
Mkuu wa Baraza Kuu la harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Iraq, Al-Nujaba, ametoa wito kwa Bunge na harakati za kizalendo kufuta makubaliano ya usalama na Marekani.
Sheikh Nadhim Al-Saidi ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X: “Kushambuliwa jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi katika maeneo mbalimbali, hasa katika maeneo yanayopakana na Syria, si tukio la kupita, bali ni kitendo kinacholenga kuvuruga usalama wa Iraq.”
Ameongeza kuwa: “Mashambulizi ya anga dhidi ya vikosi vya jeshi la Iraq na kufunguliwa njia kwa ajili ya makundi ya kigaidi vinaonyesha kuwepo mikono ya siri inayolenga kurejesha ugaidi nchini Iraq.”
Al-Saidi ameeleza kuwa: “Kwa miaka mingi, ilisemekana kwamba wanajeshi wa kigeni hapa nchini ni maafisa wa ushauri, lakini damu ya wapiganaji wa vikosi vya kujitolea vya wananchi (al Hashdu Shaabi) na jeshi inathibitisha kuwa madai hayo ni ya uongo.”
Mkuu wa Baraza Kuu la harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Iraq, Al-Nujaba, amesema: “Damu ya wapiganaji wa kujitolea iliyomwagwa na mashine ya vita ya Marekani na utawala wa Kizayuni imethibitisha kwamba wanajeshi wa kigeni ni vikosi vamizi vinavyotenda kwa mabavu na uonevu; na suala hili linaweka alama kubwa ya kuuliza kuhusu mamlaka ya kujitawala na heshima ya kitaifa ya Iraq.”
“Tunatoa wito kwa Bunge la Iraq na harakati za kizalendo kutumia fursa ya kihistoria iliyojitokeza na kuchukua hatua za kijasiri kufuta makubaliano ya usalama na Marekani, ambayo yamekuwa kifuniko cha uchokozi na uvamizi,” amesema Sheikh Nadhim Al-Saidi.
Ameongeza kuwa: “Kambi za kijeshi za Marekani nchini Iraq zimekuwa mstari wa mbele wa kuulinda utawala wa Kizayuni wa Israel na hazina uhusiano wowote na kutetea uhuru, mamlaka ya Iraq na usalama wa watu wake. Badala yake, zimekuwa jambia linalotumiwa kudunga heshima ya taifa.”
Amesema: Uhuru na kujitawala nchi hakuwezi kulindwa kwa kusaini mkataba wa makubaliano na mvamizi, bali kwa kukomesha kuwepo mvamizi mwenyewe.