
Kwa muda mrefu sasa, baadhi ya wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakilalamikia vitendo vya askari wa vikosi vya ulinzi vya Zanzibar na vya Muungano kuwapiga watu mijeledi kana kwamba miili yao ni vyombo vya adhabu visivyo na mipaka ya kisheria.
Malalamiko haya yamekuwa yakijirudia mara kwa mara bila kuonekana hatua madhubuti zikichukuliwa dhidi ya wahusika jambo linaloibua maswali kuhusu uwajibikaji na ulinzi wa haki za raia.
Katika matukio kadhaa, askari hao hudaiwa kushirikiana na makundi yanayojulikana kama valantia (mgambo) pamoja na vijana wanaofunika nyuso zao maarufu kama ninja. Ushirikiano huo umeendelea kuzua hofu miongoni mwa wananchi, hasa pale nguvu inapotekelezwa bila kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Wengi hujikuta wakikumbwa na adhabu ya papo kwa papo bila kusikilizwa au kupewa haki ya kujitetea.
Hali imefikia hatua ambayo hata baadhi ya askari wa manispaa, Mji Mkongwe na halmashauri za miji wameanza kujipa mamlaka yasiyo yao kisheria.
Kwa kisingizio cha utekelezaji wa majukumu yao, wapo wanaowanyang’anya wananchi leseni au funguo za vyombo vya moto na pale mtu anapopinga, hukumbana na kipigo kisicho na maelezo. Matendo haya yanaashiria kupanuka kwa matumizi mabaya ya madaraka, jambo linalodhoofisha misingi ya utawala wa sheria.
Licha ya matukio haya kuripotiwa mara kwa mara, bado haijawa wazi ni watu wangapi waliowahi kuwajibishwa kisheria kutokana na vitendo hivyo. Badala yake, wakati mwingine baadhi ya viongozi huonekana kuyatetea au kuyapuuza, hali inayotafsiriwa kama kuhalalisha udhalilishaji wa wananchi. Kukosekana kwa uwazi na hatua stahiki kunazidi kuongeza hofu na kukatisha tamaa kwa waathirika.
Katika ushuhuda wa moja kwa moja, tukio la vijana kupigwa katika eneo la Darajani na watu waliovaa mavazi ya kuficha sura zao lilionesha wazi namna mamlaka zinavyoweza kupuuzwa hadharani bila hofu.
Jaribio la kuhoji uhalali wa kitendo hicho kwa kiongozi aliyekuwepo halikuzingatiwa, badala yake alisisitiza kipigo kiendelee. Hii inaonyesha kiwango cha changamoto iliyopo katika kusimamia sheria.
Matukio ya aina hii yanarejesha kumbukumbu za nyakati ambazo watu walipigwa ovyo mitaani na hata majumbani, hali iliyosababisha hofu kubwa katika jamii. Inadaiwa kuwa vitendo hivyo vilianza kupungua baada ya kuwagusa watu mashuhuri, akiwamo aliyekuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Makungu, pamoja na mtoto wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume. Hata hivyo, dalili zinaonyesha kuwa mtindo huo sasa unarejea kwa sura mpya.
Zamani vitendo hivi vilihusishwa na makundi yaliyoitwa Janjaweed na baadaye Mazombi, lakini sasa vinaonekana kuhamia hata katika kampuni binafsi za ulinzi.
Tukio la hivi karibuni katika Hospitali ya Abdulla Mzee huko Pemba limezua taharuki kubwa baada ya kijana mmoja kudaiwa kupigwa kikatili kwa kosa la kutaka kumtembelea mgonjwa nje ya muda uliopangwa.
Badala ya kufuata utaratibu wa kumtoa nje, walinzi watatu wa kampuni binafsi walidaiwa kumshambulia kwa bakora na hata kutumia shoti ya umeme.
Picha zilizosambaa mitandaoni zikimuonyesha kijana huyo akipigwa ziliibua hasira na masikitiko kwa wengi. Tukio hilo limezua mjadala mpana kuhusu mipaka ya mamlaka ya walinzi binafsi na wajibu wao wa kuzingatia sheria. Ni tukio linalogusa moja kwa moja haki za binadamu na hadhi ya utu.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, lilithibitisha kupokea taarifa za tukio hilo na kuwakamata watuhumiwa kwa uchunguzi. Hatua hiyo ni muhimu na inapaswa kupongezwa, kwa sababu inaonyesha bado kuna jitihada za kurejesha imani ya wananchi kwa vyombo vya dola. Hata hivyo, kilicho muhimu zaidi ni kuhakikisha kuwa mchakato wa kisheria unafanyika kwa uwazi na haki inatendeka bila upendeleo.
Kinachotia wasiwasi zaidi ni madai ya matumizi ya umeme kama chombo cha mateso. Ikiwa ni kweli, basi ni ukiukwaji mkubwa wa haki za msingi za binadamu.
Wananchi hawawezi kukubali kuona vitendo kama hivyo vikifumbiwa macho au kushughulikiwa kimyakimya kana kwamba si kosa kubwa.
Wakati wananchi wanaaswa kutokuchukua sheria mkononi ni wajibu pia kwa vyombo vya dola kuhakikisha wale wanaokiuka sheria, wakiwamo askari, wanachukuliwa hatua kali. Sheria inapaswa kuwa kwa wote bila ubaguzi.
Wazanzibar wanahitaji kuishi kwa usalama na heshima bila hofu ya kudhalilishwa. Kuendelea kwa vitendo hivi kunaweza kuchochea hasira na hata kulipiza kisasi, hali ambayo inaweza kuhatarisha amani na utulivu kwa wananchi.
Ni wakati sasa wa kuchukua hatua madhubuti kukomesha kabisa utamaduni wa vipigo holela. Kulinda amani ya nchi kunahitaji si tu uwepo wa sheria, bali pia utekelezaji wake kwa haki na usawa kwa kila mmoja.