Na Asha Msoka na Bruno Richard
Wakati mwanga mwanana wa asubuhi ukiangaza kando ya Mto Katuma ulioko magharibi mwa Tanzania, Nasra Nassoro anaonekana amesimama ndani ya maji yanayotiririka yaliyofikia usawa wa magoti yake, akiongoza timu yake kwa utulivu huku wakishusha kifaa cha kupima mwendo wa maji ndani ya mto huo.
Kifaa hicho cha kisasa kinatoa sauti ya chini, kikirekodi kasi ya mto, kina, na kiasi cha maji kinachopita. Kwa Nasra, ambaye ni Meneja wa Rasilimali za Maji katika Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Rukwa (LRBWB), hatua hii ni zaidi ya kazi zake za kawaida za kila siku. Ni mafanikio ya taratibu.
“Nimefanya kazi hapa kama mtaalamu wa haidrolojia kwa miaka 15,” Nasra anatafakari. “Eneo hili lina uwezo wa kipekee wa utajiri wa bioanuwai, lakini tulihangaika kudhibiti rasilimali zetu za maji katika vyanzo vya Katuma na kuongeza faida zake. Mradi wa IKI Katuma umebadilisha kabisa uwezo wetu wa kuelewa na kufanya maamuzi bora.”
Mto Katuma ni moyo wa ikolojia na uchumi
Mto Katuma ni mapigo ya moyo wa moja ya kanda zenye utofauti mkubwa wa ikolojia na umuhimu wa kiuchumi nchini.
Ukianzia katika milima ya Mwese na Mpanda kwenye Nyanda za Juu za Ufipa, mto huu unakatisha kwenye Hifadhi ya Taifa ya Katavi, moja ya maeneo yanayohifadhiwa zaidi na yenye utajiri wa wanyamapori nchini, kabla ya kuingia katika Ziwa Rukwa.
Kifaa cha RS5 Acoustic Doppler Current Profiler kikiwa kimewekwa kwenye Mto Katuma ili kukusanya vipimo vya kina vya mtiririko wa maji kwa ajili ya tathmini ya rasilimali za maji.
Mafuriko ya msimu yanaupa uhai mfumo wa ikolojia na kuimarisha makazi ya viumbe yanayoibeba sekta ya utalii inayokua nchini.
Nje ya hifadhi, Mto Katuma unahudumia zaidi ya watu milioni moja wanaoutegemea kwa maji safi ya kunywa, umwagiliaji mdogo, kunywesha mifugo, uvuvi, na biashara za kila siku.
Katika miaka ya hivi karibuni, bonde hili pia limekuwa eneo la kimkakati la akiba ya chakula cha Taifa, likilinda usalama wa chakula na kuongeza mapato kupitia mauzo ya nje.
Mashinikizo yanayoongezeka na changamoto za upatikanaji wa takwimu
Hata hivyo, uwepo wa mto huu pia umekaribisha mashinikizo makubwa yanayotokana na kupanuka kwa haraka kwa shughuli za kilimo, uvunaji wa maji kinyume cha sheria, ukataji miti uliokithiri, mabwawa ya uvuvi yasiyo rasmi, na uchimbaji wa madini ya dhahabu wa kienyeji.
Shuguli hizi zote zimevuruga mtiririko wa asili wa maji, zikiongeza mchanga na kuharibu ubora na wingi wa maji. Mashinikizo haya yameongeza ushindani kati ya watumiaji wa maji na kuhatarisha maisha ya wanyamapori wa hifadhini.
Kwa miaka mingi, Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Rukwa ilikabiliwa na changamoto zinazotokana na upatikanaji mdogo wa takwimu za kuaminika, hali iliyokwamisha usimamizi mzuri wa mto. Vituo vya ufuatiliaji vilikuwa vichache, na sehemu nyingine za mto zilikosa vipimo kabisa.
Ziara za mtoni hapo mara nyingi zilikuwa zikichukua muda mrefu na wakati mwingine zilikuwa hatarishi. Kwa sababu hiyo, maamuzi kuhusu vibali vya maji, ugawaji, na utekelezaji wa sheria mara nyingi yalikuwa ya kukurupuka na kutegemea habari zisizo za uhakika.
“Bila takwimu sahihi, makadirio ya maji yaliyopo au viwango salama vya ugawaji maji, lilionekana kuwa jambo la kubahatisha,” Nasra anaelezea.
Kutumia takwimu kama fursa ya usimamizi bora wa rasilimali maji
Mageuzi yalikuja mwaka 2024 ambapo ulizinduliwa Mradi wa Bonde la Mto Katuma unaofadhiliwa na Mpango wa Kimataifa wa Hali ya Hewa (IKI), ukitekelezwa na Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Rukwa, na wadau wa ndani.
Msaidizi wa usomaji vipimo katika Mto Katuma akipiga makasia kwenye mtumbwi huku akikokota kifaa cha haidrolojia cha RS5 ADCP mtoni ili kupima kina na kiasi cha maji
Kutokana na mijadala iliyokuwepo hapo awali, Nasra na wenzake walisaidia kutekelezwa kwa mradi, wakihakikisha unashughulikia mahitaji halisi yaliyopo kwa wakazi wanaoishi kuzunguka mto huo.
Baada ya kufanya utafiti wa teknolojia zinazofaa kwa hali ya bonde hilo, SNV ilichagua kifaa cha Acoustic Doppler Current Profiler (ADCP), kifaa kinachoweza kubebeka ambacho hutoa takwimu sahihi za mtiririko wa maji. Muhimu zaidi, mradi ulilenga kujenga ujuzi, kujiamini, na uhuru wa watumiaji.
Nasra na timu yake ya wataalamu wa haidrolojia zaidi ya 10 walipokea mafunzo ya kina ya vitendo na ushauri wa kudumu, wakijifunza mzunguko mzima wa takwimu ikiwamo itifaki za mto, ukusanyaji, uhifadhi, uchambuzi, kutafsiri taarifa, uandaaji wa ripoti, na utoaji wa matokeo ya tafiti.
Kwa mara ya kwanza, Bodi ilipata taarifa za kuaminika na za wakati halisi za haidrolojia ya mto huo.
Wataalamu mbalimbali hivi sasa wanaweza kuhuisha taarifa za mienendo ya maji, kufuatilia mifumo ya mtiririko wa maji wa msimu mzima, na kuwa na ushahidi wa kutosha wa kusimamia vibali vya uvunaji maji na uwekezaji wa miundombinu.
Takwimu zilizoboreshwa pia zinawaruhusu kutabiri uhaba wa maji katika msimu wa kiangazi, kupunguza migogoro kati ya wakulima wa umwagiliaji kwenye miinuko na mahitaji yale wanaofanya shughuli zao maeneo ya tambarare (chini), na kulinda mtiririko wa mazingira muhimu kwa mfumo wa ikolojia wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi.
Jamii kama walinzi wa awali wa Mto Katuma
Nasra alisimama kama msimamizi wa mchakato huo mzima. Aliratibu ratiba za ufuatiliaji katika bonde hilo, akaandaa timu za kutembelea mto, na kuhakikisha wenzake wamepatiwa elimu ya kutosha katika kutumia taarifa za kitakwimu na mawasiliano.
Baada ya muda, Nasra alijikuta akipata ujuzi na uzoefu wa kutosha wa kiufundi, hali iliyosababisha kupandishwa kwake cheo kuwa Meneja wa Rasilimali za Maji.
Matunda ya mchakato huu yalifurahiwa hadi na wanajamii wengine kama vile wasomaji wa vipimo waliopata mafunzo kama Hilary Daudi Kapenegele, mwanachama wa Chama cha Watumiaji Maji ya Bonde le Mto Katuma.
“Sikuwahi kutambua kikamilifu jinsi takwimu hizi zingetunufaisha moja kwa moja, katika ngazi ya jamii na mtu mmoja mmoja, kama wakulima na wafugaji,” Hilary anashiriki.
“Sasa tunaelewa thamani yake, na tunajadili matokeo katika mikutano ya kijiji ili kuamua hatua muhimu.”
Mradi pia unatengeneza zana rahisi za kutazamia taarifa kama vile chati, dashibodi, na michoro rahisi inayofanya habari ngumu za haidrolojia kueleweka kwa kila mtu, wakiwemo watoto wa shule.
Hilary anabainisha: “Tunasikia mradi utatengeneza picha/video zinazovutia kiasi kwamba hata mtoto wa darasa la pili anaweza kuelewa hali ya maji katika Mto Katuma. Najisikia fahari kuwa msoma vipimo wa kijiji chetu.”
Juhudi hizi zinajenga utamaduni wa usimamizi wa pamoja. Jamii zinakuwa washirika wenye habari katika kusimamia bonde badala ya kuwa wapokeaji tu wa kanuni.
Mfano wa kuigwa kwa mabonde mengine
Uzoefu wa Mto Katuma ulibuniwa mahsusi kuja kuwa mfano utakaoigwa na jamii nyingine. Kwa kuwekeza kwenye taasisi za kizawa na wataalamu kama Nasra, mradi unakuja na mbinu inayoweza kutumiwa kwa mabonde mengine tisa ya maji nchini.
Takwimu za kuaminika, timu zenye ujuzi, na jamii zinazoshiriki hutoa msingi imara wa usimamizi endelevu wa rasilimali za nchi mahali popote pale.
Changamoto bado zipo. Mabadiliko ya hali ya hewa, ongezeko la idadi ya watu, na mahitaji yanayoongezeka kila siku yanaendelea kuleta shinikizo kwenye mto huo. Nasra anaendelea:
“Katuma imeimarika kwa kiasi kikubwa. Hatupo pale tulipokuwa zamani, lakini bado hatujafika pale tunapolenga kuwa. Uwekezaji zaidi unahitajika, lakini sasa tuna ushahidi na ujasiri wa kutetea hilo.”
Mradi wa IKI Katuma unaonyesha nguvu ya msaada unaolenga ustawi wa watu. Wakati Tanzania ikikabiliwa na changamoto zinazoongezeka za maji, hadithi ya Nasra inatoa msukumo na njia ya wazi kuelekea usimamizi jumuishi wa maji unaozingatia ushahidi, ugawaji wa haki, ustahimilivu wa mafuriko na ukame, na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa muda mrefu.
Mradi huu uko chini ya ufadhili wa Mpango wa Kimataifa wa Hali ya Hewa (IKI) wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani