Duru za kiuchumi za kimataifa zinasema mgogoro uliojitokeza kutokana na uchokozi na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umelishtua na kuliacha bara la Ulaya katika hali ya sintofahamu.

Jarida la The Economist limeeleza katika ripoti yake, kuwa Ulaya bado haijapona kutokana na athari mbaya za mgogoro wa nishati wa 2022 uliosababishwa na vita vya Ukraine, na kuandika kwamba Ulaya sasa inakabiliwa na mgogoro mpya na kwamba matokeo ya uchokozi wa pamoja wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran yameishangaza na kuiacha Ulaya katika hali ya kupigwa na butwaa.

Ripoti ya The Economist inasema: “Ongezeko kubwa la bei ya mafuta na gesi kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran limetishia ukuaji dhaifu wa uchumi wa Ulaya na kuongeza hatari ya kurudi kwenye mfumuko wa bei, na viwanda vya Ulaya, ambavyo viko chini ya mashinikizo kutokana na ushuru wa Marekani na ushindani wa China, vinaiona hali hii kuwa yenye gharama kubwa sana.”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Ulaya imeshindwa kuwa na msimamo mmoja wa kukabiliana na mgogoro huu na kwamba mwitikio wake wa kivitendo umekuwa finyu na dhaifu. Mizozo ya kidiplomasia, uwezo mdogo wa kijeshi na utegemezi mkubwa kwa nishati ya kuagizwa kutoka nje, hasa baada ya kupungua ununuzi wa gesi kutoka Russia, kumeufanya muungano huo kukumbwa na hatari ya mshtuko wa soko la kimataifa. Vilevile, kuongezeka kwa utegemezi katika soko la fedha duniani na uagizaji wa gesi ya LNG kutoka Marekani kama mbadala wa gesi ya Russia pia kumezisha bei za bidhaa mbalimbali, na sasa vita vipya zimezidisha mashinikizo hayo.

Ripoti ya The Economist inaongeza: “Hii ni katika hali ambayo uwezo wa serikali za Ulaya kuingilia kati kiuchumi pia ni mdogo, kwani madeni ya nchi hizo ni makubwa na bajeti zao ni ndogo zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka 2022.”

Likiendelea kuzungumzia athari mbaya za vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran kwa nchi za Ulaya, gazeti la The Economist limeripoti kuwa, ingawa athari za vita vya muda mfupi zinaweza kuwa ndogo, lakini kuendelea kwa matatizo katika usambazaji wa nishati kunaweza kupunguza ukuaji wa uchumi na kuzidisha mfumuko wa bei. Limeongeza kuwa: “Katika ngazi ya kisiasa, Ulaya pia imegawanyika kuhusu jinsi ya kukabiliana na mgogoro huo, kuanzia kuunga mkono kikamilifu mashambulizi hadi ukosoaji wa uhalali wake, na baadhi ya wachambuzi wanauona mgawanyiko huu kama matokeo ya wasiwasi kuhusu uwezekano wa Marekani kuzichukulia hatua nchi hizo.”

Ripoti hiyo inasema, uamuzi wa Marekani wa kuondoa vikwazo vya kununua mafuta ya Russia kwa siku 30 pia umezua wasiwasi barani Ulaya, hata miongoni mwa viongozi ambao awali waliunga mkono mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Mwishoni mwa ripoti yake The Economist imesema, Ulaya inakabiliwa na athari mbaya za vita ambazo haina uwezo madhubuti wa kuzikomesha na kuongeza kuwa: Bara Ulaya pia liko katika hatari ya kuingizwa bila kukusudia kwenye mzozo huo, na kwa sasa, vikosi vya majeshi ya nchi za Ulaya, ikiwa ni pamoja na ndege za kivita za Uingereza na Ufaransa na meli na ndege za Ugiriki, Italia na Uholanzi, vimetumwa kwa ajili ya hatua za kujilinda. Hata hivyo, maafisa wa Ulaya wana shaka kwamba vikosi hivyo vinaweza kuwa na nafasi muhimu, na Ulaya itasubiri huku wengine wakichukua maamuzi kusimamia hali hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *