
Dar es Saalam. Kila safari ya mafanikio huanza na hatua moja. Kwa baadhi ya watu, hatua hiyo huja kwa kusukumwa na mazingira, kwa wengine ni matokeo ya ndoto walizojijengea kwa muda mrefu.
Kwa Abela John, safari yake ya ujasiriamali ilianza mwaka 2020, akiwa mwanafunzi wa chuo, ambaye tayari alikuwa na mtazamo wa kuona fursa zilizokuwa zimemzunguka.
Akiwa anatoka katika familia ya wafugaji wa kuku, Abela alikua akishuhudia shughuli za ufugaji kwa karibu. Hata hivyo, tofauti na wengi waliotazama biashara hiyo kwa jicho la kawaida, yeye alianza kujihoji.
Alijiuliza kwa nini wafugaji wengi huuza kuku wakiwa wazima badala ya kuwachinja na kuwagawa katika vipande vidogo vinavyoweza kukidhi mahitaji tofauti ya wateja.
Katika tafakari yake, aligundua kuwa si kila mteja anapendelea sehemu zote za kuku. Wapo wanaopendelea mapaja, wengine vidali na baadhi hupendelea vipapatio au migongo. Hapo ndipo wazo la kuongeza thamani likaanza kuchukua nafasi akilini mwake, kwamba kugawa kuku katika vipande kungeweza kuongeza soko na kuwavutia wateja wengi zaidi.
Akiwa bado chuoni, hakusubiri mazingira yawe kamili. Alianza kwa kutumia rasilimali chache alizokuwa nazo, ikiwa ni pamoja na friji ndogo aliyokuwa akiitumia chumbani kwake chuoni hapo.
Ingawa sehemu ya kugandisha ilikuwa ndogo, aliamua kuanza kwa kiwango kidogo. Alinunua kuku kutoka kwa wazazi wake, akawa anawakata katika vipande na kuanza kuwauza kwa marafiki zake wa karibu.
Bei zake zilikuwa za kuvutia, kwa mfano pakiti ya vidali aliiuza kwa Sh4, 000. Hatua hiyo ilimwezesha kuvutia wateja wa mwanzo, huku akijifunza mwenendo wa soko kwa vitendo.
Kadri siku zilivyokwenda, aligundua kuwa mahitaji yalikuwa yanaongezeka na hata faida ndogo aliyokuwa akipata ilimpa motisha ya kuendelea mbele.
Hata hivyo, mafanikio hayo ya awali hayakukosa changamoto. Abela anasema majukumu yake kama mwanafunzi yalikuwa yakimnyima muda wa kusimamia biashara ipasavyo, huku uwezo mdogo wa friji yake ukimlazimu kuuza kwa haraka ili kuepuka hasara.
“Wakati mwingine, kuku wangu waliharibika kwa sababu friji ilikuwa ndogo, wakawa hawagandi vizuri, nikajikuta wanaharibika,” anasimulia Abela.
Hata hivyo, anasema changamoto hizo zilimfanya kufikia uamuzi mgumu wa kusimamisha biashara kwa muda.
Tofauti na wengi wanaoweza kukata tamaa katika hatua kama hiyo, Abela alichagua kuchukua muda huo kama fursa ya kujipanga upya. Anasema alitambua kuwa biashara inahitaji zaidi ya wazo zuri; inahitaji maandalizi, miundombinu na muda wa kuisimamia.
Hivyo anasimulia kuwa alipokuwa anaendelea na masomo yake hadi kuhitimu na baadaye kupata ajira, ndoto ya kurejea kwenye biashara iliendelea kukua kimya kimya ndani yake.
Anasema ulipofika mwaka 2024, aliona wakati umefika wa kuanza upya safari yake na akaanza kuchukua hatua kwa tahadhari zaidi kwa sababu pia alikuwa ni mwajiriwa kwenye moja ya ofisi za Serikali (hakutaka kuweka wazi).
Anasema alinunua jokofu dogo la ujazo wa lita 96 ikiwa ni maandalizi ya kuendelea na biashara yake. Hata hivyo, pamoja na maandalizi hayo, bado alikabiliwa na sintofahamu kuhusu namna ya kuendesha biashara sambamba na ajira yake ya kudumu.
“Nikiwa nyumbani nilikuwa naitazama ile freezer nikiwa na maswali mengi kichwani, nitaanzia wapi, nitapataje wateja na nitasimamiaje biashara wakati nipo kazini kuanzia asubuhi hadi jioni?” anasimulia.
Hata hivyo, anasema Jumamosi moja alikata shauri akiwa na ndugu yake pamoja na dalali, alianza kutafuta fremu ya biashara maeneo ya Mabibo jijini Dar es Salaam.
Anasema alikuwa na Sh100, 000 mkononi akafanikiwa kupata fremu iliyokuwa ndani ya mtaa, eneo ambalo halikuwa na mwonekano mkubwa wa kibiashara, lakini lilikuwa ndani ya uwezo wake kifedha.
Bila kusita, anasema akaamua kufungua biashara yake akiwa na jokofu hilo moja, meza, kiti na mzigo mdogo wa kuku. Anasema hakujua wazi wateja watatoka wapi, lakini aliamua kuamini katika wazo lake.
Kutokana na majukumu yake ya kazi ya ofisini, alilazimika kuajiri msaidizi wa kuuza dukani tangu siku za mwanzo, ingawa alitambua kuwa kibiashara si hatua inayoshauriwa mara nyingi.
Ili kuhakikisha biashara inasonga mbele, anasema alitumia muda wa mwisho wa wiki kuandaa bidhaa akigawa kuku katika vifurushi vya sehemu mbalimbali kama mapaja, vidali, migongo na vipapatio.
Hata hivyo, miezi ya mwanzo haikuwa rahisi. Mwezi wa kwanza haukuwa na mauzo kabisa, na mwezi wa pili ukiwa na hali isiyoeleweka.
“Wateja wachache waliokuja walikuwa wanaulizia bidhaa za bei nafuu kama dagaa, tofauti na kuku niliokuwa nikiwauza. Ilikuwa ni changamoto, lakini sikukata tamaa,” anasema.
Ndipo alipoanza kufikiria upya mkakati wake wa biashara. Alitambua kuwa wateja wengi hupendelea kununua bidhaa mchanganyiko kama inavyofanyika katika maduka makubwa badala ya kununua kitu kimoja kimoja.
Hapo ndipo ubunifu mpya ulipozaliwa.
Abela anasema aliamua kuanzisha mfumo wa vifurushi vya bidhaa ambapo mteja angeweza kupata mchanganyiko wa vyakula katika kifurushi kimoja.
Vifurushi hivyo vilijumuisha kuku, samaki, maharage, mboga za majani na kisamvu na baadaye kuongezwa bidhaa nyingine kulingana na mahitaji ya soko.
Mbali na hilo, alianzisha huduma ya kuwapeleka bidhaa hizo wateja wake moja kwa moja nyumbani, hatua iliyoongeza urahisi na kuwavutia wengi zaidi. Idadi ya wateja ilianza kuongezeka taratibu kutoka kutokuwa na mteja hadi kufikia wateja 10, 20, 100 na sasa zaidi ya 200.
Biashara yake ikaanza kukua, si tu kwa mauzo bali pia kwa uaminifu wa wateja waliokuwa wakirudi tena na tena.
Anasema ubunifu huo ulianza kuzaa matunda. Pamoja na mafanikio hayo, Abela bado anakabiliwa na changamoto ya kukuza mtaji na kuhakikisha anakuwa na akiba ya kutosha ya bidhaa, ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa ubora wa bidhaa ndicho kipaumbele chake kikuu. Anasema anaamini kuwa biashara yoyote inayotaka kudumu lazima ijenge msingi wake katika ubora. Ndiyo maana uhakikisha anapata bidhaa bora kutoka kwa wasambazaji wake na kuepuka mzigo usio na viwango.
Anasema kwa sasa biashara yake imepanuka na kujumuisha bidhaa mbalimbali zaidi ya kuku, ikiwemo samaki, dagaa, maharage, kisamvu, vigisi pamoja na viungo vya chakula.
Ili kurahisisha matumizi kwa wateja, baadhi ya bidhaa kama maharage huandaliwa kwa kuchemshwa mapema.
Bidhaa hizo hupatikana kwa vifurushi vya kuanzia Sh20, 000 na kuendelea, kulingana na mahitaji ya mteja. Mfumo huo umeendelea kuwavutia wateja wanaotafuta urahisi, ubora na mchanganyiko wa bidhaa katika ununuzi wao wa kila siku.
Safari ya Abela ni mfano wa jinsi wazo dogo linavyoweza kukua na kuwa biashara yenye tija, endapo litachangiwa na uthubutu, uvumilivu na ubunifu.
Ni simulizi ya binti aliyeanza na friji ndogo akiitumia bwenini hadi kujenga biashara inayokidhi mahitaji ya wateja wa kisasa.