Mbeya. Serikali ya Jiji la Mbeya kwa kushirikiana na Bodi ya Filamu nchini imemaliza mgogoro uliokuwa umeibuka kati ya wafanyabiashara na wasambazaji wa Movies, Muziki na Filamu dhidi ya Kampuni ya Umoja Movies Distributers, huku pande zote zikikubaliana kurejea kufanya kazi kwa ushirikiano.

Mgogoro huo ulijitokeza Machi 13, 2026 baada ya wafanyabiashara kulalamikia baadhi ya mawakala wa kampuni hiyo kukusanya Sh10,000 na kuhoji uhalali wao, hali iliyoambatana na madai ya vitisho.

Akizungumza baada ya kikao cha usuluhishi kilichofanyika Machi 26 jijini hapa, Ofisa Utamaduni wa Jiji la Mbeya, Nimwindael Joseph amesema chanzo kikubwa cha mgogoro huo kilikuwa ni ukosefu wa uelewa kuhusu majukumu ya kampuni hiyo.

Alisema baada ya kutoa elimu, pande zote zimeelewana na kukubaliana kufanya kazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

“Kila mmoja sasa ametambua wajibu wa mwenzake. Serikali imeweka mazingira ya haki kwa kila upande na hatutarajii tena kuona mivutano ya aina hiyo,” amesema.

Alisisitiza umuhimu wa mikataba na makubaliano ya kibiashara ili kuepusha migogoro, akibainisha kuwa kampuni hiyo inatambulika rasmi na inafanya kazi kwa mujibu wa sheria chini ya Bodi ya Filamu.

Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo wa Bodi ya Filamu, Omary Mbano alisema taasisi hiyo ina jukumu la kisheria la kusimamia na kuratibu shughuli zote za filamu nchini kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1976.

Amesema kikao hicho pia kilitumika kuwatambulisha rasmi Umoja Movies Distributers, huku akieleza kuwa changamoto zilizojitokeza zilitokana na ukosefu wa uwazi na matumizi mabaya ya madaraka kwa baadhi ya wahusika.

“Tumezikutanisha pande zote na kuzifanya zielewane. Hawa ni wadau wanaotegemeana, hivyo ushirikiano wao ni muhimu kwa ukuaji wa soko la filamu,” amesema Mbano.

Ameongeza kuwa serikali inalenga kuona kila mdau ananufaika na fursa zilizopo katika sekta ya filamu, huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimu kazi na kufuata utaratibu.

Katibu Mkuu wa Taasisi ya Mlezi Foundation Taifa, George Mackona amesema kupatikana kwa suluhu hiyo kutasaidia kuwaunganisha vijana na kuwafungulia zaidi fursa za kiuchumi kupitia sekta hiyo.

Amesema wanaendelea kufuatilia mchakato wa kuanzishwa kwa umoja rasmi wa wauzaji na wasambazaji wa kazi za filamu jijini Mbeya ili kuimarisha mshikamano na utambuzi wa kisheria.

Naye Mkurugenzi wa Umoja Movies Distributers, Idrisa Yassin amesema kampuni imechagua kutumia njia ya elimu badala ya hatua za kisheria, akieleza kuwa lengo ni kukuza soko la filamu ambalo kwa sasa limekuwa likiyumba.

Kwa upande wa wafanyabiashara, Cleopart Mzumbwe alisema kikao hicho kimewasaidia kuwasilisha changamoto zao na kupata majibu, akieleza kuwa wana matumaini ya ushirikiano mzuri zaidi baada ya mgogoro huo kumalizika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *