 84 inafafanua kwamba timu itakayokiuka kifungu cha 82 itapoteza mchezo husika kwa mabao 3:0 ikiwa ni pamoja na kuondoshwa jumla kwenye shindano husika.

Uamuzi huo unafuatia rufaa iliyowasilishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Morocco (FRMF) kuhusu utekelezaji wa vifungu vya 82 na 84 vya Kanuni za AFCON.

Senegal, ambayo awali ilionekana kunufaika na matokeo ya uwanjani, imeibuka kuwa mstari wa mbele kupinga kile kinachodaiwa kuwa ni ukiukwaji wa haki na taratibu za mashindano.

Katika hali iliyoongeza uzito wa mjadala huo, taarifa zinazosambaa mitandaoni zinadai kuwa nyota wa kimataifa, Lionel Messi, alimtumia ujumbe wa kumtia moyo mshambuliaji wa Senegal, Sadio Mané.

Ujumbe huo, ambao haujathibitishwa rasmi, unamnukuu Messi akimtaja Mané kama “shujaa wa Afrika” na kusisitiza kuwa haki ya Senegal haiwezi kuporwa kirahisi.

Licha ya kutokuwa na uthibitisho wa moja kwa moja, kauli hiyo imepokelewa kwa hisia kali, hasa barani Afrika, ambapo mashabiki wengi wameitafsiri kama ishara ya mshikamano wa kimataifa kwa soka la Afrika na wachezaji wake.

Shinikizo zaidi limeongezeka baada ya nguli wa soka kutoka Ivory Coast, Didier Drogba, kuikosoa wazi CAF. Drogba alieleza kushangazwa na mwenendo mzima wa maamuzi hayo, akisisitiza kuwa matukio ya aina hiyo ni nadra kushuhudiwa katika mabara mengine yenye mifumo thabiti ya uendeshaji wa soka.

Kauli hiyo imeongeza uzito wa hoja za wanaodai kuwepo kwa mapungufu katika usimamizi wa mashindano hayo, huku wengine wakitaka uwajibikaji na uwazi zaidi kutoka kwa mamlaka husika.

Kwa upande wa Senegal, msimamo umeendelea kuwa mkali.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo, Abdoulaye Sow, amesisitiza kuwa taifa hilo haliko tayari kukubali kupokonywa kile wanachoamini ni haki yao ya msingi.

Amesema mjadala huo hauishii ndani ya mipaka ya Senegal pekee, bali umevuka hadi katika jukwaa la kimataifa.

“Tunachokitetea ni haki na uhalali wa matokeo ya uwanjani. Hili si suala la Senegal pekee, bali ni la heshima ya soka kwa ujumla,” alisisitiza.

Wakati huo huo, sintofahamu imeongezeka kufuatia taarifa kuwa Sadio Mané huenda akalazimika kurejesha tuzo ya mchezaji bora wa mashindano (MVP), huku kiungo wa Morocco, Brahim Díaz, akitajwa kupewa tuzo hiyo.

 Hatua hiyo imezua mjadala mpya kuhusu vigezo vinavyotumika kutoa tuzo hizo na iwapo vilizingatia misingi ya haki na ushindani wa kweli.

Kwa wachambuzi wa soka, tukio hili linaibua maswali mapana zaidi kuhusu uongozi na mifumo ya maamuzi ndani ya soka la Afrika. Wanaonya kuwa iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa kwa haraka, hali hiyo inaweza kuathiri taswira ya mashindano ya AFCON pamoja na imani ya wadau wake kimataifa.

Kadri mvutano unavyoendelea, macho ya dunia yanaendelea kuelekezwa barani Afrika, yakisubiri kuona kama mamlaka za soka zitaweza kurejesha imani, uwazi na uadilifu katika moja ya mashindano makubwa zaidi ya soka duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *