Shirika hilo limetoa wito wa msaada wa haraka wa kimataifa ili kuhakikisha kuwa kurejea huko kwa wakimbizi kunafanyika kwa usalama, heshima na uendelevu.

Limesema wengi wa wanaorejea wanavuka kupitia mpaka wa Kavimvira karibu na Uvira katika jimbo la Kivu kusini, baada ya kukimbilia Burundi mwezi Desemba 2025 kufuatia mapigano kati ya jeshi la serikali ya DRC (FARDC) na kundi la waasi la M23. 

Hali ya utulivu iliyoanza kurejea Uvira pamoja na kufunguliwa kwa mpaka UNHCR imesema imechochea baadhi ya wakimbizi kurejea nyumbani, huku uhaba mkubwa wa ufadhili nchini Burundi ukichangia kupungua kwa misaada na kuwafanya wengi kurejea licha ya hali ya kutokuwa na uhakika.

Changamoto kambini na maeneo ya kurejea

UNHCR inasema takribani asilimia 30 ya waliorejea walikuwa wanaishi katika kambi ya wakimbizi ya Busuma nchini Burundi, ambako msongamano mkubwa na uhaba wa maji, huduma za afya, usafi wa mazingira na makazi vimeripotiwa kutokana na upungufu wa rasilimali, licha ya juhudi za UNHCR na washirika wake. 

Watu wapatao 4,500 bado wako katika vituo vya mpito wakisubiri kuhamishiwa Busuma, huku Burundi ikiendelea kuhifadhi zaidi ya wakimbizi 109,000 wa Congo kufikia tarehe 23 Machi 2026.

Hata hivyo, hali katika maeneo wanakorejea nchini DRC bado ni tete, huku mahitaji ya kibinadamu yakiwa makubwa. Tathmini za awali za UNHCR katika maeneo ya Uvira na Fizi zinaonesha familia nyingi zinawasili bila chochote, zikihitaji kwa dharura makazi, vifaa vya nyumbani, huduma za afya pamoja na maji na usafi wa mazingira

Wengi wanakuta nyumba zao zimeharibiwa au kuporwa, hali inayowaweka katika mazingira magumu na kuwazuia kurejea katika maisha ya kawaida bila msaada wa haraka.

Familia moja na watoto wanapokea huduma ya matibabu katika kituo cha UNHCR huko Uvira, DR Congo. Mfanyikazi wa UNHCR akiwa amevaa koti ya beji anasimama nyuma ya kikundi hicho, wakati wafanyakazi wawili wa afya wa kike wakiwa wamevaa nguo za kijani wakiwahudumia wagonjwa mezani.

© UNHCR/Fabrice Mbonankira

Familia za wakimbizi wa Congo zinarudi nyumbani kwao Uvira katika jimbo la Kivu Kusini DRC kupitia bandari ya Kavimvira baada ya miezi kadhaa katika kambi ya wakimbizi nchini Burundi.

Msaada wa dharura na ulinzi wa wakimbizi

Kwa sasa, shirika la UNHCR kwa kushirikiana na mamlaka za kitaifa na za majimbo inaongeza juhudi za ufuatiliaji wa ulinzi na utoaji wa msaada wa kibinadamu. Timu zimepelekwa katika maeneo ya mipakani na sehemu za kurejea ili kufuatilia hatari na kubaini watu walio katika mazingira hatarishi. 

Katika maeneo ya Uvira na Fizi, msaada unaotolewa unajumuisha maturubai, mablanketi, sabuni, huduma za ulinzi pamoja na chakula cha moto, usajili na uchunguzi kwa wanaorejea.

shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), imesisitiza kuwa maamuzi ya wakimbizi kurejea nyumbani yanapaswa kuheshimiwa, na kurejea huko lazima kuwe kwa hiari, usalama na heshima. 

Shirika hilo limesisitiza kuwa ingawa kurejea kwa sasa kunaashiria matumaini ya utulivu, pia kunaathiriwa na upungufu wa ufadhili, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha usalama, huduma za msingi na msaada kwa jamii zinazowapokea wanaorejea.

Ufadhili bado hautoshi

Kwa sasa, hatua za UNHCR, kwa wakimbizi, wanaorejea na wakimbizi wa ndani nchini DRCzimefadhiliwa kwa asilimia 34 tu ya mahitaji ya dola milioni 145 za Marekani zinazohitajika , huku msaada kwa wakimbizi wa Congo walioko Burundi ukiwa umefadhiliwa kwa asilimia 20 pekee. 

Hivyo shirika hilo limesisitiza, kuna haja ya haraka ya kuongeza ufadhili ili kuokoa maisha na kusaidia familia hizi, iwe ni wale waliorejea au wale wanaoendelea kuwa wakimbizi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *