.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa

Muda wa kusoma: Dakika 7

Tarehe 17 mwezi Juni, nyota wa Argentina, Lionel Messi, alipofunga bao lake la kwanza katika Kombe la Dunia la 2026 na kuipa taifa lake ushindi dhidi ya Algeria, wengi walishangilia ushindi huo.

Ila hakukuwa na raia wengi kutoka Argentina uwanjani.

Kati ya nchi kumi zenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani, ni mbili tu Marekani na Brazil zinashiriki katika mashindano ya mwaka huu.

Nchi nyingine mbili zenye idadi kubwa ya watu duniani, Urusi na Nigeria zimewahi kushiriki Kombe la Dunia hapo awali.

China na Indonesia kila moja imewahi kushiriki katika mashindano hayo makubwa zaidi ya soka duniani mara moja tu.

India nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani, Bangladesh, Ethiopia na Pakistan bado zinaendelea kutumai siku moja watafuzu kwa Kombe la Dunia.

India ilifuzu rasmi kushiriki Kombe la Dunia la mwaka 1950 nchini Brazil, lakini ilijiondoa chini ya mwezi mmoja kabla ya mashindano hayo kuanza.

“Haikubaliki kabisa kwamba nchi ambayo mamilioni ya watu wake wanaipenda soka imebaki nyuma kwa kiwango kikubwa katika mchezo huo,” alisema mwigizaji maarufu wa Bangladesh, mwandishi na shabiki wa soka, Odite Karim, akizungumza na BBC

Kwa nini ukubwa wa idadi ya watu hauhusiani moja kwa moja na mafanikio ya soka?

Je, idadi ya watu ina mchango wowote?

Kwa mtazamo wa haraka, unaweza kufikiri nchi yenye watu wengi kama India au Pakistan ingeweza kuwa na wachezaji wengi bora zaidi kuliko nchi ndogo kama Argentina au Uruguay. Lakini katika uhalisia, soka la kiwango cha juu linategemea zaidi “ubora wa mfumo” kuliko “wingi wa watu”.

Kwanza, maendeleo ya miundombinu na uwekezaji. Nchi zinazofanya vizuri mara nyingi zina viwanja vingi vya mazoezi, ligi zenye ushindani, na vilabu vinavyowekeza katika shule za mafunzo kwa vijana. Bila mfumo huu, vipaji vingi vinaweza kuwepo lakini havipati nafasi ya kukuzwa.

Pili, utamaduni wa soka na historia yake. Nchi kama Brazil, Argentina, Ujerumani au Ufaransa zina historia ndefu ya soka kama sehemu ya maisha ya kila siku. Hii huongeza ushiriki wa watoto na ubora wa ushindani tangu utotoni. Katika baadhi ya nchi zenye watu wengi, michezo mingine kama kriketi au riadha hupewa kipaumbele zaidi.

Tatu, ubora wa mafunzo na ukufunzi. Kocha mwenye ujuzi na mifumo ya kisasa ya mafunzo huchangia sana katika maendeleo ya mchezaji. Nchi nyingi zinazoanza kukuza soka zinakosa wigo mpana wa makocha wenye viwango vya juu.

Nne, miundombinu ya ligi ya ndani. Ligi imara ya kitaifa husaidia wachezaji kupata uzoefu wa ushindani wa mara kwa mara. Bila ligi yenye nguvu, vipaji vinaweza kupotea au kukosa changamoto ya kuboreka.

Tano, uwezekano wa kiuchumi na msaada wa kitaasisi. Nchi tajiri au zilizo na utulivu wa kisiasa mara nyingi zinaweza kuwekeza zaidi katika michezo. Hii haina uhusiano wa moja kwa moja na idadi ya watu.

Idadi kubwa ya watu ni kama “hifadhi kubwa ya vipaji”, lakini bila mfumo wa kuvigundua, kuvilea na kuvipandisha kiwango, vipaji hivyo havigeuki kuwa timu imara ya taifa.

Kwa mtazamo wa watu wengi, kadri nchi inavyokuwa na idadi kubwa ya watu, ndivyo inavyokuwa na uwezekano mkubwa wa kupata wachezaji wengi wenye vipaji ila hali si hivyo.

Nchi saba kati ya nane zilizowahi kushinda Kombe la Dunia Argentina, Brazil, England, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uhispania zina idadi ya wastani ya watu.

Hata hivyo, ukubwa wa idadi ya watu ni moja tu kati ya mambo kadhaa muhimu, kama anavyoelezea mwanasayansi na mwanauchumi wa Uingereza Stefan Szymanski.

“Soka inafanana sana na jinsi uchumi wa kitaifa unavyofanya kazi. Ili ustawi, unahitaji watu. Lakini zaidi ya hapo, unahitaji mtaji na miundombinu,” anasema Szymanski, mwandishi mwenza wa kitabu cha Soccernomics.

Szymanski anaelezea kwamba idadi kubwa ya nchi zilizofanikiwa katika soka pia zina sifa nyingine muhimu, ambao ni utajiri.

Katika kitabu cha Soccernomics, Szymanski na mwandishi mwenza Simon Kuper walihitimisha kwamba nchi kwa kawaida huhitaji kipato cha wastani kwa kila mtu cha angalau dola 15,000 kwa mwaka ili kushinda mashindano makubwa ya soka.

Hata hivyo, Brazil na Argentina, ambako kipato cha wastani kwa kila mtu kiko chini ya kiwango hicho, kwa pamoja zimejishindia mataji manane ya Kombe la Dunia.

Kulingana na mwanauchumi huyo wa Uingereza, hili linaonyesha umuhimu wa kipengele cha tatu, mila za soka na uzoefu uliokusanywa kwa muda mrefu.

“Uzoefu huja na muda.”

“Kujitahidi kuwafikia waliotangulia”

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Nchi zenye mafanikio zaidi katika soka ikiwemo zile zinazoshiriki mara kwa mara mashindano ya Kombe la Dunia, pia ndizo zenye historia ndefu zaidi ya mashindano ya kimataifa ya soka.

Hii inaeleza, kwa nini Uruguay, yenye idadi ya watu takribani milioni 3.5 tu, iliweza kushinda Kombe la Dunia mara mbili mwaka 1930 na 1950. Timu ya La Celeste ilicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa mwaka 1902, ambapo ilifungwa mabao 6-0 na Argentina. Hii ilitokea miaka 12 kabla ya Brazil kucheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa.

Nchi za Afrika na Asia Kusini ambazo zilipata uhuru baadaye sana, au ambazo soka lilianza kuendelezwa kikamilifu hivi karibuni, zililazimika kuweka juhudi kubwa kufikia pengo hilo.

Baadhi zimefanikiwa. Morocco, ambayo ilipata uhuru kutoka Hispania na Ufaransa mwaka 1956, ni timu ya kwanza na hadi sasa timu pekee kutoka Afrika kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia katika mashindano ya 2022 nchini Qatar.

Korea Kusini, ambayo ilishirikiana kuwa mwenyeji wa mashindano ya 2002 pamoja na Japan, ndiyo timu pekee ya Asia iliyowahi kufika hatua ya nne bora.

“Lakini kuna nchi nyingine kama Indonesia, India, Bangladesh na kadhaa ambazo bado hazijaweza kuziba pengo hilo,” anaelezea Szymanski.

Kulingana na mwanauchumi huyo, sababu kuu ni ukosefu wa rasilimali na uwezo wa kiutawala. Hata hivyo, anaamini kwamba hata kwa uwekezaji mkubwa zaidi, nchi hizi bado zitapata changamoto kubwa kuifikia miamba ya soka kutokana na ukosefu wa uzoefu na mila za muda mrefu za soka.

Migogoro ya Ethiopia

.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Ethiopia haijawahi kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Mafanikio yake makubwa pekee ya kimataifa yanabaki kuwa kushinda Kombe la Afcon mwaka 1962.

Wakati Ethiopia ilikuwa karibu zaidi kufuzu Kombe la Dunia ilikuwa katika mchujo wa Kombe la Dunia la 2014. Timu yake ilifikia hatua ya mwisho ya mchujo, lakini ikapoteza dhidi ya Nigeria kwa jumla ya mabao.

Leo hii, soka ya Ethiopia, kama vyombo vya habari vya nchini humo vinavyoelezea, inakabiliwa na uhaba mkubwa wa uwekezaji.

Moja ya mifano inayoonekana wazi ni hali ya Ligi Kuu ya taifa hilo ambayo inakumbwa na uhaba wa viwanja vinavyokidhi viwango hitajika vya kuandaa mechi za soka.

“Tumeandaa zaidi ya mechi 380 msimu huu tukitumia viwanja vitatu tu vilivyothibitishwa,” alisema mtendaji mkuu wa Ligi Kuu ya Ethiopia, Kifle Seife, akiliambia gazeti la The Reporter tarehe 27 mwezi Juni.

Uhaba wa viwanja vinavyofaa pia uliathiri timu ya taifa ya Ethiopia ambapo ililazimika kucheza mechi zake za nyumbani katika michuano ya kufuzu ya AFCON nchini Morocco.

Mchezo wa Kriketi Asia Kusini ni kikwazo au kisingizio?

.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Baadhi ya nchi kwa kiwango fulani huwa “mateka” wa mafanikio yao katika michezo mingine. India, kwa mfano, ni moja ya mataifa yenye nguvu kubwa duniani katika mchezo wa kriketi, na ligi yake ya Indian Premier League (IPL), inachukuliwa kuwa ligi tajiri zaidi ya kriketi duniani.

Kulingana na mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya India, Shyam Thapa, hali hii inaleta changamoto kubwa kwa soka katika kuvutia vipaji vya vijana. Mafanikio ya IPL yamepelekea wazazi wa tabaka la kati na la juu kuwafanya watoto wao kuegemea zaidi katika kriketi badala ya soka.

“Wazazi wanahitaji kuelewa kwamba ukifanya kazi ya soka, unaweza pia kupata kipato kizuri,” Thapa aliiambia BBC

Hata hivyo, mwigizaji, mwandishi na shabiki wa soka kutoka Bangladesh, Odite Karim, anaamini kwamba umaarufu wa kriketi sio kikwazo kikuu.

Anataja Australia na New Zealand, ambazo pia ni mataifa makubwa ya kriketi lakini wakati huo huo zinaendeleza soka kwa mafanikio na hushiriki mara kwa mara Kombe la Dunia.

“Umaarufu wa kriketi ni kisingizio tu,” anasema Karim, akirejelea Bangladesh, ambako mchezo huo pia unapendwa sana.

Je, China ni jitu lililolala?

.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Kesi ya China pengine ndiyo yenye kushangaza zaidi. Ingawa nchi hiyo imekuwa miongoni mwa mataifa yaliyofanikiwa zaidi katika historia ya michezo ya olimpiki katika miongo ya hivi karibuni, imeshindwa kupata mafanikio katika soka ya wanaume.

“Kitaalamu, hakuna sababu ya China kushindwa kuzalisha wachezaji wa soka wa viwango vya juu,” anasema mtaalamu wa soka wa China anayeishi Beijing, Mark Dreyer.

“Tatizo kuu ni kwamba nchini China kila kitu kinadhibitiwa na serikali, na maamuzi hufanywa kutoka juu kwenda chini. Soka inapaswa kuendeshwa na wataalamu wa soka, lakini kuna mwingiliano mkubwa wa kisiasa,”

Timu ya taifa ya China haijafuzu Kombe la Dunia tangu mwaka 2002, licha ya uwekezaji mkubwa katika maendeleo ya soka ulioanza katika miaka ya 2010.

Vilabu vya Ligi Kuu ya China,Chinese Super League viliwaleta wachezaji wengi kutoka Amerika Kusini na Ulaya, kwa lengo la kuinua kiwango cha ligi ya taifa.

Indonesia imeshiriki Kombe la Dunia mara moja tu, mwaka 1938, wakati huo ikiwa chini ya jina la Dutch East Indies, koloni la Uholanzi.

Timu ya taifa ya Indonesia ilipiga hatua kubwa katika mchujo wa Kombe la Dunia la 2026, ikifika hatua ya mwisho ya mchujo.

Hata hivyo, mafanikio haya kwa kiasi kikubwa hayatokani na maendeleo ya wachezaji wa ndani, bali ni matokeo ya sera ya kuwaleta wachezaji wa asili ya Indonesia waliolelewa Ulaya.

“Wakati mwingine, kikosi cha kwanza cha Indonesia kilikuwa na wachezaji wanane au tisa waliozaliwa Ulaya,” anasema mhariri wa habari za BBC Indonesia, Jerome Wirawan.

Pakistan na Bangladesh zilimaliza kampeni zao za kufuzu katika hatua ya makundi ya mchujo wa Asia bila kushinda hata mechi moja katika mechi sita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *