Morogoro. Wakati wananchi wengi wa Kata ya Lumemo, Halmashauri ya Mji wa Ifakara, mkoani Morogoro, wakikiri kutofahamu kuwa kulima katika maeneo oevu ni uharibifu wa mazingira na ni kinyume cha sheria, Serikali imesema imejipanga kuongeza elimu kwa jamii sambamba na kuimarisha utekelezaji wa sheria za uhifadhi.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa ukosefu wa uelewa kuhusu umuhimu wa kuhifadhi maeneo oevu umechangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa Bonde la Mto Kilombero, moja ya mifumo muhimu zaidi ya ikolojia nchini.

Bonde hilo lina mchango mkubwa katika uzalishaji wa chakula na uhifadhi wa maji yanayochangia uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP).

Hali hiyo inaendelea licha ya kuwepo kwa sheria zinazoelekeza ulinzi wa maeneo hayo. Kifungu cha 55 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 kinakataza shughuli zinazoweza kuharibu mito, kingo za mito, maziwa na maeneo ya ufukwe, huku Kifungu cha 56 kikitoa mamlaka ya kutangaza na kulinda maeneo oevu.

Aidha, Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji ya mwaka 2009, kupitia vifungu vya 34 na 37, inaelekeza kutengwa kwa maeneo tengefu kandokando ya vyanzo vya maji na kupiga marufuku shughuli zinazoweza kuhatarisha ubora na uendelevu wa rasilimali hizo, ikiwemo kilimo na ujenzi ndani ya umbali uliowekwa kisheria.

Pamoja na uwepo wa masharti hayo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa utekelezaji wake bado ni dhaifu.

Wananchi wengi wanasema hawajawahi kupewa elimu kuhusu matakwa ya sheria hizo wala umuhimu wa kuhifadhi maeneo oevu, jambo linalochangia kuendelea kwa shughuli zinazoharibu mazingira.

Kulinda maeneo haya

Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa, akizungumza na Mwananchi, anasema maeneo oevu ni miongoni mwa mifumo muhimu ya ikolojia inayolinda bioanuwai, kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhifadhi vyanzo vya maji vinavyolisha mito mikubwa nchini.

Anasema uharibifu wa maeneo hayo unaathiri si mazingira pekee, bali pia upatikanaji wa maji yanayotumika kuzalisha umeme katika mabwawa makubwa, likiwamo JNHPP.

“Endapo maeneo hayo yataendelea kuharibiwa au kutumiwa isivyo, kasi ya mabadiliko ya tabianchi itaongezeka kutokana na kupungua kwa uwezo wake wa kufyonza gesi joto,” anasema.

Akizungumzia Bonde la Mto Kilombero, anasema shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo zinapaswa kufanyika kwa kufuata taratibu na kuzingatia mipango ya matumizi bora ya ardhi.

“Serikali imekuwa ikichukua hatua za kudhibiti uvamizi wa maeneo oevu kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali, ikiwemo Tamisemi, ambapo mamlaka za mikoa na wilaya zimeelekezwa kuchukua hatua pale sheria zinapokiukwa,” anasema.

Anasema kutokana na ripoti mbalimbali, ikiwemo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Serikali inaendelea kuchukua hatua za kurejesha hali ya awali ya baadhi ya maeneo oevu yaliyoharibiwa kutokana na shughuli za kibinadamu.

Ripoti ya Ukaguzi wa Ufanisi ya CAG ya mwaka 2022 kuhusu uhifadhi na ulinzi wa mifumo ya ikolojia ya ardhi oevu ilibaini udhaifu katika uratibu wa taasisi, kuendelea kwa uharibifu wa vyanzo vya maji na matumizi ya maeneo oevu bila usimamizi madhubuti wa kimazingira.

Kwagilwa anabainisha kuwa changamoto ya mabadiliko ya tabianchi si ya Serikali pekee, bali ni ya jamii, hivyo wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira kwa kupunguza shughuli zinazoharibu mifumo ya asili.

Anasema kila mtu ana wajibu wa kuwa mlinzi wa mazingira, kuanzia ngazi ya kaya, mtu mmoja mmoja hadi taasisi, ili kuhakikisha uendelevu wa rasilimali za asili na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.

Wizara ya Maji

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, anasema pamoja na kuimarishwa kwa sera mpya ya maji inayosisitiza si tu utunzaji, bali pia uendelezaji wa vyanzo vya maji, bado elimu kwa wananchi ndiyo silaha muhimu ya kulinda rasilimali hizo.

Anasema mamlaka za mabonde huendelea kufuatilia ubora wa maji na kurejesha maeneo yaliyoharibiwa, lakini juhudi hizo haziwezi kufanikiwa bila wananchi kubadili namna wanavyotumia maeneo ya vyanzo vya maji.

Vilevile, anaonya kuhusu utupaji holela wa vifungashio vya viuatilifu na mbolea, akisema kemikali hizo huingia kwenye vyanzo vya maji na kuhatarisha afya za binadamu na viumbe wengine.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa baadhi ya wananchi, wakiwamo wa Mang’ula mkoani Morogoro, hutupa holela vifungashio vya pembejeo za kilimo, ambavyo huingia mtoni.

“Wizara ya Maji huwa hatugawi maji kwa wananchi bila kuchukua sampuli na kuyapima,” anasema.

Anasema iwapo changamoto yoyote itabainika, hurudi kuangalia kuanzia kwenye vyanzo ili kuhakikisha usalama wa maji hayo. Hatua hizo zinafanyika katika mabonde yote tisa yaliyopo nchini, likiwamo Bonde la Kilombero.

“Hii inaleta matokeo chanya, si kwenye Bonde la Kilombero pekee. Tuna vyanzo vingi, lazima tuvitunze; vinginevyo vizazi vyetu vitateseka,” anasema.

Anaeleza nchi inahitaji wakulima, wafugaji na wachimba madini, lakini wote lazima waratibiwe ili wafanye shughuli zao bila kuathiri vyanzo vya maji.

Mkakati wa Tanesco

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange, anasema uhifadhi wa Bonde la Kilombero ni suala la kimkakati kwa sababu ndilo linalochangia maji mengi yanayoingia katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP).

Anasema asilimia 52 ya umeme unaozalishwa nchini kwa sasa unatokana na bwawa hilo, hivyo uharibifu wa vyanzo vya maji unaweza kuwa na athari kwa usalama wa nishati nchini.

“Katika Bwawa la Julius Nyerere, Serikali imewekeza zaidi ya Sh6 trilioni, hivyo ni wajibu wetu sote kulilinda na kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” anasema.

Anasema Tanesco inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kufuatilia athari za kimazingira, hususan katika maeneo ya vyanzo vya maji vinavyolisha mfumo huo.

Twange anasema changamoto zilizopo ni pamoja na baadhi ya wananchi kuingiza mifugo katika maeneo nyeti na kufanya shughuli za kilimo karibu na vyanzo vya maji.

“Kikubwa kinachohitajika kwa sasa ni kutoa elimu kwa wananchi na kuimarisha udhibiti. Huenda si kila anayevamia eneo la chanzo cha maji anafanya hivyo kwa makusudi au kwa nia mbaya; wengine huenda hawafahamu madhara yanayoweza kutokea,” anasema, na kuongeza:

“Mtu anaweza kuona eneo lenye unyevunyevu na maji ya kutosha, akaanza kulima kwa lengo la kujipatia kipato bila kutambua athari zake kwa mazingira na vyanzo vya maji.”

Kwa mujibu wa Twange, wamejipanga kutoa elimu kwa wananchi kuanzia kwa viongozi wa vijiji na vitongoji hadi kwa wakazi wa maeneo husika.

“Wenyeji na wageni wanaofika katika maeneo hayo wanapaswa kupewa elimu kuhusu umuhimu wa kuyahifadhi na madhara yanayotokana na uharibifu wa mazingira. Vivyo hivyo, mifugo inayohamishwa kutoka eneo moja kwenda jingine inapaswa kusimamiwa kwa karibu kupitia viongozi wa maeneo husika,” anasema.

Twange anasema kuna haja ya kuimarisha mifumo ya kisera, akitoa mfano kuwa masuala yanayohusu kilimo katika maeneo ya vyanzo vya maji yanahitaji mwongozo madhubuti kutoka mamlaka za kilimo, huku usimamizi wa mifugo inayohama ukihitaji uratibu wa karibu kutoka sekta husika.

Fundi Sanifu wa Hidrojia wa Bonde la Rufiji, Gerald Hamisi, aliyepo Kituo cha Kilombero, anasema wamekuwa wakitoa elimu kwa wakulima na wafugaji kuhusu kuhifadhi vyanzo vya maji.

Anasema bodi zote za mabonde zilizopo Tanzania zimepewa mamlaka kisheria kuunda jumuiya za watumia maji.

Katika sehemu ya mwisho kesho, tutaangazia jinsi wadau wanavyopendekeza hatua za kunusuru maeneo hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *