
Moshi. Familia ya aliyekuwa mfanyabiashara maarufu mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, Bosco Chuwa (67) imesema licha ya mpendwa wao kuonekana mwenye afya njema, alifariki dunia ghafla barabarani baada ya kuhisi hali yake siyo nzuri alipokuwa akiendesha gari.
Chuwa alikutwa na mkasa huo mchana wa jana Jumapili, Julai 5, 2026 alipokuwa akiendesha gari ambapo alilazimika kusimamisha pembeni mwa barabara kisha kuwasha taa za hatari ‘hazard.’
Leo Jumatatu, Julai 6, 2026, Mwananchi limefika nyumbani kwa Chuwa, Mtaa wa Kambaita, Kata ya Soweto, Moshi Mjini kunapofanyika taratibu za mazishi na kuzungumza na msemaji wa familia, Allen Mtowe.
Kuhusu mazingira ya kifo hicho, Mtowe amesema marehemu hakufia nyumbani bali changamoto ya kiafya ilimwanzia akiwa barabarani baada ya kuhisi hali yake siyo nzuri alipokuwa akiendesha gari na hivyo kuegesha gari pembeni ya barabara.
Amesema Chuwa alisimamisha gari pembeni ya barabara (hakueleza ni wapi) na kuwasha taa za kuashiria hatari (hazard), ndipo wananchi walipobaini gari hilo lilikuwa limesimama kwa muda mrefu na kuanza kufuatilia hali yake.
“Walipofika walimkuta akiwa ndani ya gari kama amelala. Wakamtafuta mmoja wa watoto wake ambaye alifika eneo hilo, ndipo jitihada za kumwahisha hospitalini zilipoanza. Madaktari walijitahidi kuokoa maisha yake lakini haikuwezekana,” amesema.
Mtowe amesema familia bado inaendelea na vikao vya ndani huku taratibu za mazishi zikiendelea, na kwamba ratiba rasmi ya mazishi itatangazwa baada ya kukamilika kwa maandalizi.
“Familia kama familia tulikutana jana kidogo lakini leo tumekutana zaidi, na taratibu za mazishi bado zinaendelea. Inawezekana kesho tukawa na nafasi nzuri ya kusema ni lini na wapi mazishi yatafanyika. Kwa sasa bado tunaendelea kusubiri taratibu chache,” amesema Mtowe.
Mtowe amesema familia itaendelea kutoa taarifa rasmi kadri maandalizi ya mazishi yatakavyoendelea.
Wakati familia ikiomba utulivu, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kambaita, Agnes Lyimo amesema kifo cha mfanyabiashara huyo kimeacha pengo kubwa kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na mchango wake katika shughuli za maendeleo na usalama wa jamii.
Lyimo amesema anamfahamu Chuwa tangu mwaka 2002 alipohamia katika mtaa huo uliopo Kata ya Soweto, akieleza kabla hata hajawa kiongozi, walikuwa majirani na alimtambua kama mtu aliyekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii.
Amesema Chuwa alikuwa mdau mkubwa wa ulinzi shirikishi na shughuli mbalimbali za maendeleo katika kata hiyo huku akitoa msaada kila alipohitajika na viongozi pamoja na wananchi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali.
“Tulikuwa tukipata changamoto yoyote tukimfuata alikuwa anatupa msaada. Kwa kweli tumepoteza mtu muhimu sana katika mtaa wetu,” amesema Limo