MSIMU huu wa Ligi Kuu Bara 2025-2026, umekuwa na changamoto nyingi za nidhamu, huku Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kupitia kamati yake ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ikichukua hatua za kufungia na kutoza faini wachezaji 14 hadi sasa.

Katika orodha hiyo, wachezaji saba wamekumbana na rungu la kufungiwa mechi tano kila mmoja ambao ni Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wa Yanga, aliyeadhibiwa kufuatia kumkanyaga kwa makusudi mchezaji wa Mbeya City, Ibrahim Ame.

Mohamed Bakari wa JKT Tanzania alifungiwa kwa kosa la kumkanyaga beki wa Azam, Lusajo Mwaikenda huku Gabriel Mwaipola wa Mbeya City akipata adhabu sawa na wenzake kufuatia kumpiga kiwiko Abdallah Mfuko wa Namungo pamoja na faini ya Sh5 milioni.

Vitalis Mayanga wa Mbeya City, alikumbana na adhabu ya kukosa mechi tano kwa kosa la kumpiga kiwiko beki wa Simba, Anthony Mligo, adhabu iliyoambatana na faini ya Sh1 milioni.

Nahodha wa Singida Black Stars, Khalid Aucho, alifungiwa michezo mitano na kutozwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kumpiga na kumsukuma Adam Adam wa TRA United.

Wachezaji wengine waliokabiliwa na adhabu ya mechi tano ni Jonathan Sowah wa Simba, aliyeadhibiwa kwa kumpiga kiwiko Himid Mao wa Azam na Allasane Kante wa Simba, aliyeadhibiwa kwa kumpiga teke Feisal Salum wa Azam, ambapo kila mmoja alitozwa faini ya Sh1 milioni.

Kwa upande mwingine, wachezaji waliokumbana na adhabu ya kufungiwa mechi tatu ni Seleman Mwalimu wa Simba na Abdi Banda wa Dodoma Jiji, kila mmoja akiwa na faini ya Sh1 milioni. Mwalimu aliadhibiwa kwa kosa la kumpiga kiwiko Andy Bikoko wa Dodoma Jiji, huku Banda akijirusha kutoka kwenye machela, hali iliyotafsiriwa ni kupoteza muda. Matukio yote hayo yalijiri wakati Dodoma Jiji na Simba zikitoka 0-0.

David Kameta ‘Duchu’ wa Simba, alikumbana na adhabu ya faini ya Sh1 milioni kufuatia kitendo cha kuonyesha tabia zisizokubalika uwanjani, kinachotafsiriwa kama ishara za imani za kishirikina katika mechi dhidi ya Yanga.

Wachezaji wengine waliolimwa faini kwa makosa ya kutosalimia wenzao kabla ya mechi kuanza ni Andy Lobuka Bikoko (Dodoma Jiji), Muhsini Malima (TRA United) na Mzamiru Yassin (TRA United).

Mchezaji ambaye amekumbana na adhabu ya kufungiwa mechi moja pekee kutoka katika kamati hiyo ni Lamela Maneno wa Fountain Gate.

Nyota huyo katika mechi kati ya Fountain Gate dhidi ya Dodoma Jiji, mwamuzi Shomari Lawi kutoka Kigoma, dakika ya 48 alimwonyesha kadi ya njano, kabla ya kumwonyesha kadi nyingine ya njano dakika ya 89 bila kutoa ishara ya kumtoa kwa kadi nyekundu, jambo lililotafsiriwa kuwa ni makosa ya kiufundi.

Kosa hilo lilifanya mwamuzi Lawi kuondolewa kwenye ratiba ya uchezeshaji wa michezo ya Ligi kwa mizunguko mitano, baada ya kubainika kuwa alishindwa kutafsiri ipasavyo sheria za mpira wa miguu, huku Maneno akifungiwa mchezo mmoja.

Hata hivyo, asilimia kubwa ya wachezaji waliokumbana na adhabu hizo wamemaliza na wamerejea katika majukumu yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *