
Papa Leo wa 14 amepinga majaribio ya kutaka kuhalalisha vita na mauaji kwa kutumia vibaya jina la Mungu, katika matamshi ambayo, kwa mujibu wa Televisheni ya CNN, yamerudi na kupinga madai yaliyotolewa na utawala wa Donald Trump.
“Mungu hasikilizi maombi ya wapenda vita, bali huyakataa,” Papa huyo wa kwanza mzaliwa wa Marekani ameuambia umati wa watu katika Uwanja wa St. Peter leo wakati wa ibada ya Jumapili ya Matawi.
Akikosoa uchochezi wa vita wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, Papa ameongeza kwamba Mungu anapinga vita na “hakuna mtu anayeweza kumtumia [Mungu] kuhalalisha vita.”
Wiki Takatifu na Pasaka ya kwanza ya Papa mpya, Leo XIV, inakuja huku Marekani na Israel zikiendeleza vita na mashambulizi ya kinyama dhidi ya Iran ambayo sasa yamepanuka katika eneo lote la Magharibi mwa Asia.
Kwa mujibu wa Televisheni ya CNN kauli za kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani imetolewa kuashiria maneno ya Waziri wa Vita wa Marekani, Pete Hegseth, ambaye alinukuu maandiko matakatifu akidai Mungu anaunga mkono operesheni za kijeshi za nchi hiyo na Israel nchini Iran ili kuhalalisha vita hivyo.