
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, amesema Iran haitakubali kamwe masharti ya kujisalimisha yanayotolewa na Marekani na Israel, na itaendelea kupigana hadi ipate ushindi.
Katika ujumbe uliotolewa Jumapili kuadhimisha siku ya 30 ya kipindi cha ulinzi wa kitaifa, Ghalibaf amesifu uhamasishaji mkubwa wa wananchi, akisema uwepo wa mamilioni ya Wairanani mitaani unaonesha nguvu ya kijamii ya taifa na una mchango mkubwa katika kukabiliana na adui.
Amesisitiza kuwa umoja wa kitaifa umevuruga juhudi za maadui za kuigawanya jamii ya Iran, akiongeza kuwa badala ya taifa kusambaratika, limezidi kushikamana zaidi mbele ya shinikizo kutoka nje.
Ghalibaf amesema, “Vita vya Ramadhani sasa viko katika hatua yake nyeti zaidi,” na kuongeza, “Adui aliyedai kuwa ameangamiza vikosi vyetu vya anga, majini na makombora alikuwa na mpango wa kuuangusha Jamhuri ya Kiislamu. Sasa ameelekeza macho yake kwenye kufungua Lango‑Bahari la Hormuz ambalo lilikuwa wazi kabla ya ‘Vita vya Ramadhani’, lakini leo ni lengo kuu la kioperesheni la Trump.”
Spika wa Bunge la Iran amesema kuwa ingawa Marekani inaonesha hadharani nia ya mazungumzo, wakati huohuo inaendeleza mipango ya uvamizi wa nchi kavu. Ameonya kuwa vikosi vya Iran viko tayari kwa hali kama hiyo na vitatoa majibu ya haraka na madhubuti.
Alisisitiza, “Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu Mtukufu, hatutatoka katika vita hivi ila kwa ushindi na dalili zake tayari zinaanza kuonekana. Hatutaruhusu maadui kujiondoa vitani bila kuimarisha mamlaka na nguvu ya Iran. Tutageuza vita hivi kuwa funzo kubwa kwa yeyote atakayefikiria kufanya uchokozi.”
Ghalibaf amesema nguvu ya Marekani imepata pigo kubwa sambamba na kuimarika, Kambi ya Muqawama.
Aidha amesema: “Trump ameshindwa kuzishawishi nchi za Ulaya. Soko la nishati limeingia katika hali ya mgogoro, na mfumuko wa bei za chakula unakaribia. Alama za nguvu ya Marekani, kuanzia ndege za kivita za F‑35 hadi manowari za kubeba ndege na kambi zake za kijeshi katika eneo, zimepata mapigo makubwa. Mashambulizi dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yamekuwa yenye ufanisi, usahihi, na yenye athari za msingi.”
Ameongeza, “Hizbullah nchini Lebanon, ambayo ilikuwa ikitishiwa mara kwa mara kupokonywa silaha, leo ni sehemu muhimu na yenye nguvu ya kambi ya muqawama na imeuweka utawala huo dhalimu katika mtego. Muqawama wa Iraq unapigana kwa ujasiri na umemshangaza adui. Nchini Yemen Harakati ya Ansarullah imehuisha safu ya muqawama kwa ushiriki wake na iko tayari kuleta mshangao mkubwa.
Ameongeza kuwa: “Operesheni zetu zinaendelea. Makombora yetu yako katika hali kamili ya utendaji. Azma na imani yetu imeongezeka. Tunafahamu udhaifu wa adui na tunaona wazi dalili za hofu na taharuki ndani ya safu zao.”
Marekani na utawala wa Israel walianzisha uchokozi wao wa pamoja wa kijeshi dhidi ya Iran tarehe 28 Februari sawa na tarehe 10 ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na hivyo vita hivyo sasa ni maarufu kama ‘Vita vya Ramadhani.”