Dar es Salaam. Wanawake wengi imeelezwa wanapata kipato lakini bado hawajui namna ya kukikuza au kukilinda ili kiweze kudumu kwa vizazi viwili hadi  vitatu vijazo.

Hayo yamesemwa na Mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi Mtendaji wa Studiored Communications (SRC), Dk Doris Rwebangira,   kwenye mkutano wa Women Shaping the Future (WSF 2026),  uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuratibiwa na SRC kwa kushirikiana na benki ya Stanbic.

Dk Doris amesema kutokana na hilo mapato pekee hubaki katika hatari, hasa yanapovurugwa na matukio yasiyotarajiwa.

“Utulivu wa kifedha wa muda mrefu unahitaji mipango ya makusudi, uwezo wa kustahimili misukosuko ya kiuchumi na mikakati ya kuunda fursa endelevu kwa vizazi vijavyo,” amesema Mkurugenzi huyo.

Amesema katika kuendelea kuwajengea uwezo wanawake katika hilo kwenye mkutano huo wamewakutanisha wanawake 200 viongozi wakiwemo wataalamu, wajasiriamali na watunga sera katika programu yenye vipindi vya wataalam, majadiliano ya jopo  vyote vikiwa na lengo la kuwapatia wanawake zana, uelewa na kujiamini ili kuchukua hatua madhubuti kuelekea uhuru wa kifedha.

Amesema mkutano huo wa kila mwaka ambao hii na mara yake ya pili kufanyika wakati wa Mwezi wa Wanawake umebeba kaulimbiu “Jenga Utajiri. Jenga Nguvu.” na matarajio ni kuufanya mfululizo kwa miaka kumi.

Kwa upande wake 
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Benki kwa Makampuni na Uwekezaji kutoka Benki ya Stanbic Tanzania, Ester Manase,  amesema benki hiyo katika mkutano huo ilipeleka utaalam wake katika uwekezaji na usimamizi wa mali, ikithibitisha dhamira yake ya kuendeleza ujumuishaji wa kifedha na uwezeshaji wa wanawake nchini Tanzania. 

“Sisi kama benki tunaamini katika mchango wa wanawake kwa kuwawezesha kufikia malengo yao hivyo kupitia idara yetu inayoshughulika na wateja wa biashara, tuliona umuhimu wa kushirikiana na SRC ili kuchunguza fursa mbalimbali,” amesema.

Naye Meneja wa Bancassurance wa Alliance Life Assurance,  Tumaini Pyanisa, alisisitiza umuhimu wa si tu kujenga utajiri bali pia kuulinda.

“Watu wengi huzingatia kupata kipato na kuwekeza, lakini husahau kulinda mali zao hadi wanapokumbana na changamoto,” alisema Tumaini.

Ofisa Mwandamizi wa Masoko na Mawasiliano wa UTT, Oliver Minja, amesema kuwa kupitia elimu na juhudi mbalimbali, maendeleo yamepatikana katika kuhamasisha uwekezaji kupitia mifuko ya uwekezaji wa pamoja.

“Watu wengi sasa wanaelewa jinsi ya kufanya fedha zao zifanye kazi na kuleta faida, jambo ambalo ni muhimu katika uwekezaji,” amesema Oliver.

Emilian Busara amesema kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia ili fedha wanazopata ziweze kuzaa matunda kupitia uwekezaji kuna haja ya  kuchunguza fursa kama uwekezaji katika hati fungani za serikali, hati za hazina na hisa ambapo zinaweza kuwasaidia wanawake kupanua usalama wao wa kifedha na kujenga utajiri kwa vizazi vijavyo.

“Kwa mfano, watu wengi huwekeza kwa kununua viwanja, jambo ambalo si baya, lakini mara nyingi fedha hizo hazizai faida kwa i kuna njia nyingine nyingi za uwekezaji zinazoweza kuleta faida zaidi kama mtu atakuwa na nidhamu na mkakati,” amesema Emilian.

Aliongeza kuwa wakati umefika kwa watu kuacha tu kuhifadhi fedha bila kuzizalisha na badala yake kuzielekeza kwenye uwekezaji wenye manufaa ya muda mrefu.

Tukio hilo liliongozwa na msimamizi wa kimataifa, Georgie Ndirangu, ambaye pia alitoa hamasa kwa wanawake kwa kuwajengea uwezo wa kukuza vipato vyao.

Katika mkutano huo pia kulikuwa na vipindi vya mchana vinavyoongozwa na wataalam katika vikundi vidogo, vilifanyika kwa ushirikiano na Alliance Life Assurance na  Tanzania Securities Limited.

Wengine ni  UTT Asset Management ambapo kila kikao kilitoa fursa kwa washiriki kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwa wataalam wa bima, uwekezaji na mipango ya kifedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *