
Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limeilenga kamandi ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni iliyoko katika eneo la kaskazini la Safed katika wimbi jipya la mashambulizi ya makombora.
IRGC imetangaza Jumatano kuwa imefanya wimbi la 80 la mashambulizi ya kulipiza kisasi katika fremu ya Operesheni “Ahadi ya Kweli 4” dhidi ya maadui wa waliovamia Iran yaani Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vituo vya kijeshi vya utawala wa Kizayuni wa Israel vilivyoko katika sehemu za kaskazini za ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu vimelengwa kwa mashambulizi mazito na ya mfululizo ya makombora yaliyorushwa na Kikosi cha Anga na Anga-Nje cha IRGC.
IRGC imesema wimbi hili la mashambulizi ya kulipiza kisasi limefanywa kwa kuunga mkono operesheni za kujivunia za Hizbullah wa Lebanon na pia kwa mshikamano na watu waliodhulumiwa wa kusini mwa Lebanon.
Kwa mujibu wa IRGC, operesheni hii imelenga kamandi ya kijeshi ya jeshi la Israel iliyoko kaskazini mwa mji wa Safed, ambayo ina jukumu la kuongoza shughuli za mashambulizi i kando ya mipaka ya kaskazini ya Palestina.
IRGC imesisitiza kuwa operesheni hii ni mwanzo wa mfululizo wa hatua zilizokuwa zimetangazwa hapo awali dhidi ya utawala wa Israel ambao ni maarufu kwa mauaji ya watoto, ikiongeza kuwa maeneo ya vikosi vya Israel katika kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na katika Ukanda wa Gaza yatakabiliwa na mashambulizi makali ya makombora na ndege zisizo na rubani kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bila kusita.
Aidha, IRGC imeongeza kuwa malengo yaliyo ndani kabisa ya maeneo yanayokaliwa, ikiwemo Tel Aviv, Kiryat Shmona na Bnei Brak, pamoja na kambi za jeshi la Marekani katika nchi za Kiarabu kama vile Kituo cha Anga cha Ali Al Salem, Camp Arifjan, Kituo cha Anga cha Al Azraq, na Kituo cha Anga cha Shaikh Isa, yalishambuliwa kwa makombora ya mafuta ya kimiminika na imara yenye usahihi wa hali ya juu pamoja na ndege za kivita zisizo na rubani zenye nguvu ya uharibifu.
Wakati huo huo, Idara ya Mahusiano ya Umma ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, imetangaza kuwa makombora ya “Qadir” ya Pwani‑kwa‑Bahari ya Jeshi la Wanamaji yamelenga meli kubwa ya kivita ya Marekani yenye uwezo wa kusheheni ndege ya “Abraham Lincoln” na kuilazimisha kubadili mwelekeo wake.
Admeri Shahram Irani, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji, ambaye binafsi ametoa amri ya kurushwa kwa makombora ambayo yamelenga manowari ya USS Abraham Lincoln, sambamba na kuwaenzi mashahidi shujaa wa manowari “Dena” iliyolengwa kinyume cha sheria na Marekani amesema: “Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa azimio thabiti na uimara wa mamlaka kamili ya baharini ya Iran katika Ghuba Uajemi, na ulinzi makini wa Lango Bahari la Hormuz, pamoja na uangalizi madhubuti juu ya misafara ya kijeshi, halitasita hadi kulipiza kisasi cha damu ya mashahidi wetu wapendwa.
Admeri Irani ameongeza kuwa: Harakati na mienendo ya kikosi hasimu cha manowari zinazoadhamana na USS Abraham Lincoln daima inafuatiliwa kwa karibu na Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na mara tu kitakapokuwa ndani ya upeo wa mifumo ya makombora ya Iran, kitakuwa shabaha ya mashambulizi makali ya Jeshi la Wanamaji.