
Duru zinadokeza kuwa, Harakati ya Ansarullah ya Yemen iko tayari kuchukua udhibiti wa eneo la kimkakati la Lango Bahari wa Bab al‑Mandab kama sehemu ya hatua za nguvu za Muqawama (Mapambano) za kuwaadhibu maadui walioanzisha hujuma ya kichokozi dhidi ya Iran.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, duru za Ansarullah zimedokeza kuwatangu siku ya kwanza ya Vita vya Ramadhani vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran, harakati hiyo ya Muqawama ya Yemen imekuwa katika hali ya tahadhari kamili na iko tayari kuingia katika uwanja wa mapambano.
Afisa wa Ansarullah ambaye hakutaka jina lake litajwe amesisitiza kuwa: “Iwapo kutahitajika kudhibiti Lango Bahari la Bab al‑Mandab ili kuongeza gharama na adhabu kwa adui, mashujaa wa Ansarullah wa Yemen wako tayari kikamilifu kutekeleza jukumu hili muhimu.”
Wakati huo huo, chanzo hicho kilibainisha kwamba Ansarullah tayari wameonyesha kuwa kufunga Lango Bahari la Bab al‑Mandab na kutekeleza matakwa ya harakati ya Muqawama katika Bahari Nyekundu ni jambo rahisi kwao.
Hapo awali, chanzo cha kijeshi kilikuwa kimeiambia Tasnim kwamba “iwapo adui ataamua kuchukua hatua za uchokozi kusini mwa Iran, kunaweza kufunguliwa medani mpya za mapambano ambazo zitamshangaza adui.”
Chanzo hicho kimeongeza kuwa: “Ikiwa adui atajaribu kuchukua hatua za kijeshi katika visiwa vya Iran au sehemu nyingine yoyote ya ardhi yetu, au kujaribu kuilazimisha Iran kubeba gharama kupitia harakati za kijeshi za majini katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman, tutafungua medani nyingine za mapambano kwa mshangao, ili hatua yao isiwe na faida yoyote bali iongeze gharama zao mara dufu.”
Lango la Bahari la Bab al‑Mandab liko kati ya Bahari ya Shamu (Bahari Nyekundu) na Ghuba ya Aden, likitenganisha Yemen katika Rasi ya Uarabuni na nchi za Djibouti na Eritrea katika Pembe ya Afrika. Ni njia muhimu sana ya kimkakati kwa sababu meli nyingi za biashara na za mafuta hupita hapo zikisafiri kati ya Ulaya, Asia na Mashariki ya Kati kupitia Mfereji wa Suez. Umuhimu wake ni kwamba hufanya biashara ya kimataifa kuwa rahisi na ya haraka; kama njia hii itazuiwa au kuwa na migogoro, usafirishaji wa mafuta na bidhaa duniani unaweza kuchelewa na gharama za biashara kuongezeka. Ndiyo maana Bab al‑Mandab inachukuliwa kuwa mojawapo ya lango muhimu zaidi za bahari katika uchumi na usalama wa dunia.