Ingawa rasimu ya maandishi ilifanyiwa marekebisho kidogo wakati wa kikao hicho cha dharura kilichofanyika mjini Geneva Uswisi, mwelekeo wake mkuu umebaki kuwa ule ule “kulaani wazi wazi mashambulizi makubwa sana ya Iran dhidi ya nchi za Ghuba”.

Azimio hilo pia linataka kusitishwa kwa “mashambulizi yote yasiyo na uchokozi dhidi ya Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia, Emarati na Jordan”.

Hata hivyo, katika azimio hilo hakuna rejea ya mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran yaliyosababisha vita, jambo lililomulikwa na Indonesia wakati wa mjadala huo wa dharura.
“Maandishi haya hayashughulikii mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, pamoja na mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon, ambayo yanaendelea kuzidisha hali tete,” mujumbe huyo ameliambia Baraza.

Kati ya nchi zaidi ya 65 zilizozungumza leo, Uswisi imeeleza kuunga mkono azimio hilo, ikisema “tunaamini mashambulizi ya Iran yanazidi haki ya kujilinda kisheria.”

Baraza pia limekubali kufanya “Mdahalo wa Dharura” mwingine kuhusu shambulio la shule ya Minab nchini Iran lililosababisha vifo vya watoto 168, kufuatia ombi la Iran pamoja na China na Cuba.

Kamishina Mkuu wa UN wa Haki za Binadamu akihutubia Baraza la Haki za Binadamu Geneva Uswisi

Kamishina Mkuu wa UN wa Haki za Binadamu akihutubia Baraza la Haki za Binadamu Geneva Uswisi

Mashambulizi yanazua hofu chini za sheria za kimataifa

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, akihutubia Baraza hilo wakati wa mdahalo huo wa dharura kupitia ujumbe wa video kuhusu athari za mashambulizi ya Iran kwa nchi za Ghuba na Jordan ameonya kuwa “Zaidi ya wiki tatu tangu Marekani na Israel zianzishe mashambulizi dhidi ya Iran, mzozo unaenea na kuongezeka katika eneo hili na kwingineko, huku raia wakibeba mzigo mkubwa”.

Amesema “Hall hiyo ni hatari sana na haitabiriki, na imeleta machafuko katika eneo lote, ikiathiri Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, Jordan na kwingineko.” 

Ameongeza kuwa tangu kuanza kwa mapigano, Iran imezindua idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani au droni na makombora dhidi ya vituo vya kijeshi, maeneo ya makazi na miundombinu ya nishati katika nchi hizo. Mashambulizi hayo yamesababisha madhara makubwa kwa raia, ikiwemo vifo na majeruhi kadhaa.

Bandari, miundombinu ya nishati, viwanja vya ndege, mifumo ya maji na majengo ya kidiplomasia pia vimeharibiwa, na hivyo kuvuruga huduma muhimu na kuongeza hatari kwa raia.

Türk amesema “Mashambulizi mengi katika mzozo huu yanazua wasiwasi mkubwa chini ya sheria za kimataifa, ambazo zinakataza kulenga raia na miundombinu yao, pamoja na mashambulizi ya kijeshi ambapo madhara kwa raia ni makubwa kupita kiasi,”.

media:entermedia_image:469c6b37-7f4d-4093-8740-47935195a423

UN Human Rights Council/Hongdao Yang

Balozi Ali Bahreini wa Iran akihutubia Baraza la Haki za Binadamu kuhusu mgogoro baina ya Israel, Iran na Marekani

Iran: Hospitali na shule nyingi zimeshambuliwa

Kwa upande wake Mwakilishi wa Iran kwenye mjadala huo ameeleza kuwa mashambulizi ya Israel na Marekani tangu tarehe 28 Februari 2026 yamesababisha uharibifu wa karibu nyumba 45,000, pamoja na kulengwa kwa hospitali 53 na shule 57.

“Leo, Iran inaomboleza vifo vya zaidi ya watu 1,500, wakiwemo watoto 300,” amesema balozi Ali Bahreini.

Pia amesisitiza shambulio la shule ya msingi mjini Minab siku ya kwanza ya vita, lililosababisha vifo vya takriban watu 150, wengi wao wakiwa wanafunzi.

Wakati huo huo, Emarati imelaani mashambulizi ya Iran, ikisema haijawahi kuruhusu anga yake kutumika kushambulia Iran.

“Kinachopuuzwa ni mgongano kati ya kauli za Iran kuhusu uhusiano mwema wa ujirani na vitendo vyake, ikiwemo kuhalalisha mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu kama viwanja vya ndege, bandari na vituo vya mafuta,” amesema balozi Jamal Al Musharakh wa Emarati.

Picha ya satelaiti ya Mlango-Bahari wa Hormuz, ikionyesha njia nyembamba ya maji kati ya Peninsula ya Arabia na Peninsula ya Musandam ya Oman.

© NASA/GSFC/Jacques Descloitres

Picha ya satelaiti ya mlango wa bahari wa Hormuz

IMO yajiadili Mlango Bahari wa Hormuz na Iran

Shirika la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Baharini IMO, limethibitisha kuwa limezungumza na Iran ili kubaini vigezo vinavyotumika kuruhusu meli kupita katika Mlango Bahari wa Hormuz.

Katika barua mahsusi iliyoilekeza kwa IMO tarehe 22 Machi Iran imeeleza kuwa mlango huo bado uko wazi na meli zote “zisizo na uhasama zitaruhusiwa kupita salama”.

Hata hivyo, meli zinazohusishwa na Marekani na Israel pamoja na washirika wao hazitaruhusiwa kupita kwa uhuru.

Shirika hilo limesema baadhi ya meli hazitaruhusiwa kupita na mazungumzo zaidi yanahitajika, huku likisisitiza kuwa kipaumbele chake ni kuwaokoa mabaharia 20,000 waliokwama magharibi mwa Mlango Bahari wa Hormuz.

Shirika hilo limeongeza kuwa “Mabaharia wanatoka mataifa mbalimbali na hawahusiani na mzozo huu wanafanya kazi yao tu”.

Jua linapochomoza nyuma ya moshi mkubwa wa viwanda unaoinuka juu ya eneo la jiji la Tehran nchini Iran.

Domain ya Umma

Tehran, Iranmoshi ukitanda angani kufuatia mashambulizi ya Israel na Marekani

Mashambulizi yanaendelea

Wakati Baraza hilo la Haki za Binadamu likijadili mzozo huo, ripoti za vyombo vya habari zinaonesha kuwa mashambulizi ya makombora yanaendelea katika eneo hilo.

Kuwait na Bahrain zimeripotiwa kushambuliwa na Iran ndani ya saa 24 zilizopita.

Wakati huo huo, wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya mji mkuu wa Iran, Tehran, limeanzishwa na Israel.

Watu tisa wameripotiwa kuuawa nchini Lebanon kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel, ingawa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa walioko mji mkuu Beirut wameripoti usiku tulivu zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *