
Kupitia ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X, Tedros amesisitiza kuwa, “afya inapaswa kulindwa kwa gharama yoyote na kamwe isiwekwe katika mikono ya siasa za kijiografia, vikwazo vya nishati na kukatika kwa umeme.”
Ameielezea hali ya Cuba kuwa “inatisha sana,” akibainisha kuwa nchi hiyo inakumbwa na changamoto kubwa katika kuendelea kutoa huduma za afya wakati wa kipindi cha misukosuko mikubwa.
Wagonjwa na wajawazito hatarini
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa WHO, uhaba wa umeme umeathiri kwa kiasi kikubwa hospitali kote Cuba.
“Taarifa zinaonesha kuwa hospitali za Cuba zimekuwa zikihangaika kuendeleza huduma za dharura na uangalizi maalum (ICU),” amesema, akiongeza kuwa “maelfu ya huduma za upasuaji yameahirishwa katika mwezi uliopita.”
Tedros ameonya kuwa hali hiyo inaweka maisha ya wagonjwa hatarini, hasa wale wanaohitaji huduma za haraka. Ametaja kuwa wagonjwa wa saratani na wanawake wajawazito wanaojiandaa kujifungua ni miongoni mwa walioathirika, kutokana na ukosefu wa umeme wa kuendesha vifaa vya tiba na kuhifadhi chanjo katika mazingira salama.
Ingawa amepongeza juhudi za Cuba kurejesha umeme, Tedros amesisitiza kuwa msaada zaidi unahitajika akisema, “hospitali, kliniki na magari ya wagonjwa ya Cuba yanahitajika sasa kuliko wakati mwingine wowote, na lazima yaungwe mkono ili yaendelee kuokoa maisha.”
Amesisitiza kuwa huduma za afya “haziwezi kuachwa katika hali ya kutegemea umeme usiotabirika na siasa za kijiografia.”